Usibishe, Messi ampoteza Ronaldo kwenye mechi 700

Tuesday December 3 2019

Usibishe- Messi -ampoteza -Ronaldo -mechi -700-klabu-Messi-mabao-mwanasport-MwanaspotiSoka-MwanaspotiGazeti-

 

BARCELONA, HISPANIA . USIKU wa Jumatano iliyopita, Lionel Messi alifanya kile ambacho Lionel Messi anapaswa kufanya.

Muargentina huyo alitoa shoo ya maana wakati Barcelona ilipojipigia Borussia Dortmund 3-1 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Usiku wa jana Jumatatu, Messi alifanya tena kile ambacho huwa anafanya mara nyingi, alipoibeba kwa mgongo wake Barcelona kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Atletico Madrid ugenini na hivyo kurejea kwenye kilele cha msimamo wa La Liga.

Kwenye mchezo ule wa Dortmund, Messi mwenye umri wa miaka 32, alifikisha mechi yake ya 700 akiwa na kikosi cha Barcelona. Kwenye mechi hizo 700, mara nyingi, Messi amekuwa hakabiki.

Uwezo wake na kufanya maajabu mengi anapokuwa ndani ya uwanja umemfanya aibue mjadala kila wakati kutoka kwa mashabiki wakisema kwamba ndiye mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea duniani.

Linapokuja suala hilo, ndipo unapoibuka jina la Cristiano Ronaldo na kufanya wawili hao, wanaoaminika kuwa bora zaidi kwenye kizazi hiki, wakishindanishwa kuona nani zaidi ya mwingine.

Advertisement

Lakini, yote kwa yote wanasema namba hazidanganyi. Kupata majibu mazuri ya ubora wa wachezaji hao basi ni kutazama namba zao tu za mambo ya uwanjani. Wakati sasa Messi akiwa amefikisha mechi yake ya 700 kwenye ngazi ya klabu, ilikuwaje wakati Ronaldo anafikisha idadi kama hiyo miaka miwili iliyopita?

Ni mchezaji gani zaidi kati ya Ronaldo na Messi wakati kila mmoja alipofikisha idadi ya mechi 700 kwenye ngazi ya klabu? Nani zaidi?

Mabao

Messi: 613

Ronaldo: 504

Kwenye mjadala wa mchezaji gani bora baina ya Messi na Ronaldo, huwezi kupata mshindi hapo, kwa sababu mastaa hao wote wawili kila mmoja ana mashabiki wake wanaoamini mchezaji wao ni bora kuliko mwingine. Lakini, ndani ya uwanja, nje ya mambo ya kishabiki, wachezaji hao kila mmoja amekuwa akifanya mambo yanayomfanya ajitofautishe na mwenzake.

Ronaldo wakati anafikisha mechi zake 700 za ngazi ya klabu alikuwa amefunga mabao 504, hiyo ilikuwa pungufu kwa mabao 109 ambayo amefunga Messi ndani ya mechi hizo 700.

Kwamba kwenye mabao hayo ya Ronaldo, mengi yalikuwa ya penalti, tofauti na mwenzake, Messi, ambaye amekuwa akifunga kwa staili ya mabao mengine tofauti. Penalti chache sana. Messi ameendelea kuwa staa hatari kwa kutikisa nyavu kwenye kikosi cha Nou Camp.

Asisti

Messi: 237

Ronaldo: 185

Kwa mara nyingine, Messi anaendelea kumbuluza Ronaldo kwenye kipengele kingine. Hapa kwenye asisti, Messi ameonekana kuwa ni moto, akipiga asisti 237 wakati anafikisha mechi zake 700 kwenye ngazi ya klabu, wakati Ronaldo yeye alikuwa na asisti 185, wakati anacheza mechi yake ya 700 alipomenyana na Valencia, Februari 22, 2017.

Gwiji huyo wa Barcelona ameonyesha kwamba ni mahiri kwenye kuwatengenezea mabao wachezaji wenzake na kwamba amekuwa si mbinafsi na ndiyo maana amefunika kwa asisti nyingi sana dhidi ya mpinzani wake. Ubora wa Messi kwenye hilo umekuwa na msaada mkubwa kwa Barcelona na ndio maana asipokuwapo kwenye kikosi cha Barcelona, basi mambo huwa wanakuwa magumu sana.

