Unaambiwa udhaifu wa Maguire huu hapa

Wednesday August 7 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND. STAA wa zamani wa Manchester United, Paul McGrath amefichua udhaifu mkubwa wa beki mpya wa timu Harry Maguire ambao utawagharimu sana wababe hao wa Old Trafford msimu huu.

Man United imenasa huduma ya Maguire kwa ada ya Pauni 80 milioni akitokea Leicester City na hivyo kumfanya kuwa beki ghali zaidi duniani.

Maguire, ambaye amesaini dili la miaka sita kwenye kikosi cha Man United ni mchezaji watatu kunaswa na timu hiyo baada ya Aaron Wan-Bissaka na Daniel James na dhamira kubwa atakwenda kumaliza tatizo la beki kwenye kikosi hicho.

Lakini, staa wa zamani wa Old Trafford, McGrath amedai kwamba shida kubwa ya Maguire ni kwamba anapenda kukokota mipira kutoka kwenye eneo la nyuma, huku akiwa hana kasi ya kutosha kitu ambacho kitakuwa na shida kubwa atakapopoteza mpira.

"Naamini Man United watakuja na mfumo ambao utawafanya aweze kuziba udhaifu wa Maguire. Kwa sababu wasipofanya hivyo, basi watasumbuka sana watakapocheza na timu yenye washambuliaji hatari kama Manchester City na Liverpool," alisema.

"Harry anapenda sana kukokota mipira kutoka kwenye eneo la ulinzi, kitu ambacho kinakubalika zaidi kwenye soka la kisasa. Lakini, shida yake, atakapopoteza mipira tu, basi inakuwa balaa kwa sababu hana kasi kama aliyokuwa nayo Virgil van Dijk au Raphael Varane.

Advertisement

"Hivyo kwenye hilo, ni lazima Man United wafanye mazoezi sana huko Carrington ili kuweza kumfanya beki huyo awe na mtu wa kumlinda anapojaribu kwenda mbele na mipira."

Man United ilihusishwa na mabeki kibao wa kati akiwamo Kalidou Koulibaly kabla ya kocha Ole Gunnar Solskjaer kuamua kuvunja benki na kupata huduma ya Maguire kutoka huko King Power.

Advertisement