Usishangae ndio imetokea! Alliance Girls yashinda mabao 17-0

Sunday May 19 2019

 

By James Mlaga

MWANZA. Alliance Girls wamefanikiwa kuandika historia ya kuwa timu ya kwanza iliyoshinda mabao mengi zaidi Msimu huu kwenye michuano ya Ligi Kuu ya Wanawake baada ya leo jioni kuicharaza Mapinduzi Queens mabao 17-0 na kufanikiwa kushika nafasi ya pili wakiwa na alama 47.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza mabao ya Alliance yamefungwa na Aisha Khamis ( matano) , Aisha Juma ( matano) Elizabeth Edward ( mawili) , Enekia Kasonga ( mawili) Suzan Adam, Grace Edward  na Janeth Matulanga.
Akizungumza na Mwanaspoti Kocha Mkuu wa kikosi hicho Ezekiel Chobanka amesema walicheza mpira wa kasi sana ndio maana waliweza kupata ushindi huo pia Uwanja ulikuwa rafiki kwa mfumo wao wa pasi za chini chini.
"Malengo yetu msimu huu yalikuwa tumalize nafasi ya pili kwasababu msimu uliopita tulikuwa wa tatu hivyo baada ya ushindi wa leo tumetimiza malengo yetu pia tuna imani msimu ujao tutakuwa mabingwa" amesema Chobanka.
Alliance wamemaliza katika nafasi ya pili licha ya kulingana alama na Simba Queens wote wakiwa na point 47 lakini  mtaji wa mabao matano ya faida yamewapa nafasi Alliance kuwa wa pili huku JKT Queens wakiwa mabingwa baada ya kushinda mechi zake zote na kufikisha alama 66.   

Advertisement