UKWELI NDIVYO ULIVYO: Kipigo sio hoja, ila Simba ijipange

JIONI ya Alhamisi kwenye mitandao ya kijamii kulijaa vurugu. Vurugu zilizojaa ule utani wa Simba na Tanzania kwa bao 1-0. Ulikuwa ni ushindi wa tano mfululizo katika Ligi Kuu Bara.

Halafu sasa watani zao, Simba walikuwa wamepasuka ugenini mjini Sumbawanga. Maafande wa Yanga. Mashabiki wa Yanga walikuwa na furaha ya ushindi kwa timu yao. Yanga waliifumua Polisi Tanzania Prisons waliicharaza kwa bao 1-0.

 

Bao tamu la kichwa lililowekwa kimiani na Samson Mbangula mbele ya Mkenya Joash Onyango zilizima kelele zote. Zile kelele za kwamba Msimbazi kwa sasa inapiga pira biriani... sijui pira pishori na haizuiliki labda icheze na timu kama Barcelona, Liverpool na kadhalika.

Kelele hizo zote zilizimwa na pira gwaride kama walivyojinasibu nyota wa Prisons na kuwapa fimbo.

Yanga kuwakejeli. Kejeli zilizowajaza upepo wenzao wa Msimbazi hadi kufikia kuanza kuwalaumu nyota wao. Wanamlaumu kipa Aishi Manula. Wanaona alifungwa bao kizembe kwa kutoka langoni bila ya taimingi.

Wanawapiga madongo kina Charles Ilanfya, Miraj Athuman, Hassan Dilunga na wachezaji walioanzishwa kwenye mchezo huo ukimuondoa Luis Miquissone kwa namna walivyocheza ovyo.

Ndio mashabiki wa klabu hizi za urithi zenye masikani yake Kariakoo walivyo. Hawapendi kusikia au kuona timu zao zikifungwa. Wameaminishwa timu zao ni bora. Lakini ukweli haupo hivyo. Soka hata uwe bora kiasi gani bado timu hufungika. Soka ni mchezo wa makosa.

Beki ya Simba ilifanya uzembe ikaadhibiwa. Kama ilivyoadhibiwa Polisi kwenye Uwanja wa Uhuru. Tayari kuna watu watamuona Kocha Sven hafai, lakini wanasahau, Real Madrid wikiendi iliyopita ilichapika mbele ya timu iliyopanda daraja katika La Liga, Cadiz CF. Siku chache tena ikakumbana na kipigo kingine kutoka Shakhtar Donetsk kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hao hao Yanga walikuwa wakiibeza Simba, siku chache zilizopita walikuwa wakikosa raha na kelele za wenzao wa Msimbazi. Sare dhidi ya Prisons kwenye mechi ya ufunguzi wa msimu na soka lisilovutia chini ya Zlatko Krmpotic liliwafanya wakose amani. Mabosi wao wakasikiliza kelele zao wakamuondoa Mserbia huyo na kumleta Cedric Kaze. Kwa sasa mashabiki wa Jangwani wana matarajio makubwa kwa Kaze. Wanaona kama Nabii flani aliyekuwa kuwakomboa.

Ikitokea wakapoteza mechi yoyote, upepo utabadilika. Ndivyo soka la Kibongo lilivyo. Mashabiki na hata viongozi hawangalii chochote ila kutaka timu zao zishinde. Haijalishi vikosi vyao kama ni vipya ama kocha ni mpya. Wanajenga dhana kwamba soka ni kama mtu kukoroga chumvi katika mboga na kukolea fasta.

Wanasahau soka ni sayansi inayohitaji muda kupata matokeo chanya. Bahati mbaya ni kwamba klabu zote zimekuwa zikiaminishwa, timu zao zina vikosi vipana na nyota wanaoweza kuvaana na timu yoyote na kupata ushindi tu. Ila ukweli ni kwamba timu zote zilizopo Ligi Kuu Bara hazichekani.

Zinatofautiana tu ukubwa wa majina na labda kiuchumi tu, lakini kisoka uwanjani tofauti zao huwa ndogo sana.

Kwa waliofuatilia mechi zote za Alhamisi, kama ni mtu mgeni na hazijui Simba na Yanga, ni rahisi kuamini Polisi ndio waliokuwa Yanga, huku Prisons wakidhania ndio Simba kwa jinsi wakongwe walivyozidiwa.

Ila kuna kitu ambacho lazima Wanasimba wanapaswa kujua. Kipigo cha Prisons kiwazindua sasa kwa kujua lazima wajipange kwelikweli kabla ya kuanza mechi za kimataifa. Kukosekana kwa nyota sita tegemeo wao, Clatous Chama, Pascal Wawa, John Bocco, Meddie Kagere, Chris Mugalu na Fraga Gerson, kulionekana wazi kwenye mchezo huo wa Sumbawanga.

Huwezi kuwalaumu sana kina Erasto Nyoni, Hassan Dilunga, Miraj Athuman na Charles Ilanfya kwa walivyocheza. Wachezaji wasiopewa nafasi ya kutumika mara kwa mara kikosini lazima wapoteze kujiamini. Lazima wawe na presha, kiasi cha kushindwa kuonyesha ubora wao. Ila ukweli ni kwamba timu yenye kuwategemea wachezaji flani tu, siku wakikosekana hutibua kila kitu.

Pia ni wazi ndani ya kikosi chao cha sasa kuna wachezaji ambao wanaweza kuwaangusha kama watawategemea kwenye mechi za kimataifa, pale kina Chama, Kagere na wenzao watakapokosekana kwa sababu mbalimbali.

Kwa kuwa katika soka kuna ishu za kupewa kadi, kuumia ama matatizo mengine binafsi yanayoweza kumuondoa mchezaji nyota ndani ya kikosi, ni lazima Simba ianze mapema kutafuta plan B ili mambo yasije yakawachachia pale wanapokutana na mziki wa kina Al Ahly, TP Mazembe, Mamelodi Sundowns ama Wydad Casablanca wanaoweza kukutana nao CAF.

Timu ambazo zimekuwa zikiundwa na nyota wenye viwango vya juu na kiu kubwa ya mafanikio kwa timu zao, hata ni kweli huwezi kuanza kuihukumu Simba kwa sababu ya matokeo dhidi ya Prisons, lakini ukweli ile dhana ya Simba ina kikosi kipana inakataa mchana kweupeee! Ni mtazamo tu!