V-Money, Jux hakuna matata

Friday July 12 2019

 

By Olipa Assa na Rhobi Chacha

NANI kakwambia msanii wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee anaumia na mpenzi wake wa zamani Juma Jux kumpata mrembo mwingine, baada ya kuachana naye, ukiwa na wazo hilo basi umechemka.

Vanessa a.k.a V-Money anayetamba na ngoma kibao kama Never Ever, Kisela na Niroge ametoka mafichoni na kuzungumza na mashabiki wake ishu nzima ya kuachana kwao.

Kwa taarifa yako tu, Vanessa ameweka wazi kwamba walishaachana na Jux zaidi ya miezi tisa, akifichua kilichowafanya wasiweke wazi kuvunjika kwa uhusiano wao kuwa ni biashara ambazo walizokuwa wanazifanya pamoja pia kuhofia kuwachanganya mashabiki wao.

Kabla ya Vanesa kufunguka ukweli ulivyo kuhusu penzi lao kuingia mchanga, Jux alionekana na mrembo mmoja wakiponda raha maeneo mbalimbali ya kula bata.

Achana na kuonekana wakiponda raha na mpenzi wake huyo mpya, pia kwenye kumbukumbu ya kuzaliwa ya Tanasha mpenzi wa Diamond, Jux akiwa anatumbuiza alimpandisha mpenzi wake huyo jukwaani huku akicheza naye.

Mashabiki wa mitandao baada ya kuona Jux kamtambulisha mpenzi wake mpya wakaanza kumtolea maneno ya karaha Vanesa ambayo yalimfanya afunguke kila kitu kupitia ukurasa wake wa Instagram.

“Mashabiki wangu naomba tubadilike kwani napenda sana mnaponiunga mkono, ilikuwa hivi mimi na Jux tuliachana zaidi ya miezi sita, tukabaki kuwa washikaji wa kutupwa na kuendelea kufanya kazi.

“Baada ya kuachana hatukutaka kukurupuka kwa sababu kuna biashara ambazo tulikuwa tunazifanya kwa pamoja, pia, hatukutaka kuwachanganya mashabiki wetu kuwaambia tumeachana halafu wanatuona muda wote tupo pamoja.

“Kuna nyimbo ambayo tumetoa pamoja inayokwenda kwa jina la Sukuma, kuna nyingine tena itatoka siyo muda mrefu, ujue mapenzi yetu yalikuwa ya maelewano sana, kuna mambo ambayo tulipishana hatukuona haja ya kuendelea.

“Nina furaha kuona Jux amepata mtu anayependana naye sina tatizo juu ya hilo, mashabiki wafahamu kuwa sisi bado ni washikaji, hivyo wasinichukulie tofauti na mengine yanaendelea ni maisha tu,” anasema.

Alipoulizwa na mmoja kati ya mashabiki kinachosemwa kuwepo kwa uhusiano kati yake na Majizo, Vanessa alijibu: “Ni kaka yangu hilo jambo halipo kabisa nashangaa watu wanatoa wapi.

“Kumbuka yule ni mfanyabiashara na ni mdau wa muziki nchini, hivyo kuna biashara ambazo nafanya namheshimu sana na Lulu pia namheshimu sana,” anasema.

Aaah! Eti kumbe ni kiki tu

Wakati ya ishu ya Vanessa na Jux kupigana chini zikipambamna moto mara paap jana wakashusha video ya ngoma yao ya Sumaku ambayo wameimba pamoja.

Kuachiwa kwa video hiyo ya Sukuma ambayo imeanza kukamatia mashabiki kibao huko You tube, mahakimu na waendesha mashtaka huko Instagram wakaibuka na kuanza kuwaponda wakidai kuwa kupigana chini kwao ilikuwa ni kiki tu.

Tangu jana Alhamisi baada ya video hiyo kuachiwa, kauli za shombo na kejeli kwa mastaa hao zikarindima huku wengi wakimponda Vanessa ambaye awali walikuwa wakimuunga mkono kwa uamuzi wake wa kutemana na Jux.

Kwanza mashabiki waliokuwa wakimuunga mkono walikuwa wakimshauri kuhakikisha anafuta kabisa kumbukumbu zote za Jux kuanzia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii na kuanzisha uhusiano mpya ili kumuondoa kabisa kwenye ramani Jux.

Hata hivyo, kuachiwa kwa ngoma hiyo ambayo Jux na Vanessa wamekiharibu kinoma, kumeonakana pigo kubwa kwa mashabiki hao ambao sasa wameishia kutema shombo tu huko mitandaoni.

Wengi wanaamini wawili hao hawajaachana bali ni kiki ya wimbo huo.

Advertisement