UCHAMBUZI: Tusapoti kikapu ili tumuenzi Mbamba Uswege

Thursday October 15 2020

 

Tanzania kuna michezo mingi inayopendwa na watu ukiachana na mpira wa miguu ambao ni mchezo pendwa ulimwenguni ila kuna riadha, ngumi, kikapu, wavu na mingine mingi tu.

Mbali na kwamba michezo hiyo haina wadau wengi, lakini miongoni mwayo ndio michezo iliyoiletea medali Tanzania kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Olimpiki upande wa riadha.

Wiki hii, Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam maarufu kama RBA inamalizika ambapo ilishirikisha zaidi ya timu 10 kumpata bingwa wa ligi hiyo.

Kuna timu kongwe ambazo zimeshiriki ligi hiyo kama Pazi, Vijana, JKT na hata zile ambazo zilifanya vizuri miaka ya nyuma tangu ligi hiyo ianze katika miaka ya 1992 na 1993 ikiwa na mwanzilishi wake, hayati Mbamba Uswege kama Savio na UDSM Outsider.

Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni ligi hiyo imekuwa ikikosa mvuto na imekosa udhamini hata zile amsha amsha zimepungua.

Kwa sasa ligi inachezwa kwa sababu kuna ratiba inayopaswa ifuatwe maana ni kama wanajitolea tu.

Advertisement

Miaka ya nyuma hata wachezaji walicheza kwa kujituma zaidi ukiachana na wale waliochezea timu za jeshi kama JKT na Mgulani ambao kwao ni ajira - walilipwa na jeshi tofauti na timu zingine zilizo chini ya watu binafsi.

Lakini wachezaji walifurahia maisha ya mchezo huo kwa sababu udhamini ulikuwepo na walipewa posho na zile zawadi zilizokuwa zinatolewa kila wiki ilikuwa moja ya motisha kwao kupambana zaidi.

Hakika RBA iliifunika hata mashindano ya kitaifa ambayo yanasimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF), ambapo RBA ilionekana kama yenyewe ndio ligi kubwa nchini.

Baada ya udhamini kuondoka kila kitu kilianza kubadilika, zawadi kwa wachezaji zilianza kuadimika ambapo hadi sasa sidhani kama zipo.

Hakika mpira wa kikapu unapaswa kurejeshwa hasa wadau kutoa sapoti kama ilivyo kwa michezo mingine.

Uongozi thabiti ndio unaotakiwa kuongoza sehemu yoyote ili wadhamini wajitoe kuwekeza pesa zao wakiamini kwamba ziko kwenye mikono salama - maana hili ndilo tatizo lililoonekana kuchangia udhamini kuondoka kwenye kikapu.

Lakini kuna nafasi bado ya kutengeneza na kurudisha udhamini kama lengo na nia ni moja. Hili la kurudisha wadhamini linawezekana ingawa mpaka sasa udhamini wanao ila si kwa kiwango ambacho RBA wangekuwa nacho hivi sasa.

Uongozi wa Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (DB) unapaswa sasa kuingia chimbo kupanga mikakati ya namna gani watatoka RBA ijayo kwa kupata udhamini mnono.

Nadhani kuna haja ya kujitoa hasa kama walivyokuwa wanajitoa waanzilishi wa RBA.

Kingine ni kwamba katika imani wanasema mtu akifariki dunia huona yanayoendelea, hivyo hata hayati Mbamba atakuwa anaona yanayoendelea kwenye RBA na kusikitika, basi DB wanapaswa kufanya jambo lingine la kumuenzi Mbamba aliyefariki kwa ajali ya gari miaka michache tu baada ya kuanzisha RBA yenye mafanikio. Hayati Mbamba amesahaulika katika anga ya mpira wa kikapu, hakuna anayemuenzi sasa wala hasikiki ni kama vile waanzishi wa mchezo huo ni hawahawa waliopo sasa.

Ni vyema lifufuliwe kombe la Mbamba Uswege japo hata kwa kuchezwa kwa wiki hata mbili tu ikiwa ni ishara ya kumuenzi na kuuthamini mchango wake katika kuubeba mpira wa kikapu nchini.

 

Advertisement