Vigoma vya Keko hatari, hiyo misosi yake sasa

Muktasari:

Gazeti hili lilifuatilia kwa ukaribu mashindano hayo na leo linakuletea tathmini ya jumla baada ya kuhitimishwa kwake rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mashindano ya Sports Extra Ndondo Cup yamemalizika Jumapili iliyopita huku timu ya UV Temeke ikiibuka bingwa kwa kuichapa timu ya Uruguay kwa mikwaju ya penati 5-3.

Mechi hiyo ililazimika kuamriwa kwa mikwaju ya penati baada ya timu hizo kupata matokeo ya sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Bandari na Utalii, Tandika, Dar es Salaam.

Gazeti hili lilifuatilia kwa ukaribu mashindano hayo na leo linakuletea tathmini ya jumla baada ya kuhitimishwa kwake rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Historia kuwahukumu UV Temeke?

Kwa kutwaa ubingwa huo, UV Temeke inakuwa ni timu ya sita kufanya hivyo tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 2014 yakihusisha timu za soka kutoka mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Tangu yaanzishwe hakuna timu iliyotwaa taji la mashindano hayo mara mbili na pia kuingia hata hatua ya fainali.

Mwaka 2014, bingwa alikuwa Abajalo akafuatiwa na Faru Jeuri kisha Temeke Market. Mwaka 2017 walichukua Misosi FC na mwaka jana walibeba Manzese United.

Baada ya UV Temeke kutwaa ubingwa huo wengi wanajiuliza je itavunja mwiko wa mabingwa kutotamba tena au wataendeleza nuksi ya muda mrefu kwa timu zinazochukua kombe hilo?

Pacha wa Msuva anatisha

Nyota wa JKT Tanzania, Abdulrahman Mussa aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kupachika jumla ya mabao 14, idadi iliyokuwa sawa na ile ya Saimon Msuva ambapo kila mmoja alipewa zawadi ya Ufungaji Bora.

Baada ya kushindwa kutamba tena kwenye Ligi Kuu kwa misimu miwili iliyofuata, Mussa ameibukia kwenye Ndondo Cup ambako amekuwa mfungaji bora, akipachika jumla ya mabao manne ambayo ameyafunga akiwa na kikosi cha Toroli Kombaini.

Aliyeshika nafasi ya pili kwa ufungaji mabao ni Sultan Kasikasi wa Misosi FC na Saad Kipanga wa Opec ambao kila mmoja amepachika mabao matatu wakati wachezaji Moses Kitandu wa Uruguay pamoja na Salum Kihimbwa wa Banda FC kila mmoja amefunga mawili.

Vita ya Keko ilibamba

Kama kuna mambo yaliyonogesha mashindano ya Ndondo Cup mwaka huu ni utani wa jadi na upinzani uliohusisha timu tatu zinazotoka eneo la Keko ambazo ni Ninga FC, Toroli Kombaini na Keko Furniture.

Kutokana na umati wa mashabiki na shamrashamra ambazo vikundi vya ushangiliaji ambavyo timu hizo zilikuwa nazo, mechi hasa zile zilizozikutanisha zilikuwa na msisimko wa aina yake na zilijaza idadi kubwa ya mashabiki.

Vita ya Keko ilianzia kwenye kundi A ambako timu ya Toroli FC iliichapa Keko Furniture kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya kwanza ya mashindano hayo.

Lakini baadaye Ninga wakaja kuzima ubabe wa Toroli kwa kuichapa kwa mikwaju ya penati 4-2 kwenye mechi ya hatua ya robo fainali baada ya timu hizo kwenda sare ya bila kufungana katika dakika 90 za mchezo.

Temeke, Ubungo zinatisha

Wilaya za Ubungo na Temeke kila moja imetwaa ubingwa wa mashindano hayo mara mbili zikifuatiwa na Kinondoni na Ilala ambazo zenyewe kila mmoja imebeba mara moja tangu yalipoanzishwa.

Kwa upande wa Temeke, timu zilizotwaa ubingwa ni Temeke Market na UV Temeke wakati kwa Ubungo ni Manzese United na Misosi FC.

Ilala iliwakilishwa vyema na Faru Jeuri ya Vingunguti ambayo ilitwaa ubingwa huo mwaka 2015 na Kinondoni ilitolewa Kimasomaso na mabingwa wa kwanza wa Ndondo Cup, timu ya Abajalo.

Ni wilaya moja tu ya Kigamboni ambayo tangu maahindano hayo yaanzishwe, hakuna timu yake iliyowahi kutwaa taji.

Ndondo Food ilibamba

Imezoweleka kuona vyakula mbalimbali vikiuzwa kwenye mechi za mashindano ya Ndondo Cup kama vile mihogo mibichi, karanga na uji.

Mashindano ya mwaka huu yalikuwa na kitu cha ziada ambapo chakula aina ya wali uliokuwa na mboga ya nyama, maharage na majani ambacho kilichangamkiwa vilivyo na mashabiki wa soka.