Una hela! Bei ya kila nyota wa Manchester City hadharani

Muktasari:

Msimu huu, ngoma imekuwa ngumu kwa kikosi hicho cha Pep Guardiola, wakijikuta nyuma kwa pointi 25 dhidi ya vinara Liverpool.

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHESTER City imejibebea taji la Ligi Kuu England mfululizo kwa misimu miwili iliyopita. Wamefanya hivyo kwa kucheza soka la kibabe, hasa msimu uliopita, walipowabwaga Liverpool kimafia kwa tofauti ya pointi moja tu.
Msimu huu, ngoma imekuwa ngumu kwa kikosi hicho cha Pep Guardiola, wakijikuta nyuma kwa pointi 25 dhidi ya vinara Liverpool.
Hata hivyo, msimu wenyewe haueleweki kama utaendelea au utasitishwa. Kama utasitishwa, kiufundi hiyo ina maana Man City itaingia msimu ujao ikiwa mabingwa watetezi wa ligi hiyo. Licha ya kushindwa kufikia kiwango cha msimu uliopita kiuchezaji, ubora wa mchezaji mmojammoja kwenye kikosi bado upo juu na kufanya thamani zao kuwa juu. Hii hapa orodha ya thamani ya kila mchezaji kwenye kikosi cha Man City. Staa Raheem Sterling, hayupo kwenye ubora wa msimu uliopita, lakini ndiye anayeshika namba moja kwa thamani kubwa, akidaiwa kuwa na thamani ya Pauni 144 milioni. Hiyo ina maana ukimtaka Mwingereza huyo, basi mkwanja wako usipungue kiasi hicho.
Kevin De Bruyne anashika namba mbili, ambapo Mbelgiji huyo aliyepiga asisti 20 msimu huu anatajwa kuwa na thamani ya Pauni 135 milioni. Hivi karibuni staa huyo alijifunga zaidi huko Etihad, abaki hapo kwa muda mrefu.
Kisha wanafuata Leroy Sane na Bernardo Silva, ambapo kila mmoja anatajwa kuwa na thamani ya Pauni 90 milioni huko sokoni.
Kiungo mpya, Rodri ametajwa kuwa na thamani ya Pauni 72 milioni, wakati beki wa kati, aliyetumikia muda mwingi msimu huu nje ya uwanja kwa kuwa majeruhi, Aymeric Laporte ana thamani ya Pauni 67.5 milioni. Kipa Ederson na straika Gabriel Jesus kila mmoja ana thamani ya Pauni 63 milioni, wakati Sergio Aguero ni Pauni 58 milioni, Riyad Mahrez ni Pauni 54 milioni na Ilkay Gundogan ni Pauni 45 milioni sawa Kyle Walker.
Joao Cancelo na John Stones thamani zao kila mmoja ni Pauni 40.5 milioni, huku Benjamin Mendy akiwa na thamani ya Pauni 31.5 milioni.
Oleksandr Zinchenko na Phil Foden kila mmoja ana thamani ya Pauni 27 milioni, Nicolas Otamendi Pauni 16.2 milioni, David Silva Pauni 13.5 milioni na Fernandinho Pauni 9 milioni.