Ufunguzi AFCON kiboko

SHEREHE za ufunguzi wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu nchini Misri zilizofanyika nchini Misri juzi, zimeandika historia mpya kutokana na namna zilivyogeuka kivutio kwa mamilioni ya wadau na wapenzi wa soka duniani walioshuhudia moja kwa moja wakiwa uwanjani au kwenye luninga.
Idadi ya vigogo wa soka na viongozi wa kisiasa walioshiriki sherehe za ufunguzi, burudani na maonyesho yaliyoambatana na tukio hilo pamoja na kiwango cha soka kilichoonyeshwa na Misri na Zimbabwe ambazo ziliumana, vimebaki kuwa gumzo kwa wengi.
Moja ya matukio yaliyovutia wengi ni namna Misri ilivyotumia sherehe hizo za ufunguzi zilizofanyika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, kuonyesha utamaduni na vivutio vya utalii vilivyomo nchini humo hasa Mapiramidi ambayo waliokuwa Wafalme wa nchi hiyo 'Mafarao' wamezikwa.
Mbali na hilo, kulikuwa na shoo za vikundi mbalimbali vya burudani pamoja na wasanii maarufu barani Afrika wakiwemo mwanamuziki maarufu wa Nigeria, Femi Kuti, staa wa muziki nchini Misri, Hakim pamoja na msanii kutoka Ivory Coast, Dobet Gnahore walipamba sherehe hizo zilizoanza mnamo saa 2.30 usiku.
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Ahmad Ahmad waliuongoza umma wa wapenzi wa soka kushuhudia ufunguzi huo wakiungana na Rais wa Misri, Abdel Fattah Al-Sisi na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi.
Sherehe hizo za ufunguzi wa mashindano hayo mwaka huu zilihitimishwa kwa mchezo baina ya Misri na Zimbabwe ambao ulimalizika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililopachikwa na Mahmoud Hassan 'Trézéguet' dakika ya 41.