Ballon d’Or

Messi: 5

Ronaldo: 4

Baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa akiwa na Barcelona kwa mwaka huu wa 2019, hakikuonekana kuwa kitu cha kushangaza sana kwa kuona Messi anapewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or iliyofanyika usiku wa jana Jumatatu huko Paris, Ufaransa. Hiyo ilikuwa tuzo yake ya sita, kama atakuwa amebeba.

Supastaa Ronaldo yeye ameshinda tuzo hiyo mara tano pia, lakini wakati anafikisha mechi 700 kwenye mechi ambayo Real Madrid walichapwa 2-1 na Valencia huko Mestalla, wakati huo, alikuwa ameshinda tuzo nne za Ballon d’Or. Kwa wakati huo, mwenzake Messi alikuwa ameshinda tuzo hiyo mara tano, huku usiku wa jana alikuwa na nafasi ya kuweka rekodi ya kuwa mshindi wa kihistoria wa Ballon d’Or kama atakuwa amenyakua kwa mara ya sita.

Hat-Tricks

Messi: 46

Ronaldo: 41

Inaonekana kama sasa imekuwa kawaida kuona kwenye kila kipengele Messi anakuwa juu ya Ronaldo. Hilo pengine linaweza kuwa na ukakasi kwa mashabiki wa Ronaldo, lakini rekodi hizi zimechukuliwa wakati wachezaji wote hao walipofikisha mechi zao za 700 kwenye ngazi za klabu.

Kwa upande wa hat-trick, wakati anafikisha mechi 700, Messi alipiga 46 kwenye kikosi cha Barcelona, tano zaidi ya alizopiga Ronaldo, ambaye alikuwa kwenye timu nyingi ikiwamo Man United na Sporting CP.

Messi alikuwa hatari kwa kutupia tatu tatu kwenye mechi, huku hat-trick yake tamu inayokumbukwa kwenye ndani ya mechi hizo 700 ni ile ya mwaka 2014 aliyopiga dhidi ya Sevilla na ile aliyowapiga Arsenal msimu wa 2009/10 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alipiga Bao Nne kwenye usiku huo wa Ulaya.

Mataji ya ligi

Messi: 10

Ronaldo: 4

Messi alibeba mataji 10 ya ligi wakati anafikisha mechi 700, wakati Ronaldo alibeba mataji manne tu. Lakini, hilo halina maana kwamba Messi amekuwa hodari sana kuliko mpinzani wake.

Wakati Barcelona inabeba La Liga msimu wa 2004/05 na 2005/06, sawa Messi alikuwamo kwenye kikosi chao, lakini hakuwa na mchango mkubwa kihivyo, alivunga mabao saba tu kwa misimu yote miwili hiyo, huku Barca ikibeba na wakali Samuel Eto’o na Ronaldinho, ambao kwa pamoja walifunga mabao 77.

Zaidi ya hapo, Messi alikuwa kwenye kikosi chenye mafundi wengi kama Xavi na Andres Iniesta, hivyo ilikuwa sawa kubeba mataji mengi ya ligi ukilinganisha na mpinzani wake Ronaldo, ambaye alibeba manne tu wakati anafikisha idadi ya mechi 700 za klabu.

Mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya

Messi: 4

Ronaldo: 3

Hapa ndipo kwenye utata, ambao wengi utawachanganya. Kitendo cha Ronaldo kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa miaka miwili mfululizo 2017 na 2018 kimemfanya awe amebeba taji hilo mara tano, lakini kwa kutazama wakati anafikisha mechi 700, alikuwa amebeba mataji hayo mara tatu.

Kwa kipindi ambacho, Messi amefikisha mechi 700, yeye tayari alikuwa amebeba mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne na hivyo kumfanya awe amemfunika mpinzani wake wa muda wa mrefu, Ronaldo.

Mataji mengine

Messi: 20

Ronaldo: 14

Ronaldo alifanya uamuzi wa kucheza soka kwenye nchi nne kubwa za Ulaya, akatamba Ureno, kisha England, Hispania na sasa Italia. Kote huko ameshinda mataji ya kutosha na kuwa mmoja wa wachezaji matata kabisa.

Messi, kwa upande wake ameamua kubaki kwenye timu yake ya muda wote tangu akiwa mtoto, Barcelona. Ameshinda mataji makubwa sita tofauti akiwa na Barcelona na kumfanya kwa ujumla wake awe amekusanya mataji 20, wakati mpinzani wake huyo wa karibu, Ronaldo ameshinda mataji 14.

Advertisement