VIDEO: Ajibu noma sana!

Muktasari:

IBRAHIM Ajibu amehusika na mabao nane kati ya 11 ya Yanga, lakini bao alilofunga jana dhidi ya Mbao FC lilikuwa la aina yake kwani limefuata mabao makali yaliyowahi kufungwa na nyota mbalimbali wa kimataifa akiwamo Wayne Rooney, Zlatan Ibrahimovic na Cristiano Ronaldo.

Dar es Salaam. UNALIKUMBUKA lile bao alilowahi kufunga nyota wa zamani wa Man United, Wayne Rooney katika mechi yao dhidi ya Man City iliyopigwa Mei 4, 2012 na kushinda Bao Bora la msimu? Sasa bao hilo lilifungwa usiku wa jana na Ibrahim Ajibu 'Akadabra'.
Ndio, Ajibu ambaye ameendelea kuwapa raha mashabiki wa Yanga, alifunga dakika za nyongeza za pambano lao dhidi ya Mbao FC na kuwafumua Wauza Mbao hao wa jijini la Mwanza kwa mabao 2-0 lililopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na kuipeleka timu hiyo nafasi ya pili kutoka nafasi ya saba katika Ligi Kuu Bara.


Ajibu aliyehusika katika bao la kwanza lililofungwa kipindi cha kwanza na Rafael Daud kwa kichwa, alifunga bao hilo la kideoni akiunganisha mpira uliookolewa vibaya na beki wa Mbao, Amos Charles aliyeokoa krosi ya Gadiel Michael.
Bao hilo la Ajibu linafanana pia na lile alilowahi kufunga Zlatan Ibrahimovic alipokuwa akiichezea Sweden.
Akiwa katika utulivu, straika huyo alibinjuka tiktak na kupiga mpira uliomshinda kipa Hashim Mussa, bao lililowainua vitini mashabiki wa Yanga, waliokuwa na presha baada ya kipa Beno Kakolanya kutumia na kutolewa, nafasi yake kuchukuliwa na Klaus Kindoki.


Lilikuwa ni shambulizi la ghafla ambalo Yanga lilifanya baada ya kupokonya mpira kwa Mbao na Gadiel alikimbia nao upande wa kushoto na kupiga krosi hiyo iliokolewa  na kabla haujatua, Ajibu alijipindua vyema na kubinuka tik tak hiyo iliyozaa bao.
Furaha ya bao hilo tamu, lilimfanya Ajibu kushangilia kwa kuivua jezi na kulimwa kadi ya njano. Bao hilo ni la pili kwa Ajibu msimu huu, lakini likimfanya afikishe idadi ya mabao nane aliyohusika nayo msimu huu kati ya mabao 11 ambayo Yanga imefunga katyika Ligi Kuu, huku Yanga ikipanda hadi nafasi ya pili nyuma ya kinara Mtibwa Sugar.
Ajibu aliyetua Yanga msimu uliopita akitokea Simba, ametoa pasi ya mabao sita katika mechi sita walizocheza mpaka sasa, huku akizidi kuwadhihirishia mashabiki kuwa, Kocha Mwinyi Zahera amemrejesha kwenye kiwango chake.


Ajibu alimshukuru Mungu kwa kuweza kufunga bao hilo ambalo linaweza kuwa kali mpaka sasa msimu huu, huku Amos alimsifia Ajibu kwa kutumia uzoefu wake kuwahi mpira aliokoa vijana na kufunga bao lililomsisimua hata yeye japo ameumia Mbao kulala.
Katika mchezo huo, Mbao ilionekana kushuka uwanjani kusaka matokeo ili kulinda rekodi yao ya kibabe dhidi ya Yanga, japo haijawahi kushinda jijini Dar es Salaam, hata hivyo umakini wa kipa Kakolanya na safu nzima ya Yanga iliokoa hatari zote.


Ajibu alianza kwa kupiga faulo kiufundi dakika ya 16 na Rafael kukwamisha wavuni kwa kichwa baada ya kuruka mbele ya mabeki wa Mbao, walioitungua Simba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba hivi karibuni.
Mbao iliyomiliki mpira kwa asilimia 54 dhidi ya 46 ya Yanga, itajilaumu kwa kushindwa kuopata ushindi kwa namna kipindi cha kwanza walivyotengeneza nafasi na kumiliki eneo la kati wakiwazima viungo wa Yanga, Feisal Salum na Rafael.
Miongoni mwa mashambulizi makali ambayo Mbao walipeleka langoni mwa Yanga ni lile la dakika ya 22 ambalo Herbert Lukindo na Pastory Athanas walimjaribu mfululizo kwa mashuti Beno Kakolanya ambayo yote yaliokolewa na kipa huyo.
Dakika tano baadaye, Kakolanya alifanya kazi ya ziada kuokoa mpira wa Hamim Abdulkarim ambao ulikuwa unaelekea nyavuni kwa kuupangua kwa mkono wake wa kulia kabla haujaenda kugonga mwamba na kuokolewa na mabeki wake.


Yanga ilipata pigo jingine baada ya Andrew Vincent naye kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Abdallah Shaibu 'Ninja'.
Katika hali ya kushangaza wakati Kindoki anaingia golini kuchukua nafasi ya Kakolanya, mashabiki wachache wanaokaa jukwaa la upande wa Simba huku wale wa Yanga wakionekna kuwa na wasiwasi.
Mbali na Kakolanya na Dante, Yanga pia ilimtoa Matheo Anthony na kumuingiza Thaban Kamusoko wakati Mbao iliwatoa Abubakar Ngalema, Herbert Lukindo na Said Khamis huku nafasi zao zikichukuliwa na Ngalema, Emmanuel Mtumbuka na Rayson Okello