Utata waghubika usajili wa Makambo

WAKATI baadhi ya mashabiki na wachezaji wa Yanga wakipigwa na butwaa kusikia taarifa za straika wao tegemeo, Heritier Makambio kutua Horoya AC ya Guinea, nao mabosi wao ni kama hawaamini kilichotokea, wakidai wanamsubiri Mkongo huyo arudi wamhoji zaidi.

Makambo amedaiwa kusajiliwa na Horoya kwa mkataba wa miaka mitatu wiki moja baada ya Mwanaspoti kufichua juu ya mipango ya kutengewa kitita kinono ili atue katika klabu hiyo iliyoishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimi huu.

Ishu nzima imekuja baada ya kusambazwa kwa picha zinazomuonyesha Makambo akiwa na uzi wa klabu ya Horoya, huku viongozi wakidai wanachojua amepelekwa na kocha kwa mazungumzo na sio kusajiliwa kama ilivyoripotiwa akiwa na uzi wa Horoya.

Hata hivyo, taarifa za usajili wake zilizothibitisha na wanahabari waliopo Guinea pamoja na nyota wenzake wa Kikongo waliopo Yanga, kuwa Makambo keshamalizana na Horoya baada ya kukubaliana kila kitu ndio maana alitambulishwa juzi nchini humo.

Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla aliliambia Mwanaspoti jana Ijumaa kuwa, wanachojua wao Makambo ameenda kuzungumza na klabu hiyo baada ya kuweka ofa mezani, lakini hawajui kilichomfanya avishwe jezi wakati akiwa na mkataba na Yanga.

“Tunamsubiri arudi tumhoji, lakini kifupi tuna ofa tatu mezani juu ya Makambo ambayo aliingia mkataba wa miaka miwili na Yanga ukiwa na kipengele cha kumruhusu kujiunga na timu yoyote itakayomhitaji,” alisema Dk Msolla na kuongeza:

“Ilikuwa ni lazima kwa Makambo kuondoka kwa mujibu wa mkataba wake, lakini pia tumeona tuwe na fursa kwa nyota wengine waliopo ndani ya klabu yetu kama wakipata nafasi ya kuondoka waachwe waende kujaribu maisha mengine.”

Alisema kama Horoya itamalizana nao ni wazi fedha zake za usajili zinazokadiriwa kufikia Sh230 milioni zitainufaisha Yanga, ambayo imekuwa kwenye kipindi kigumu tangu Mwenyekiti na bilionea wa klabu hiyo, Yusuf Manji alipojiuzulu Mei mwaka juzi.

Msolla alisema Makambo ameondoka kipindi ambacho timu inahitaji kufanya usajili, ila watamkumbuka kwa vile ameifanyia mambo makubwa na endapo dili lake litaenda sawa anaamini kuondoka kwake kutakuwa chachu kwa wengine.

“Soka siku hizi ni ajira kama kazi nyingine, hivyo ni muhimu kuona wachezaji wetu wakipata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa wanaachwa waende ili waweze kuendelea kukuza vipaji vyao na hilo linawezekana kwa mchezaji mwingine yeyote aliyepo Yanga akipata timu ataruhusiwa kuondoka na mwalimu atatafuta mbadala wake,” alisema.

Kuhusiana na dau watakalopata kutokana na usajili huo alisema wana kila sababu ya kupata fedha kwa vile bado wana na mkataba na mchezaji huyo.

WENZAKE WAFUNGUKA

Kusepa kwa Makambo kumewafanya nyota wa timu hiyo kufunguka. Klaus Kindoki alisema hawana taarifa rasmi waliyopewa na klabu kuhusiana na kuondoka kwa mshambuliaji huyo, ila wanajua ameenda Horoya na wanamtakia kila la heri.

“Sio jambo zuri kwangu kwani nimeshamzoea na nimetoka naye nchi moja, ila kwa kuwa mpira ndio maisha yake namtakia kila la heri katika majukumu yake mapya naamini ataenda kuliwakilisha vizuri taifa letu la Congo,” alisema Kindoki.

“Kikubwa alichokifanya akiwa Yanga kitakumbukwa na ndicho kilichomfungulia milango ya kuonwa na klabu nyingine kubwa, nina imani atafanya makubwa zaidi ya aliyoyafanya hapa Jangwani,” alisema Kindoki.

Naye kiungo fundi, Papy Kabamba Tshishimbi alisema ni muda sahihi kwa Makambo kutimka kutokana na kiwango alichokuwa nacho na kuongeza wamempoteza mchezaji muhimu kikosini kwao.

“Kuondoka kwa Makambo kama ilivyoripotiwa mi sioni kama ni jambo la ajabu sana, kutokana na uwezo wake na kujituma bila kukata tamaa. Amekuwa na mipango mingi ndani na nje ya uwanja, anaamini katika mazoezi mchezaji kama huyo huwezi kuona ajabu akitoka kwenda kucheza katika nchi nyingine,” alisema.

Feisal Salum ‘Fei Toto’ alisema Makambo ameacha pengo kubwa katika kikosi cha Yanga kutokana na uwezo wake ambao ameouonyesha, kwani ndiye aliyekuwa kinara wa mabao akifunga mabao 16 ya Ligi Kuu na manne ya Kombe la FA.

“Yanga wameshajua kama kuondoka kwa Makambo kumesababisha pengo katika safu ya ushambuliaji, hivyo wajipange tu kuziba pengo lake,” alisema Fei, huku beki Andrew Vincent ‘Dante’ alipatwa na kigugumizi kuondoka kwa mchezaji huyo, huku akiwa haamini kama dili hilo limekamilika kweli.

“Unajua bado siamini, nadhanini mpaka nitakapokuwa simuoni mazoezini ndio nitaamini, lakini kama anaondoka ni hatua kubwa kwake kwa sababu ni mpambanaji wa kutosha tangu tulipokuwa naye kwenye timu,” alisema Dante.