Unaambiwa Pauni 200 milioni unabeba Neymar

Wednesday July 10 2019

 

PARIS, UFARANSA. Unaambiwa hivi, Paris Saint-Germain wapo tayari kumpiga bei supastaa wao wa Kibrazili, Neymar, lakini kama tu kutawekwa mezani ofa ya Pauni 200 milioni.

Barcelona wapo kwenye harakati za kuinasa huduma yake na kumrudisha huko Nou Camp, lakini mambo yamekuwa magumu kwa sababu PSG hawawezi kumruhusu kirahisirahisi mwanasoka wao huyo ghali duniani.

PSG walimsajili Naymer kutoka Barcelona mwaka 2017 kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia kwenye uhamisho, Pauni 198 milioni.

Mkurugenzi wa michezo wa PSG, Leonardo alisema kwamba mazungumzo yoyote ya kumpiga bei mchezaji huyo yataanza kama kutawekwa mezani kiwango cha pesa cha pesa.

Lakini, Barcelona wanataka kuja na mpango wa kuchanganya pesa pamoja na mchezaji ili kumnasa Neymar, ambaye anatakiwa na maswahiba wake, Lionel Messi na Luis Suarez huko Nou Camp ili wakarudishe ile kombinesheni yao matata kwenye fowadi iliyokuwa ikifahamika kwa jina la MSN.

Kwenye mpango wa kuwalegeza PSG, Barcelona wamepanga kumweka mezani beki wa kati Mfaransa, Samuel Umtiti na pesa ili kumchukua Neymar, huku wachezaji wengine wanaodaiwa kwamba huenda wakawekwa kwenye chambo cha kunasa supastaa huyo wa Kibrazili ni Philippe Coutinho, Ousmane Dembele, Ivan Rakitic na Malcom.

Advertisement

Neymar amekuwa kwenye mgogoro mkubwa na waajiri wake huko PSG baada ya kuripotiwa kuwaambia kwamba hayupo tayari kuendelea kuitumikia timu hiyo msimu ujao, huku akishindwa pia kurudi kujiunga na wenzake kwenye mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya.

Advertisement