United, City zawekwa mtegoni Ulaya

Muktasari:

Zaidi ya watu 254,195 wamebainika kuambukizwa virusi vya Corona nchini Uingereza, huku watu takribani 36,393 wakipoteza maisha kutokana na janga hilo

London,Uingereza. Ushiriki wa timu za Manchester City, Chelsea na Manchester United katika mashindano ya Ulaya msimu huu umewekwa kwenye mabano baada ya serikali ya Uingereza kupitisha sheria ngumu inayoweza kuziathiri.

Sheria hiyo ni ya wasafiri wote wanaoingia nchini humo kuwekwa karantini kwa siku 14 (wiki mbili) na baada ya hapo ndipo waendelee na shughuli nyingine zilizowapeleka nchini humo.

Uamuzi huo umeonekana utaziletea shida Manchester City na Chelsea zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na Manchester United iliyopo katika Kombe la Europa kwani utavuruga ratiba zao au za wapinzani wao katika mashindano hayo.

Kwa City, sheria hiyo inaonekana haitowaumiza sana kutokana na kuwa na mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora dhidi ya Real Madrid ambao itauchezea nyumbani baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini katika mchezo wa kwanza

Real Madrid ndio wanaonekana wataumia zaidi kwani watalazimika kuwekwa karantini kwa wiki hizo mbili jambo litakalowafanya wakose baadhi ya michezo ya Ligi Kuu ya Hispania.

Chelsea nao watalazimika kukosa mechi kadhaa za Ligi Kuu ya England kwani nao watalazimika kuwekwa karantini kwa siku 14 pindi watakaporejea England baada ya mechi yao inayosubiriwa ugenini dhidi ya Bayern Munich.

United nayo itajikuta katika wakati mgumu kwenye mashindano ya Ligi ya Europa kwani wapinzani wao Lask Linz ya Austria nao watalazimika kuwekwa karantini kwa wiki mbili pindi watakapotua England kucheza mechi ya marudiano ya hatua ya 16 bora baada ya kuchapwa mabao 5-0 katika mechi ya kwanza nyumbani.

Sheria hiyo imepitishwa kwa lengo la kuepuka kuibuka kwa maambukizi mapya ya Corona nchini humo na watakaokiuka watatozwa faini ya Pauni 1000, kifungo au vyote viwili kwa pamoja.