Vibonde presha juu Ligi Kuu

Wednesday July 8 2020

 

By Oliver Albert

Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikitarajiwa kuendelea leo, presha kubwa ipo kwa timu ambazo zinapambana ili zisishuke daraja.

Timu hizo zaidi ya saba, kila moja itakuwa na harakati za kuchanga vyema karata zake, ili mkosi wa kushuka daraja usizikute mwishoni mwa msimu kama ilivyokuwa kwa Singida United.

Singida United yenye pointi 15 imeshashuka daraja hivyo zinasubiriwa timu tatu zitakazoungana na 'walima alizeti' hao kushuka moja kwa moja na mbili nyingine ambazo zitacheza hatua ya mtoano na akama zitapoteza mechi hizo zitashuka daraja.

Timu nyingine zilizo katika hatari ya kushuka daraja ni Mbao yenye pointi 32, Mbeya City (33), Ndanda (36), Alliance (37), Lipuli(37)  na Mtibwa Sugar yenye pointi 38.

KMC na Mwadui zenye pointi 40 kila mmoja nazo haziko sehemu salama hivyo zinatakiwa kuchanga karata zake vizuri ili ziendelee kusalia kwenye ligi msimu ujao.

KMC leo Jumatano itacheza na Singida United kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Mbeya City itaikaribisha Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Mbao itapambana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Nyamagana Mwanza, Ndanda itaikabili JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara wakati Mwadui itakuwa ugenini Chamazi kucheza na Azam.

Advertisement

Mbeya City inatakiwa kutumia vema uwanja wake wa nyumbani leo kwa kupata pointi kwani kama itapoteza itazidi kujiweka katika mazingira magumu zaidi ya kubaki msimu ujao kwa sababu mechi nyingine nne zote zitakazofuata itacheza ugenini.

Baada ya mchezo wa leo, Mbeya City itakuwa na michezo dhidi ya  Ndanda,Azam, KMC na Namungo ambayo yote itafanyika ugenini na ugumu zaidi ni kwamba inakutana na timu ambazo nazo zinapambana kujinasua na janga la kushuka daraja, Ndanda na KMC  wakati Azam inawania nafasi ya pili kwenye ligi.

Kocha wa Mbeya City, Amri Said amekiri wana kazi kubwa kuweza kuvuka mlima ulio mbele yao lakini anaamini hakuna kinachoshindikana kwa Mungu na muhimu ni wao kuendelea kupambana na kufanya vizuri katika mechi zao na mwesho mbivu na mbichi zitafahamika.

"Si kazi rahisi kwa nafasi tuliyonayo lakini muhimu ni kuhakikisha tunakomaa na kuweza kupata matokeo mazuri katika michezo iliyo mbele yetu na mwisho wa msimu tutajua tutakuwa katika nafasi gani,"alisema Amri.

Kwa upande wa KMC haiko pabaya sana na  ushindi wa mechi mbili tu utawahakikishia nafasi ya kuendelea kubaki kwenye ligi kwani itafikisha pointi 46 lakini inapaswa iombee Mbao na Mbeya City zipoteze mechi moja moja na timu mbili kati ya  Ndanda, Alliance na Lipuli zipoteze mechi mbili tu ili yenyewe iwe salama zaidi.

Mbao ambayo tangu ujio wa kocha Fred Felix Minziro imeonekana kung'ara baada ya kushinda michezo mitatu mfululizo inatakiwa kufanya kazi kubwa sana ili ibaki msimu ujao kwani ina mechi ngumu mbele yake baada ya mchezo wa leo.

Timu hiyo ina mchezo miwili ugenini dhidi ya Simba na JKT Tanzania ugenini na itakuwa na miwili nyumbani dhidi ya Namungo na Ndanda ambayo hata ikishinda yote  pamoja na wa leo dhidi ya Mtibwa itafikisha pointi 50 lakini itabaki ligi kuu endapo Mbeya City, Ndanda,Alliance  na Lipuli zitapoteza michezo miwili miwili.

Kocha wa Mbao Fred Minziro amesema wamejiandaa kufanya vizuri katika mchezo wa leo na mingine yote iliyo mbele yao.

"Tumejiandaa vizuri dhidi ya mchezo huo. Tunajua tunakutana na timu nzuri na ngumu lakini malengo yetu nni kuendeleza kasi yetu ya ushindi nyumbani.

Tunataka kushinda mchezo huu na mingine ijayo ili tuone jinsi gani tunaweza kujinasua na janga la kushuka daraja,"alisema Minziro.

Advertisement