VIDEO: Ligi Kuu kuchezwa kwa vituo

Friday May 22 2020

By Charles Abel

Mechi zilizobakia za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Ligi Daraja la Pili (SDL) na Kombe la Azam Sports Federation, zitachezwa kwa mtindo wa vituo.
Uamuzi huo umetangazwa siku moja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kutangaza kuruhusu kurejea kwa shughuli za michezo kuanzia Juni Mosi mwaka huu.
Akizungumza jijini Dodoma leo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alisema kuwa mashindano hayo yatachezwa katika vituo viwili ambavyo ni Dar es Salaam na Mwanza.
"Kufuatia michezo kuruhusiwa na Mhe. Rais John Magufuli,Tunaruhusu Ligi Kuu,Ligi daraja la kwanza na la pili pamoja na Kombe la  Shirikisho (Azam Federation Cup) kuendelea ili tupate bingwa pamoja na Mwakilishi katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Viwanja vitakavyotumika  kwenye Michezo inayotarajiwa kufunguliwa juni mosi,2020 ni Viwanja vya Taifa,Uhuru na Chamazi kwa Ligi Kuu, na Viwanja vya CCM Kirumba na Nyamagana vya Jijini Mwanza kwa Ligi daraja la kwanza na la pili" Dk. Mwakyembe.
Ligi Kuu Tanzania Bara yenyewe imebakiza raundi tisa ingawa zipo timu zilizocheza idadi ndogo ya mechi kulinganisha na nyingine wakati Ligi Daraja la Kwanza imebakiza raundi nne.
Upande wa Ligi Daraja la Pili yenyewe imebakiza raundi moja ya hatua ya makundi kabla ya kuingia katika hatua ya 6 bora kupata timu tatu nne zitakazopanda Ligi Daraja la Kwanza.
Waziri Mwakyembe alisema kuwa uamuzi huo umetolewa baada ya tathmini ya kina iliyofanywa na timu ya wataalam.
"Baada ya mkuu wa nchi kuelezea kwamba ana nia ya kuruhusu baadhi ya shughuli za jamii kuendelea kufanyika, sisi wizara haraka kabisa tukaanza vikao vya kujiandaa. Je mkuu wa nchi akisema tunaanza wiki ijayo tunafanyaje
Tulikaa vikao na mimi nikawapa wataalamu wangu hadidu za rejea.Kwanza watambue kwamba klabu zetu za mpira ziko hoehae kiuchumi.
Ule utaratibu wa zamani timu inatoka Songea kwenda Mara na baada ya hapo kwenda kwingine hawatoweza lazima tulitambue kwa sababu hawana kipato, ligi ilisimama na wakawa wanalipa wachezaji," alisema Dk. Mwakyembe.

Advertisement