Ufalme wa Makapu Yanga una mengi nyuma yake

Wednesday March 25 2020

Mechi kadhaa tu zimempa ufalme Yanga,mkabaji wa Yanga, Said Juma Makapu,elvin Yondani , Ally Mtoni ‘Sonso’,

 

By Thobias Sebastian

UNAKUMBUKA ule msamiati, kila jambo na wakati wake. Ndio limetokea kwa kiungo mkabaji wa Yanga, Said Juma Makapu baada ya hapo misimu kadhaa nyuma kuonekana mchezaji wa kawaida kabla ya sasa kuonekana lulu ndani ya klabu hiyo.

Makapu anayeitumikia klabu hiyo kwa mwaka wa tano sasa, alijiunga nayo mwaka 2015 akitokea klabu ya Shangani ya Visiwani Zanzibar.

Hata hivyo, msimu pekee aliofanya vizuri ilikuwa mwaka 2017, Yanga ikiwa chini ya Kocha Mzambia, George Lwandamina na alikuwa akimwanzisha kikosi cha kwanza eneo la kiungo na kumweka benchi nyota wa kigeni Thaban Kamusoko.

Baada ya hapo, hakuwa tegemeo tena na amekuwa ni mchezaji wa benchi na wakati mwingine hakuonekana uwanjani hadi alipokuja Kocha Luc Eymael msimu huu na kuona kiwango chake mazoezini na amekuwa akimtumia mara kwa mara kikosi cha kwanza na kuwaweka benchi mabeki kama Kelvin Yondani na Ally Mtoni ‘Sonso’.

Makala haya yanakuletea mambo kadhaa ya Makapu tangu kuwasili kwa Kocha Eymael.

KUTEMWA

Advertisement

Wakati Eymael anatua Jangwani alikutana na orodha ya nyota wanaotakiwa kutemwa au kutolewa kwa mkopo na miongoni mwao alikuwepo Makapu.

Hata hivyo, Eymael baada ya kuanza kazi aliomba wachezaji wote wawepo katika mazoezi ya kwanza chini yake yaliyofanyika Chuo cha Sheria na kutokana na kiwango chake akicheza kwenye nafasi mbili za beki wa kati na kiungo mkabaji na kumvutia Eymael aliyeamua kumbakisha kikosini.

NIDHAMU YAMBEBA

Makapu kwa kawaida si mzungumzaji na hata ilipofichuka atatemwa Yanga, hakuzungumza chochote hata kwenye vyombo vya habari.

Hii ni utokana na nidhamu yake na ndio imemfanya akae na klabu hiyo kwa muda mrefu hadi kufikia wakati huu anapata nafasi tofauti na awali alikuwa anaonekana si lolote na kuishia benchi.

Kutokana na nidhamu hiyo, Kocha Eymael aliliambia Mwanaspoti kwenye timu zote alizowahi kufundisha pamoja na kiwango bora, pia anapenda nidhamu ya aina hiyo na anapenda kufanya kazi na wachezaji wa aina hiyo.

“Kwangu nidhamu ni jambo la kwanza kwani naamini ili kufanikiwa na timu kufikia malengo kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa kuonyesha nidhamu ya hali ya juu,” anasema Eymael ambaye amekuwa mkali akisimamia vyema suala hilo ndani ya kikosi chake na kusisitiza katika mambo yaliyomkosesha Kelvin Yondani namba kwenye kikosi chake ni nidhamu na ndio hapo alipopatia mwenzie.

HANA MAMBO MENGI

Makapu ambaye kiasili ni kiungo mkabaji licha ya sasa kocha wake Eymael kumtumia kama beki wa kati ameonekana si mchezaji wa mambo mengi anapokuwa uwanjani kwani ni nadra kumuona akiwa na mpira zaidi ya sekunde tano.

Akicheza kama kiungo mkabaji muda mwingi huwa anazunguka katika maeneo mengi kubaka viungo wa timu pinzani, hushuka chini kuwasaidia walinzi kukaba, mzuri katika matumizi ya nguvu lakini anaweza kupokonya mipira mingi kwa wachezaji wenye uwezo wa kumiliki mpira kama Claytous Chama wa Simba.

