Usajili wa Kwasi shaka tu Simba

Muktasari:

  • Beki huyo amejitegenezea jina kubwa kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao kwa mipira ya adhabu katika Ligi Ku Bara msimu huu

 Sakata la usajili wa mchezaji mpya anayedaiwa kusajiliwa na Simba, Asante Kwasi limechukua sura mpya baada ya klabu hiyo kudai inaendelea na mazungumzo na Lipuli.

Kwasi ameibua mzozo baada ya klabu yake ya Lipuli ya Iringa kudai bado inamtambua ni mchezaji wake kwa kuwa ana mkataba.

Uongozi wa Lipuli unadai Simba imemsajili kinyemela mchezaji huyo mwenye uwezo wa kucheza zaidi ya moja katika safu ya ulinzi.

Mwenyekiti wa Lipuli, Ramdhani Mahano ameliambia gazeti hili jana kwamba, Kwasi alitia saini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia klabu hiyo Julai 29, 2017.

"Tumemlipa mshahara wake wa mwezi huu dola 500 baada ya kutueleza ana matatizo na alikwenda kwenye msiba Ghana tukampa tiketi na tulimtumia dola 470 ambazo alitueleza za tiketi ya kurudi nchini akitokea Ghana.

"Aliporejea alitueleza kwamba Simba inamtaka, nikamwambia asifanye chochote hadi tuelewane na Simba, lakini akatukiuka," alidai mwenyekiti huyo.

Mahano alisema hawawezi kukaa meza moja na Simba kuzungumza na wanasubiri kupeleka pingamizi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

"Ingekuwa hajasaini mkataba tungeweza kukaa nao mezani, lakini kwa hatua lilipofika suala hili hatuwezi tunasubiri kupeleka pingamizi TFF," alisema Mihano.

Akizungumza kuhusu sakata hilo, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah 'Try Agai' alisema wapo katika mazungumzo kuhusu usajili wa Kwasi.

"Hili suala la Kwasi, mchakato wake unaendelea na hatuwezi kuzungumzia kitu nusu nusu, tupeni muda siku si nyingi tutatoa taarifa yetu ya usajili na kila kitu kitakuwa wazi," alisema Abdallah.

Hata hivyo, wachambuzi wa soka waliobobea katika taaluma ya sheria, walisema endapo Simba imekiuka utaratibu katika usajili, mchezaji huyo anaweza kufungiwa.

Mbali na mchezaji kupewa adhabu, pia klabu ya Simba inaweza kukumbwa na rungu la kutokusajili au kupigwa faini kwa kosa hilo.

Wanasheria hao nguli, Ndumbaro, El Maamry walisema endapo mchezaji huyo alikuwa na mkataba na Lipuli usiopungua miezi sita kabla ya kumalizika, akatia saini kujiunga na Simba anatakiwa kufungiwa mwaka mmoja kwa mujibu wa sheria.

Wakili Damas Ndumbaro alisema kwa mujibu wa sheria za soka, mchezaji haruhusiwi kuzungumza na klabu nyingine kuhusu usajili endapo mkataba wake utakuwa umebakiza miezi saba au zaidi.

"Kama kweli Kwasi bado ana mkataba wa miezi minane na Lipuli na ikabainika amekwenda Simba hilo ni kosa na kwa mchezaji itabidi afungiwe kucheza soka mwaka mmoja.

"Vilevile klabu iliyomsainisha inatakiwa kufungiwa kwa kipindi fulani kufanya usajili au inatozwa faini na wakati mwingine kupewa onyo kali,"alisema Wakili Ndumbaro.

Naye Said El Maamry alisema mchezaji anaruhusiwa kuzungumza na timu nyingine kama tu amebakiza mkataba wa miezi sita na klabu husika kinyume na hapo ni kosa.

"Suala la Kwasi kama ni kweli na ushahidi upo basi itabidi Simba wawe wapole waende kukaa mezani na Lipuli," alisema El Maamry.

Mchezaji huyo amekaririwa na vyombo vya habari kwa nyakati tofauti akidai anataka kucheza Simba na ametia saini mkataba wa miaka miwili.