Ukarabati Uwanja wa Azam Complex watumia Sh 400milioni

Muktasari:
- Mechi tano zitakuwa za kundi B linalojumuisha timu za Cameroon, Guinea, Morocco na Senegal na mechi ya mwisho ya kundi A baina ya Nigeria na Uganda.
Dar es Salaam. Takribani Shilingi 400 milioni zimetumika kufanyia ukarabati wa Uwanja wa Azam Complex ili ukidhi vigezo vya kutumika kwa mashindano ya Afrika kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON U17) zitakazofanyika nchini kuanzia Aprili 14 hadi 28.
Ukarabati huo umefanyika kwenye eneo la kukaa wageni maalum, waandishi wa habari, vyumba vya kubadilishia nguo, sehemu ya kupimia matumizi ya dawa za kusisimua misuli pamoja na chumba cha matibabu.
Akizungumza katika ziara yake ya ukaguzi wa miundombinu mbalimbali itakayotumika kwa mashindano hayo, Waziri Mwakyembe alifichua kuwa kiasi hicho cha fedha chote kimegharamiwa na Azam FC.
"Kwa kweli Azam mnastahili pongezi kubwa sana na mnatakiwa kupongezwa. Hii ndio maana ya sekta binafsi kwamba wakati taifa linapoonyesha kuhitaji miundombinu fulani, kwa ajili ya michezo mikubwa kama hii, nyie mmejitokeza na mimi nina uhakika kwa makadirio ya mwanzo nyie mmetumia kama Shilingi 400 milioni kwa ukarabati huu," alisema Waziri Mwakyembe.
Kwa mujibu wa meneja wa Uwanja wa Azam Complex, Sikitu Kilakala, ukarabati huo umefanyika kwa kufuata maelekezo na maagizo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
"Ukarabati kama mnavyouona umekamilika na sasa tunasubiri tu wakaguzi kutoka CAF waje kufanya ukaguzi wa mwisho tayari kwa mashindano," alisema Kilakala.
Uwanja huo wa Azam Complex utatumika kwa mechi sita za hatua ya makundi ya mashindano hayo.
Mechi tano zitakuwa za kundi B linalojumuisha timu za Cameroon, Guinea, Morocco na Senegal na mechi ya mwisho ya kundi A baina ya Nigeria na Uganda.