Umtiti amtosa besti’ake Lacazette kutua Emirates

Tuesday September 10 2019

 

BARCELONA, HISPANIA. BEKI Samuel Umtiti amezima kabisa ndoto za straika Alexandre Lacazette anayepiga za chinichini akimtaka Mfaransa mwenzake huyo wakakipige pamoja Arsenal.

Umtiti na Lacazette ni marafiki na Juni walikwenda likizo pamoja huko Miami, Marekani - jambo ambalo liliibua uvumi mwingi kwamba beki huyo wa Barcelona alikuwa akijiangaa kutua Arsenal, kwa sababu kwa wakati husika Kocha Unai Emery alikuwa akisaka beki wa kati wa kiwango bora.

Lakini majuzi tu hapo, wakiwasiliana kupitia Twitter, Lacazette alimtumia video Umtiti akimwambia anamsubiri huko Emirates.

Arsenal ilihusishwa na Umtiti katika kipindi chote cha uhamisho wa majira ya kiangazi, ambapo ilikuwa ikisaka beki wa kati wa kiwango cha dunia ili kuimarisha safu yake ya ulinzi.

Lacazette, 28, ambaye alijiunga na Arsenal mwaka 2017, alimwambia swahiba wake huyo “nakusubiri”.

Lakini, Umtiti, ambaye hakuwamo kwenye kikosi cha Ufaransa kilichoichapa Albania 4-1 kwenye kufuzu Euro 2020, huku akiwa amekosa pia mechi zote tatu za kwanza za Barcelona ilizocheza kwenye La Liga msimu huu, alimjibu rafiki yake huyo jibu la kwanza hawezi kwenda Arsenal.

Advertisement

Umtiti alisema: “Nilikuwa na malengo tangu nikiwa mdogo. Malengo yalikuwa Barcelona. Nimekuja hapa kukaa sana na kushinda mataji.”

Kocha Emery anataka beki baada ya kumpiga bei Nacho Monreal kwenda Real Socieded kwa ada ya Pauni 8 milioni huku Hector Bellerin akiwa majeruhi. Kutokana na hilo anaweza kuanza na ofa ya Pauni 60 milioni kumnasa Umtiti wakati dirisha la usajili wa Januari litakapofunguliwa. Inachoombea Arsenal, Umtiti aendelee kusugua tu benchi huko Nou Camp ili iende kumbeba kirafiki.

Advertisement