Viashiria 7 vya kufeli kwa TFF ya Rais Karia

Muktasari:

  • Ikiwa ukaribia mwaka wa sasa tangu Shirikisho la Soka (TFF) liwe chini ya Rais, Wallace Karia, mambo mengi yametokea. Kwa bahati mbaya mabaya yamekuwa mengi kuliko mazuri. Makala haya yanazungumzia viashiria saba vinavyoonyesha kuwa TFF ya Karia ilivyochemsha mapema ikiwa katikati ya safari yao.

HAKUNA kazi ngumu kama kuongoza. Kuongoza ni kipawa na sio utashi wa mtu. Ni kazi ngumu inayohitaji utulivu, weledi na busara ya hali ya juu. Ndio maana wale waliojaribu kulazimisha kuongoza huku wakijua hawana kipawa hicho waliishia wakifeli.

Ugumu wa kuongoza taasisi inayohusisha watu kama masuala ya siasa, michezo na mengine ni kazi ngumu zaidi. Ndiyo sababu baadhi ya watu wanaojitambua huachia ngazi kwa hiari yao pale wanapoona jahazi limewashinda. Huo ndio uungwana.

Nani asiyekumbuka aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismael Aden Rage aliamua kuachia ngazi baada ya kuiongoza timu hiyo kwa miaka minne tu. Kwanini hakutaka kuongeza muhula mwingine. Miaka minne ilitosha kumpa darasa, licha ya kupawa alichonacho. Hali kama hiyo pia iliwafanya Yusuf Manji na aliyekuwa Makamu wake kujiuzulu Yanga. Ipo mifano mingi ya maana.

Ikiwa ukaribia mwaka wa sasa tangu Shirikisho la Soka (TFF) liwe chini ya Rais, Wallace Karia, mambo mengi yametokea. Kwa bahati mbaya mabaya yamekuwa mengi kuliko mazuri. Makala haya yanazungumzia viashiria saba vinavyoonyesha kuwa TFF ya Karia ilivyochemsha mapema ikiwa katikati ya safari yao.

RATIBA YA OVYO

Unaweza kumsifu Kinyonga kwa kubadilika rangi mara nyingi? Kama jibu lake ni ndio utakuwa hujaiona ratiba ya Ligi Kuu Bara inayosimamiwa na TFF pamoja na Bodi ya Ligi.

Ratiba hiyo inabadilika kiasi hata Kinyonga akitaka kwenda na mabadiliko hayo anaweza kufa. Kwa msimu huu pekee ratiba hiyo imebadilika zaidi ya mara nane.

Ilianza kubadilika tangu ligi ilipoanza msimu yaani Agosti mwaka jana, kisha kubadilika na kubadilika kwa kisingizo hiki na kile.

Yaani TFF ya Karia na TPLB inayosimamia ligi hiyo, ilikuwa ikiendelea kuibadili ratiba hiyo kwa kadiri walivyojisikia.

Ilibadilika Novemba, Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili na hata tukiwa Mei, sio ajabu kusikia ikibadilika tena. Mara nyingine ilibadilika hadi mara tatu kwa mwezi mmoja. Hii ni ishara tosha ya utawala mbovu na usiojitambua. TFF inawekaje mechi za Ligi Januari 1-12 wakati inafahamika wazi kwamba kuna michuano ya Kombe la Mapinduzi? Inawekaje mechi siku ya mechi za kalenda ya CAF na FIFA? Huku ni kutokujielewa.

VIPORO VYA KUMWAGA

Kwa umri wangu huu wa kufuatilia soka, sijawahi kuona Ligi ya nchi moja, klabu moja inakuwa na viporo zaidi 10. Sijawahi, ila katika TFF ya Karia nimeona na kunistaajabisha sana.

Simba iliyokuwa ikiiwakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa na viporo vingi na hata sasa bado inavyo vya kutosha.

Kisingizio ni ushiriki wake wa michuano hiyo, lakini katika kundi lao ilipangwa na Al Alhy ya Misri, AS Vita ya DR Congo na JS Saoura ya Algeria, lakini timu hizo kwao hazikuwa na viporo vingi.

Timu hizo zilipisha mechi kati ya mbili hadi nne na timu shiriki za ligi zao, lakini kwa Simba ushiriki wake wa CAF ilikuwa kama ishu kubwa, mabosi wao walikuwa wakipiga simu tu kwa wanene wa TFF na kuomba mechi zao ziahirishwe. Viporo hivyo vimeitia doa TFF ya Karia kwani haijawahi kutokea hali hiyo licha ya kila mwaka na misimu yote Tanzania kuwakilisha na timu Afrika.

Hiki ni kiashiria cha pili kwa TFF ya Karia kuchemsha kwani ni kama waliitengenezea Simba ubingwa mapema msimu huu. Hili ni tatizo na TFF na TPLB haiwezi kukwepa mzigo wa lawama.

UBOVU WA WAAMUZI

Hapa ndipo utakapotambua kuwa TFF ni kichwa cha mwendawazimu. Mwamuzi anafanya madudu uwanjani mbele ya Rais wa TFF, Wallace Karia na watendaji wake, lakini hakuna kinachofanyika. Licha ya kuona madudu hayo utawakuta wanasubiri taarifa ya Kamisaa wa mechi eti ndipo wafanye maamuzi, ujinga ulioje. Kama refa ana maelekezo na kamisaa pamoja na washika vibendera nao watakuwa na maelekezo pia. Unahitaji kuona nini tena ili kufanya maamuzi wakati mambo yote yalikuwa wazi uwanjani.

