VIDEO: Taifa Stars ushindi upo hapa

Muktasari:

Tanzania inahitaji ushindi katika mchezo wa leo dhidi ya Cape Verde ili kurudisha matumani yake ya kusaka kufuzu kwa AFCON mwakani Cameroon

Dar es Salaam.Achana na matokeo ya mchezo wa kwanza Taifa Stars ilipoteza 3-0 dhidi ya Cape Verde, hayo weka mfukoni kisha angalia leo mtu anavyokufa pale kwenye Uwanja wa Taifa.

Katika mchezo huu Stars wana kila sababu ya kushinda kutokana na kwamba wachezaji na benchi la ufundi wanajua wapi walipokosea, lakini vile vile wapo katika uwanja wa nyumbani.

Ukiliangalia Kundi L siyo kundi gumu ambalo linaweza likafanya Stars ishindwe kushika nafasi ya pili, lakini kinachohitajika kuipa safari ni ushindi katika mchezo wa leo.

Mwanaspoti limeangazia baadhi ya vitu ambavyo vinaweza vikaipa ushindi wa mapema Stars katika mchezo huu utakaopigwa leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa.

MASHABIKI KUUNGA MKONO

Mashabiki wa kitanzania wanakuwa na moyo mwepesi mno pale panapokuwa na matokeo mabovu, katika mchezo wa kwanza tu tayari kulishaanza kuwa na matabaka ya watu wanaoiunga mkono Stars wengine wakijitoa kabisa katika kuunga mkono.

Njia nyepesi ni leo mashabiki wote kuungana kwa pamoja na kuweka tofauti zetu pembeni kisha kuishangilia Stars kwani wachezaji wakivunjwa moyo wakiwa uwanjani haitopendeza.

Ushabiki wa klabu unabidi uwe pembeni katika mchezo huu, badala yake jezi zenye rangi ya kijani ndio zitawale katika majukwaa na hiyo itakuwa neema kwa benchi yetu.

MAGOLI YA MAPEMA

Katika mchezo wa kwanza Cape Verde iliweza kucheza vizuri karata zao baada ya kufunga magoli mawili ya haraka na kuwavuruga vilivyo wachezaji na benchi la Stars.

Magoli yale yaliwafanya Stars washindwe kujipanga vizuri kwasababu wenzao walikuwa wamewaotea, hivyo hata Stars katika mchezo huu wanabidi wapate magoli ya mapema ambayo yatawalinda.

Kupata magoli kwa Stars kutawafanya hata kuwa sehemu nzuri katika msimamo wa kundi, ikiwa kama wamepata pointi katika mchezo huu.

MABADILIKO SAFU YA ULINZI

Safu ya ulinzi katika mchezo wa kwanza dhidi ya Cape Verde, Stars ilionekana kukatika mara kwa mara na washambuliaji wa Cape Verde walikuwa hawana kazi ngumu.

Ilikuwa ni rahisi mno kuingia katika 18 ya Stars kwasababu mabeki walikuwa kama wamechoka na ilikua ngumu kucheza kwa kufuatana (Man to Man) katika mchezo huu.

Amunike anaweza akafanya kitu katika kikosi cha leo kitakachoshuka katika uwanja wa Taifa kukipiga na Cape Verde.

USHAMBULIAJI PANOGA

Kuingia kwa John Bocco katika mchezo uliopita, alionyesha Dhahiri kwamba alikuwa anakaa nje kwa bahati mbaya, inawezekana kwasababu kocha Emmanuel Amunike alikosa kumuona vizuri katika mazoezi yake kutokana na muda kuwa mdogo.

Lakini kukosekana kwa Thomas Ulimwengu katika mchezo huu kunaweza kukatoa nafasi ya Bocco kuanza, amekua na historia nzuri ya kutupia akiwa uwanja wa Taifa.

Hata kwa upande wa Samatta pia itakuwa ni njia nyepesi kwake kufanya vizuri kwasababu uwanja wa Taifa anaufahamu, hivyo kazi ni nyepesi kwake kufunga tu.

NYASI HALISI KUIBEBA STARS

Wachezaji wa Tanzania wote wamezaliwa hapa hapa, viwanja vyao walivyozoea kuchezea ni michangani, mabonde na milima, kwahiyo wanapokuwa wanaenda katika viwanja vya nyasi bandia kunakuwa na mtihani kidogo kama ilivyokuwa Cape Verde.

Jinsi walivyocheza Uganda ni tofauti na walivyocheza Cape Verde, kwasababu viwanja vya sehemu hizi ni tofauti, Uganda nyasi halisi na Cape Verde nyasi bandia.

Leo Stars wapo katika uwanja ambao wachezaji wote wameshaucheza kwa muda mrefu na wameuozoea hivyo itakuwa kazi nyepesi mno kuamua ushindi katika mchezo huu.