Unajua tatizo la Juma Mgundai? Ni KISS tu

Saturday November 16 2019

Unajua -tatizo- Juma -Mgundai- KISS -tasnia -Kocha -Msaidizi - Taifa Stars-Juma -Mgunda

 

By Ezekiel Kamwaga

WIKI inayoisha kesho Jumapili imetufunza jambo moja kubwa katika familia yetu ya michezo hapa nchini; kwamba bado kuna safari ndefu katika eneo la mawasiliano ya umma miongoni mwa wadau wakubwa wa tasnia yetu.

Mawasiliano haya yanahusu ni taarifa gani iende kwa umma, kwa wakati gani na kwa namna gani. Tunaishi katika zama za taarifa na ndiyo sababu hakuna tena taasisi muhimu hapa duniani ambayo haijaajiri wataalamu wa mawasiliano ya umma.

Matukio mawili yameingia akilini mwangu wiki hii. La kwanza linahusu kauli ya Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda, kuhusu mlinda mlango wa Simba, Aishi Manula.

Katika safu hii wiki iliyopita niliasa kwamba ni muhimu kwa wahusika wa Stars watoe taarifa kuhusu nini hasa kimesababisha mlinda mlango huyo asiitwe kwenye timu. Nikaandika kwamba hilo ni muhimu kwa sababu watu watakuwa na taarifa sahihi na kama Aishi atakuwa anahitaji msaada wa aina yoyote, anaweza kuupata kama watu wakijua kinachomsibu.

Nashukuru kwamba Mgunda alitoa taarifa hiyo muhimu ingawa kidogo ‘aliteleza’ kwa kutoa mifano ya posa wakati anajaribu kufafanua. Ninamfahamu Mgunda na ninajua hakuwa na tafsiri ambayo ilikuja kuwakera mashabiki na wanachama wa Simba SC.

Kama asingeenda kwenye mifano hiyo ya posa, Mgunda alikuwa na maelezo ya kujitosheleza kabisa. Ndiyo sababu, katika eneo hili la mawasiliano watu hufundishwa kuhusu dhana ambayo hufupishwa kwa herufu nne tu –KISS.

Advertisement

KISS ni kifupisho cha maneno ya Lugha ya Kiingereza Keep It Short and Simple. Kwamba taarifa inatakiwa iwe rahisi na kwa ufupi kwa kadiri inavyowezekana.

Kwa kuingiza masuala ya posa katika masuala ya mpira, Mgunda alikuwa amekwenda nje ya mstari. Na ikumbukwe mchezo wa soka ni mchezo ambao mfumo dume umetamalaki na jambo lolote la kumhusisha mchezaji au klabu na jinsia ya kike huwa linaleta shida kidogo.

Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa wachezaji, viongozi na wadau wote wa michezo wahakikishe kwamba dhana hii ya KISS inakaa vichwani mwao wakati wowote wanapoona wanatafutwa na waandishi wa habari.

Mkude na Taifa Stars

Wiki hii pia kulikuwa na suala la mchezaji wa Stars, Jonas Mkude, kuomba ruhusa ya kushughulika na masuala yake ya kifamilia na kujiondoa kwenye kikosi kinachojiandaa na mchezo dhidi ya Guinea ya Ikweta.

Taarifa rasmi ilieleza Mkude alikuwa na matatizo ya kifamilia. Nilikuwa nasikiliza mojawapo ya vipindi vya michezo vya usiku katika redio za hapa nchini na mmoja wa wasikilizaji mara moja alianza kutoa shutuma kuhusu mchezaji huyo.

Kwamba kila wakati ana matatizo ya kifamilia, hataki kukaa kambini na wakati umefika sasa kwa viongozi wa TFF na makocha wa Stars kuachana naye.

Katika lugha ya kimawasiliano, matatizo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Hizi shida zote tuzionazo ni za kawaida na sababu kuna wengine hutumia pia neno changamoto za kimaisha.

Hata hivyo, kwa wenzetu huko, wameanza kutumia neno compas sionate leave yaani ruksa ya kibinadamu au likizo ya utu kwa sababu wakati mwingine wachezaji hupewa ruhusa kwa mambo ambayo si matatizo kusema ukweli.

Mchezaji anaweza kuwa anataka kushuhudia mkewe akijifungua hospitalini, kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa ya mzazi wake ambayo ni ya muhimu sana kifamilia, kujitibia uraibu wa aina yoyote (ulevi, uzinzi nk). Kwa hiyo si kila ruhusa ambayo mchezaji au mfanyakazi anapewa huwa inatokana na matatizo. Wakati mwingine mchezaji anaweza kukubaliwa ruhusa ya jambo la kusherehekea kabisa lakini sisi hapa tutabaki na neno matatizo ya kifamilia.

Inaanza kujenga picha kwamba kuna watu kila siku wana matatizo tu wakati wengine hawana.

Katika nchi kama yetu ambayo kila mtu ana matatizo chungu nzima; mtu mmoja kuonekana akipewa ruhusa kwa sababu ya matatizo ni jambo linaloweza kuleta ukakasi.

Kama mchezaji ana mzazi au mtoto ambaye yuko mahututi, isemwe kwamba anakwenda kuuguza mzazi.

Tuliona namna Manchester City ilivyompa ruhusa David Silva kwenda kumshughulikia mtoto wake aliyezaliwa njiti kwao Hispania. Mashabiki walielewa na wakampa baraka zao.

Pale inapobidi, isemwe tu kwamba huyu mkewe amejifungua na tumemruhusu akamsaidie mkewe katika wakati huo. Hili si tatizo lakini kumnyima mtu ruhusa ya kukaa na mpenzi wake katika wakati huu si jambo linalokubalika.

Kama mtu mtoto wake amegongwa na gari, isemwe tu hivyo kwamba kuna hilo tukio. Neno kwa matatizo ya kifamilia, linafunika vitu vingi na linaweza kutumika kama kichaka cha kuficha uvivu na kiburi cha wachezaji na kwa upande mwingine kuleta tafsiri potofu kwa mashabiki na wadau wengine wa mchezo huo.

Kama kuna tatizo na wahusika wanattaka libaki ndani ya familia, ndipo sasa FA inapoweza kutoa taarifa kuhusu mchezaji husika kwa kubaki kwenye KISS kama tulivyozungumza mapema.

Kwa kufanya hivyo, wachezaji watalindwa dhidi ya kashfa na dhana potofu kutoka kwa mashabiki wao na wakati huohuo wakawa wanacheza huku wakiwa na uhakika kwamba watashughulikiwa mahitaji yao kwa kuheshimiwa na kupata lugha wanazostahili.

Tukiwa na mfumo huu tunaweza kuwa pamoja na wachezaji wetu kwenye matatizo yao. Na wao watakuwa wanajua kuwa tuko nao pamoja kwenye shida na raha.

Advertisement