Makapu akiwa na mpira katika miguu yake ni nadra sana kumuona akiwa nao zaidi ya sekunde tano kwani akiwa nao huwa anatulia na kupeleka pasi ndefu au fupi kwa mchezaji mwenzake na si kama viungo wengine wakabaji wakiwa na mpira lazima wakae nao ndani ya sekunde kadhaa.

Jambo hilo la kutokuwa na mambo mengi huwa analifanya hata akicheza katika nafasi ya beki wa kati Makapu huwa anagusa mpira mara moja au mbili kama kuokoa kwa kichwa anafanya hivyo au kama kuokoa na mguu huwa anafanya hivyo na si beki mwenye kuonyesha madaha hata mara moja.

Ukiangalia viungo wote wakabaji na mabeki wa kati wa Yanga wanapenda kufanya madaha na kumiliki mpira hata sekunde kadhaa wakiwa uwanjani lakini kwa Makapu hilo halipo huenda jambo hilo ni miongoni mwa vitu ambavyo vinamvutia Eymael na kumpa nafasi.

YONDANI

Haikuwa kazi rahisi kuona kikosi cha Yanga kinacheza mechi zaidi ya tatu huku kikimkosa beki wao wa kati Kelvin Yondani tena akiwa mzima bila ya majeraha au tatizo lolote lakini chini ya Eymael limewezekana hilo tena mpaka katika mechi kubwa hapa nchini dhidi ya Azam na Simba.

Kukosekana kwa Yondani katika mechi za mwanzo kulileta baadhi ya maneno kwa mashabiki na viongozi wa timu hiyo lakini Eymael aliziba masikio na nafasi hiyo kumpatia Makapu ambaye amekwenda kuifanyia kazi ipasavyo mpaka kuwafanya wale waliokuwa wakimbeza kumshangilia.

Mechi mbili dhidi ya Azam pamoja na Simba ambazo Makapu alianza katika kikosi cha kwanza na kuonesha kiwango bora ndio kilimuhakikishia zaidi nafasi beki huyo ambaye alikuwa akionekana wa kawaida na hakuwahi kuwa midomoni mwa mashabiki.

Kiwango cha Makapu hususani kwenye mechi ya watani ambayo Yanga ilishinda bao 1-0 kiliwafurahisha mashabiki wengi wa Yanga huku wakidai ni miongoni mwa hazina zijazo za Stars.

KUITWA STARS

Aliitwa Taifa Stars iliyokuwa inajiandaa kucheza mechi za Chan na kufuzu fainali za mataifa Afrika (Afcon).

Mara ya mwisho kuitwa Stars ilikuwa mwaka 2015,enzi hizo ikiitwa Taifa Stars Maboresho.

NINJA AMWELEZEA

Beki wa timu ya FK Rigas Futbola Skola ya nchini Latvia, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ anasema Makapu ana uwezo wa kucheza kama kiungo mkabaji na muda huu aliopata nafasi ya kucheza kama beki wa kati tena akimuweka nje mchezaji mzoefu Yondani anatakiwa kuongeza umakini na ukomavu wa hali ya juu kila mabpo anapokuwa uwanjani.

“Sina mashaka na uwezo wa Makapu kama anaweza kucheza katika nafasi ya kiungo basi nafasi ya ulinzi wa kati ataimudi kwani nafasi hiyo haitaki mambo mengi zaidi ya kuokoa na kuwalinda washambuliaji wa timu pinzani, namwona mbali mno anaweza kuwa lulu kama ataendelea kufanya zaidi ya sasa,” alisema.

“Nikiwa Tanzania amekuwa akiniomba nimpatie mazoezi ya beki wa kati, anatakiwa kufanya mambo yapi na mazoezi mengi ambayo nilikuwa nikimpatia amekuwa akifanya vizuri kwa maana hiyo namuona akiendelea kudumu katika kikosi cha Yanga huku akifanya vyema,”anasema Ninja ambaye ni tegemeo kwenye Zanzibar Heroes.

Advertisement