Hali hii imesababisha waamuzi kuendelea kufanya madudu na kuharibu ladha ya ligi. Mechi nyingi zimekuwa na madudu ya wazi, ilianza kitambo lakini kwa karibuni ni ile ya Yanga na Mtibwa Sugar zikafuata nyingine ikiwamo ya Simba na KMC.

TFF imechemka katika hili, japo iliamua kuwatoa kafara Abdallah Kambuzi na wenzake kabla hata haijapokea ripoti ndani ya muda.

KUSHUKA KWA MAPATO

Mapato ya mlangoni katika mechi za ligi msimu huu yameshuka vilivyo. Prisons na Biashara United zimewahi kuingiza Sh 9,000 na ulipotembezwa mgao ilikuwa aibu kubwa. Mashabiki wamekauka viwanjani, kwa vile hawajui ratiba zilivyo, kwani unaweza kulala ukijua mechi inachezwa leo, kisha asubuhi ukasikia haipo.

Mechi ya kwanza ya Yanga na JKT Tanzania ilibadilishwa uwanja na muda zaidi ya mara tatu kiasi cha kuwatia mashabiki kizunguzungu. Mara itapigwa Mkwakwani, Tanga ghafla ikahamia Uwanja wa Taifa, huo muda nao ulikuwa utata, mara saa 8 mchana, ghafla saa 1 usiku kisha saa 10 jioni kiasi Kocha Mwinyi Zahera aliwachezesha vijana wake na njaa na kuishia kulalama tu.

KUKOSEKA MDHAMINI MKUU

Mpaka sasa Ligi Kuu Bara ikiwa inaelekea ukingoni, klabu shiriki hazina uhakika wa zawadi za msimu. Hii ni kwa sababu TFF ya Karia ilishindwa kupata Mdhamini Mkuu wa Ligi hiyo na kuishia kupiga danadana kwamba atapatikana, lakini hadi sasa hakuna.

Kukosekana kwa mdhamini kumetokana na Kampuni ya Vodacom kutoongeza mkataba baada ya miaka mitatu ya udhamini wake kumalizika na kuelekezwa kulikuwa na figisufigisu zilizowachosha.

Inasikitisha Ligi Kuu kukosa mdhamini na TFF wala haishtuki ilihali wanajua klabu nyingine shiriki hazina uwezo wala wadhamini wa kuzipiga

Ila mbaya ni kwamba hata bingwa hajui itavuna nini katikati ya ukata huo. Hii ni moja ya dalili za kuchemsha kwa TFF ya Karia.

KUFUNGIA WADAU OVYO

Enzi za utawala wa Jamal Malinzi, Rais huyo alilalamikiwa kwa kitendo chake cha kumfungia miaka saba Wakili wa kujitegemea Damas Ndumbaro aliyekuwa akifanya shughuli zake nyingi na Simba kwa kukataa wizi waliotaka kufanyiwa klabu kwa kukatwa buku moja (Sh 1,000) katika kila tiketi waliyokuwa wakiuza.

Lakini TFF ya Karia imetia fora kwa kufungia kila ambaye amekuwa yupo tofauti na mtazamo wa TFF hiyo. Orodha ni ndefu, lakini kati ya dalili za kiongozi aliyechemsha ni kutokubali uhuru wa mawazo, ilihali hata mapacha wa tumbo moja nao utofautiana.

KUMTEMA KOCHA KIM

Sawa Taifa Stars imefuzu Fainali za Afcon 2019, lakini kila mtu anajua Uganda ilikuja Tanzania kukamilisha ratiba tu, lakini ukitaka kujua TFF ya Karia imechemsha ni jinsi ambavyo ilivyofanya mabadiliko ya Kurugenzi ya Ufundi.

Ilimtoa Salum Madadi na kumpa Oscar Mirambo kisha kumtoa na kumpa kocha aliyefeli mapema na Kilimanjaro Stars, Ammy Ninje, huku kule kwa vijana wakimtimua Mshauri wa Ufundi kwa soka la vijana, Kim Paulsen.

Madhara ya Kim kuondolewa ni kufanya vibaya kwa Serengeti Boys katika Fainaliza za Afcon U17 zilizofanyika kwa mara ya kwanza katika ardhi ya Tanzania.

Hakuna asiyejua ufundi wa Kim, lakini uswahiba unaoendelea ndani ya TFF ya sasa iliamua kuachana na watu makini ili kuwapa kazi washkaji zao na mwishowe tumeambulia aibu.

Timu zote kuanzia ya Taifa Stars, Ngorongoro Heroes hadi Serengeti Boys zimekuwa zikiteuliwa kwa mazoea, huku kule U17 Kocha Mirambo ana wachezaji wake, Minje kadhalika na hata mabosi wa TFF nao wlikuwa na wachezaji wao. Aibu tupu. Hivyo ni kati ya viashiria vichache vya kuchemsha kwa TFF hii ya Karia.