Vifaa 10 vinavyotikisa usajili Ulaya

Muktasari:

Manchester United  wanahitaji  kuongeza beki wa kati katika kikosi chao  na baada ya kukwaa kisiki kwa nahodha  wa Ajax Amsterdam, Matthijs de Ligt, sasa anayetupiwa jicho la karibu ni  Harry Maguire.

London, England. Mastaa mbalimbali duniani wameanza kurejea katika klabu zao ili kuanza maandalizi  ya msimu ujao, lakini makocha wanahaha kuboresha vikosi vyao kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.

Klabu za Ligi Kuu England zimebakiza mwezi mmoja tu kumaliza uboreshaji wa vikosi vyao na vigogo kama, Manchester United, Tottenham Hotspurs , Arsenal, Liverpool, Manchester City viko mawindoni kuwania saini za mastaa wapya.

Ipo idadi kubwa ya wachezaji ambao wameonyesha makali katika Fainali za Afrika akiwemo Wilfried Zaha wa Ivory Coast anayehusishwa na Arsenal.

Kwa namna tetesi zinazoendelea za usajili wachezaji hawa 10 muda wowote uhamisho wao unaweza kukamilika kabla ya kufungwa dirisha hili la usajili majira ya kiangazi.

Wilfried Zaha (Arsenal)

Winga wa Crystal Palace ni mchezaji ambaye yupo katika rada za Arsenal  na mwishoni mwa msimu aliweka wazi dhamira ya kutaka kuondoka kwenye klabu yake kwa lengo la kutaka kwenda kuanza maisha mapya ya soka sehemu nyingine.

Palace ilizigomea Pauni40 milioni za Arsenal na huenda Kocha Unai Emery anaweza kupima kina cha maji kwa kutuma ofa nyingine ili kuishawishi klabu yake imuiachie mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast.

Dani Ceballos   (Tottenham)

Hakuna uwezekano wa kinda Dani Ceballos   ambaye ni kiungo kusalia Real Madrid hivyo alikuwa akihusishwa na  kujiunga na  Tottenham iliyocheza Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.

Ceballos ambaye anahitaji sehemu atakayopata nafasi ya kucheza, alifanya vizuri mwezi uliopita  katika mashindano ya Ulaya kwa vijana chini ya umri wa miaka 21 akiwa na timu yake ya taifa  Hispania.

Kocha wa Tottenham,  Mauricio Pochettino anapambana kiungo huyo ili achukue nafasi ya Christian Eriksen ambaye hata kama asipoondoka kipindi hiki anaweza kutimka katika dirisha dogo Januari, mwakani.

Harry Maguire  (Manchester United)

Manchester United  wanahitaji  kuongeza beki wa kati katika kikosi chao  na baada ya kukwaa kisiki kwa nahodha  wa Ajax Amsterdam, Matthijs de Ligt, sasa anayetupiwa jicho la karibu ni  Harry Maguire.

 Mchezaji huyo wa kimataifa wa  England, inadaiwa klabu yake ya Leicester  City  haipo tayari kumwachia kwa dau ambalo litakuwa chini ya  Pauni80 milioni.

Kocha wa  Manchester City,  Pep Guardiola naye anammezea mate beki huyo  ili awe mrithi wa  Vincent Kompany  ambaye mwishoni mwa msimu uliopita alitangaza kuondoka Etihad.

 

Nicolas Pepe  (Liverpool)

Kuongeza upana wa kikosi chao, majogoo wa Liverpool wapo kwenye mchakato wa kuhakikisha wanapata saini ya nyota huyo wa Lille ya Ufaransa.

Rais wa Lille, Gerard Lopez  alisema   Liverpool imeanza mazungumzo na wakala wa Pepe ili kumng’oa mshambuliaji huyo.

Maxi Gomez  (West Ham)

Baada ya kufunguliwa mlango wa kutokea, Marko Arnautovic macho yote yameelekezwa  kwa mabadala wake ambaye anatajwa kuwa ni Muaustria, Maxi  Gomez  ambaye huenda akatua kwa wagonga nyundo hao wa Jiji la  London.

Akiwa na  Celta Vigo ya Hispania, mshambuliaji huyo amefunga mabao 30 katika mechi   70 za  Ligi Kuu nchini humo ambayo ni maarufu kama La Liga.

Kurt Zouma (Everton)

Kiwango alichokionyesha msimu uliopita akiwa kwa mkopo Everton ndicho kinachoisukuma klabu hiyo kuwa na mipango ya kumsajili beki huyo endapo asipokuwa kwenye mipango ya Frank Lampard msimu ujao wa majira ya kiangazi.

 Kieran Tierney  (Arsenal)

Arsenal wapo kwenye vita ya kumsajili beki  wa kushoto kutoka Scotland, Kieran Tierney  kwenye klabu ya Celtic kwa ada ya uhamisho inayokaribia Pauni 15 milioni.

Ryan Sessegnon  (Tottenham)

Nyota wa kimataifa wa timu ya England chini ya miaka 21, Ryan Sessegnon anayecheza, Fulham ya  daraja la kwanza  anamnyima usingizi Kocha wa  Tottenham,  Mauricio Pochettino.

Bruno Fernandes  (Man United)

Sporting Lisbon imeripotiwa  kutaka Pauni  70milioni ili kumwachia  kiungo wao, Bruno Fernandes  ambaye anatajwa kama akijiunga na mashetani hao wekundu atakuwa akivuta Pauni  100,000 kwa wiki kama mshahara wake.

 Nathan Ake (Manchester City)

Guardiola amekuwa akivutiwa kwa ukaribu na  beki wa kati wa Bournemouth, Nathan Ake mwenye uwezo pia wa kucheza kama kiungo mkabaji, beki huyo raia wa Uholanzi anatajwa kuwa atamgharimu Paundi 40 milioni katika kipindi hiki.