Ushindi upo wazi Taifa Stars

Muktasari:

Stars inapaswa kutumia mbinu mbadala, kama walivyofanya kipindi cha pili cha mchezo uliopita ambapo Idd Seleman aliingia kuchukuwa nafasi ya Hassan Dilunga.

TAIFA STARS  itarudiana na Burundi Jumapili hii ya Septemba 8 uwanja wa Taifa kusaka mbio za kuwania kucheza hatua ya makundi ya kupata nafasi ya kucheza Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa jana jijini Bujumbura, Stars ilitoka sare na Burundi ambapo nyota wa zamani wa timu hiyo pamoja na makocha wametoa maoni yao kuelekea mechi ya marudiano, mechi hiyo Stars ilitoka sare ya bao moja.
Mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayai alisema timu yoyote inapaswa kufahamu malengo yake katika mchezo wa marudiano ili kupata matokeo mazuri na kusonga mbele.
'‘Mchezo uliopita, Stars hawakuwa na muunganiko mzuri kulikuwa na kasoro kidogo hasa safu ya ushambuliaji ambapo walicheza Mbwana Samatta na Simon Msuva,” alisema.
Stars inapaswa kutumia mbinu mbadala, kama walivyofanya kipindi cha pili cha mchezo uliopita ambapo Idd Seleman aliingia kuchukuwa nafasi ya Hassan Dilunga.
"Kutumia wachezaji wenye uwezo binafsi kama hawa wanaweza kuisaidia Stars kupata matokea mazuri," alisema
Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny  Mwaisabula alisema mchezo wa marudiano utakuwa mgumu ingawa Stars ina mtaji wa bao la ugenini, hivyo inapaswa kuwa makini.
Pia ameitaka safu ya ulinzi ya Stars kuwasoma washambuliaji wa Burundi ili kuwadhibiti wasiweze kupata bao mapema.
Mwaisabula alisema Stars inapaswa kutengeneza nafasi za kutosha na kuzitumia vizuri, kwani mchezo uliopita Stars ilishindwa kutumia nafasi walizokuwa wakizipata.
Naye mchezaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema kitu kizuri kwa Stars ni kupata bao la ugenini ambalo litazidi kuwapa nguvu mchezo wa marudiano.