Upamecano kuwa mbadala wa Van Dijk huko Liverpool

BAADA ya beki wao wa kati, Virgil van Dijk kupata majeraha ambayo yatamfanya kukaa nje kwa msimu mzima, ripoti zinadai kwamba Liverpool imeanza harakati za kuiwania saini ya beki wa kati raia wa Ufaransa na RB Leipzig, Dayot Upamecano, 21, ili kuipata huduma yake katika dirisha lijalo la majira ya baridi au kiangazi. Inaaminika, Liver kwa sasa inapambana kuhakikisha inapata mbadala wa Van Dijk ili kuendelea kuimarisha safu yao ya ulinzi ambayo ubora wake ulikuwa unachagizwa zaidi na beki huyo.

Upamecano ambaye alikuwa anawindwa sana na Manchester United iliyoshindwa kuipata saini yake, amekuwa na kiwango bora ndani ya timu hiyo tokea ajiunge nayo mwaka 2017.

Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2023 na thamani yake katika soko la usajili ni Euro 60 milioni, mpaka sasa amecheza mechi sita za michuano yote akiwa na Leipzig.