Umri umesogea lakini dhahabu Ligi Kuu Bara

Muktasari:

Kwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hawa hapa ni nyota ambao umri umesogea lakini wanakinukisha balaa.

WANASEMA mchezo wa soka ni wa vijana kutokana na mchakamchaka unaokuwapo ndani ya dakika tisini.

Hata hivyo, ubora wa mvinyo huongezeka kadri umri unavyosogea.

Kwa Ulaya, ambako soka ndiyo gumu zaidi, tunawashuhudia wachezaji kadhaa wenye umri wa miaka 30 na zaidi (ambao katika mchezo huu huitwa wazee) wakitisha.

Kwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hawa hapa ni nyota ambao umri umesogea lakini wanakinukisha balaa.

JOHN BOCCO (29)

Miezi mitatu ijayo anatimiza umri wa miaka 30. Mchakamchaka anaowapeleka mabeki, juhudi na kutokata tamaa ni vitu vinavyofanya iwe ngumu kujua kama umri wa straika huyu wa Simba umesogea. Akilitumia vyema umbo lake lililojengeka kimichezo na urefu wake, Bocco ni habari mbaya kwa mabeki wa Ligi Kuu ya Bara.

Bocco ambaye alicheza kwa mafanikio kwa muda mrefu akiwa na Azam FC, ni tegemeo kwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars akihusika kuiwezesha kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, pia aliifikisha Simba robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na tayari ametupia mabao 14 katika Ligi Kuu ya Bara, akipitwa mabao sita na kinara Meddie Kagere.

AMISSI TAMBWE (30)

Straika Mrundi wa Yanga, ni miongoni mwa nyota wanaowanyima usingizi mabeki kutokana na uwezo kubwa wa kuliona goli. Akicheza mara nyingi ni kama hayupo vile uwanjani, lakini mashabiki wamezoea kumwona akirudi akishangilia.

Amefungaje siyo muhimu sana kwake. Anatisha kwa magoli ya vichwa na kwa misimu kadhaa amekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara.

Japo msimu huu amepungua makali kutokana na majeraha, bado anaogopesha anapoingia kutokea benchi. Ametupia mabao 7 hadi sasa msimu huu.

ERASTO NYONI (31)

Huu ni msimu wake wa 13 dimbani tangu alipoanza kucheza Ligi Kuu mwaka 2005 katika kikosi cha AFC Arusha. Nyoni aliwahi kucheza soka ya kulipwa Vital O ya Burundi kabla ya kutua Azam. Kwa sasa ni mchezaji wa Simba na Taifa Stars, akiwa mchezaji mzoefu, lakini ubora wake umempa nafasi ya kuwamo katika kikosi cha kwanza.

Makocha wote wanaopita alipo, wanaonekana kumwelewa sana kiraka huyo ambaye amekuwa akifunika katika nafasi zote nne za ulinzi anazocheza na kiungo. Anarusha mipira kama kona na ‘frii-kiki’ anazopiga, weka mbali na watoto.

MEDDIE KAGERE (32)

Ni msimu wake wa kwanza kucheza kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Ameonyesha uwezo mkubwa sana tangu alipojiunga na Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya kwa dau la dola 60,000 (Sh 138 milioni).

Amethibitisha kuwa Simba haikukosea kumwaga kiasi hicho kikubwa cha pesa pamoja na mshahara wa dola 5,000 (Sh. 11 milioni) kila mwezi kwa ajili ya kumsajili straika huyo mwenye umri wa miaka 32. Kagere ndiye kinara katika chati ya wafungaji wanaoongoza kwenye Ligi Kuu ya Bara msimu huu akiwa na mabao 20m akiwapita kwa mabao manne wanaomfuatia Heritier Makambo wa Yanga na Salum Aiyee wa Mwadui.

Licha ya umri mkubwa, Kagere ambaye pia alitisha wakati Simba ikichanja mbuga hadi robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika alikopiga mabao sita kabla ya kutolewa dhidi ya TP Mazembe ya DRC, ameendelea kuwa tegemeo Msimbazi akiwaweka benchi hadi chipukizi kama Adam Salamba.

SERGE PASCAL WAWA (33)

Mkoba wa Simba, Serge Pascal Wawa, ameupiga mwingi sana msimu huu katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi ambacho kinaongoza Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Alijihakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kilichopata mafanikio makubwa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kilichoenda hadi robo-fainali kabla ya kutolewa na TP Mazembe ya DR Congo.

Licha ya umri wake mkubwa, raia huyo wa Ivory Coast aliyetua Simba akitokea Azam alikocheza kwa kiwango cha juu kabisa, alitengeneza pacha imara ya ulinzi wa kati Simba akishirikiana na Erasto Nyoni na wakati mwingine Juuko Murushid. Hata hivyo, majeraha yamemfanya ashindwe kumalizia mechi za mwisho wa msimu huu.

KELVIN YONDANI (34)

Siyo Yanga tu, huyu ni panga pangua hadi katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kilichofuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019.

Alitamba akiwa katika klabu ya Simba na anaendelea kutamba akiwa Yanga. Amekuwa akikutwa na baadhi ya wachezaji akachezanao katika Ligi Kuu ya Bara na anaachwa bado kiwango chake hakijawahi kushukua. Mkoba huyu hamna mchezaji Taifa Stars wala Yanga anayempa changamoto katika nafasi yake ya beki wa kati.

Haijawahi kutokea ukaona mkongwe huyu akayumba kwa kiwango chake kushuka. Muda wote ni muhimu kikosini na asipokuwepo pengo lake huonekana wazi.

JUMA KASEJA (34)

Ndiye kipa aliyecheza muda mrefu zaidi miongoni mwa makipa waliopo katika vikosi mbalimbali vya timu za Ligi Kuu. Ni kipa aliyedumu kwa muda mrefu zaidi katika kikosi cha timu ya taifa akiwa ni panga pangua.

Kaseja alianza kucheza soka mwaka 2000, alipojiunga na Moro United akitokea Makongo Sekondari kabla ya kuhamia Simba alikodumu kwa zaidi ya miaka kumi. Kipa huyu amekuwa katika kiwango katika timu zote alizocheza kuanzia Moro United, Simba, Yanga, Mbeya City na Kagera Sugar. Uimara wake na umri alionao vinambeba kuwa miongoni mwa nyota wa kuigwa na vijana wanaochipukia katika soka. Hivi sasa anakipiga KMC katika Ligi Kuu ya Bara.

AGREY MORRIS (35)

Nahodha wa Azam FC, Aggrey Morris ni mmoja wa mabeki tegemo kwa timu yake na Taifa Stars. Alianza kucheza Ligi Kuu Zanzibar mwaka 2004 akitamba na kikosi cha Mafunzo kabla kusajiliwa na Azam mwaka 2009 alikodumu hadi sasa.

Morris ni mchezaji tegemeo sasa kikosini kwake na ubora wake haupungui amekuwa mpambanaji nyakati zote pia amejijengea namba ya kudumu katika kikosi cha timu ya taifa.

Goli lake katika mechi ya mwisho ya kuwania kufuzu kwa Afcon 2019 ambayo Stars walishinda 3-0 dhidi ya Uganda, lilikuwa muhimu sana kuipa tiketi Tanzania ya kwenda kwenye fainali zao za pili za Mataifa ya Afrika, Misri.