Unyama unyamani : Wilder v Fury II ,tantalila kwisha

Muktasari:

Katika pambano la Desemba Mosi, 2018, Fury alikaa chini mara mbili kutokana na ngumi nzito za Wilder, lakini alitawala asilimia kubwa ya mchezo huku akimtesa Bronze Bomber kwa ngumi nyingi za haraka na kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine.

LAS VEGAS, MAREKANI . VIPI umeshachagua upande? Kama bado huu ndio wakati wako wa kufanya hivyo maana siku zimeisha kwa sababu kesho alfajiri ndiyo ule ubishi wa nani mbabe kati ya Deontay Wilder na Tyson Fury utamalizwa. Moto utawaka.

Ndiyo, katika Kasino ya MGM Grand Garden Arena, Las Vegas, Nevada, Marekani ndiko litapigwa moja ya pambano kali la ngumi uzito wa juu duniani kati ya Wilder ‘The Bronze Bomber’ na Fury ‘The Gypsy King’. Walipokutana mara ya kwanza Desemba Mosi, 2018, pambano hilo liliisha kwa droo, yaani majaji na utaalamu wao baada ya raundi 12 za ngumi nzito na burudani walishindwa kujua nani alikuwa mbabe.

Droo hiyo ya pambano la kwanza ni sababu ya pambano la kesho alfajiri lililopewa jina la Wilder vs Fury II, kusubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa ngumi duniani, maana hakuna namna lazima mbabe apatikane.

Katika pambano la Desemba Mosi, 2018, Fury alikaa chini mara mbili kutokana na ngumi nzito za Wilder, lakini alitawala asilimia kubwa ya mchezo huku akimtesa Bronze Bomber kwa ngumi nyingi za haraka na kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Baada ya kukutana mara ya kwanza unatarajia kuona pambano ambalo linawakutanisha mabondia ambao tayari wanajuana vizuri, hivyo linatarajiwa kuwa la ufundi mwingine huku Fury akitarajiwa kutawala sehemu kubwa na Wilder kama kawaida yake akivizia na lile konde lake la mkono wa kulia.

Kiufundi

Pambano hilo linawakutanisha mabondia wawili wanaosimama kwa kutanguliza mguu wa kushoto mbele ‘Orthodox Boxers’, lakini wenye aina mbili tofauti za kupigana. Na sifa zao kiufundi ni hizi:

Wilder fundi wa KO

Silaha kubwa ya Wilder ni mkono wake wa kulia, ni mara chache sana utakuta bondia anasimama baada ya kukutana na konde la mkono wa kulia wa Bronze Bomber (Fury pekee ndiye aliwahi kuinuka mara mbili baada ya kukutana na ngumi hiyo).

Wilder hatabadilika sana safari hii na ataendelea kutegemea ngumi yake ya mkono wa kulia na ‘hook’ ya mkono wa kushoto kummalizia pambano, mwenyewe huwa anatamba kuwa hakuna bondia anayeweza kuikwepa ngumi hiyo ndani ya raundi 12.

Fury yuko vizuri kiufundi

Fury ni bondia ambaye yuko vizuri kiufundi, ana uwezo mkubwa wa kujilinda na kushambulia, anahama haraka, uwezo mkubwa wa kukwepa na ‘movement’ nzuri kwenye miguu yake.

Ni bondia ambaye anaweza kukudhuru akiwa anarudi nyuma na pia akiwa anashambulia kwa aina yake ya upiganaji kwani akishindwa kukutwanga kwa KO, basi atashinda kwa pointi na ndiyo maana pambano la kwanza alitawala sana mchezo.

Kikubwa ambacho kilimsaidia Wilder kupata droo katika pambano hilo ni kitendo cha kumuangusha mara mbili Fury, lakini kiujumla Fury ndiye aliyepiga ngumi nyingi zaidi zilizofika na zenye pointi.