UCHAMBUZI: Thamani ya wachezaji sokoni bado ipo juu

HAKUNA binadamu yeyote anayeishi duniani ambaye hajaguswa na madhara ya kiuchumi yaliyotokana na uwepo wa corona ambao umesababisha biashara mbalimbali kukwama hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa dunia.

Janga hilo lilipelekea vitu vingi kubadilika duniai hadi utaratibu wa maisha ambao tulikuwa tumezoea kuutumia katika maisha ya kila siku umebadilika kutokana na janga la corona.

Tunavyozungumzia biashara kuathirika ni biashara aina zote kuanzia za vitu hadi huduma kwani biashara zote hutegemeana.

Katika dunia ya sasa ikumbukwe kuwa mchezo wa soka unaendeshwa kibiashara, hivyo unatambulika kama bidhaa ambayo huingizwa sokoni kwa ajili ya kutengeneza faida kama zilivyo bidhaa nyingine.

Na soka pia iliathirika kutokana na uwepo wa janga hilo na kusababisha baadhi ya mataifa kuahirisha hadi michezo ya ligi mbalimbali, hiyvo kukosa kipato ambacho hutokana na biashara hiyo.

Baada ya ligi mbalimbali kurejea hivi karibuni dirisha kubwa la usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu wa 2020/2021, lilikuwa limefunguliwa ambapo tumeshuhudia klabu zikifanya usajili wa wachezaji.

Tukiangalia barani Ulaya tena katika Ligi Kuu ya soka England, tumeona usajili wa wachezaji ambapo umeshuhudiwa dirisha la usaili likifungwa wiki iliyopita, huku baadhi ya klabu zikitumia fedha nyingi kusajili wachezaji ambao kwa jicho la kibiashara wanatambulika kama bidhaa zilizopo sokoni - ndio maana huuzwa.

Ukiangalia usajili wa baadhi ya wachezaji katika Ligi Kuu England kwa msimu huu utagundua kuwa licha ya uwepo wa janga la corona ambalo limeathiri uwezo wa kifedha wa mashirika na kampuni mbalimbali za kibiashara, lakini katika mchezo wa soka bado bidhaa ya wachezaji imeendelea kubaki katika thamani yake ileile sokoni kiasi cha klabu kuweza kutumia fedha nyingi kusajili wachezaji.

Ukiangalia usajili wa wachezaji watano waliosajiliwa kwa gharama kubwa katika ligi hiyo utaona kuwa thamani ya bidhaa ya wachezaji wa soka haijaathiriwa kwa kiasi kikubwa na janga hili kama zilivyoathiriwa bidhaa nyingine katika soko.

Tofauti hiyo kati ya bidhaa hii ya wachezaji na nyingine sokoni ipo kwa kuwa ni kazi rahisi kupata gharama ya kutengeneza au kuzalisha bidhaa na kujua gharama halisi ya uzalishaji na usafirishaji wa kuifikisha sokoni, hivyo kuwa na bei halisi ya kuiuza au kuinunua bidhaa husika.

Hii ni kwa kuwa na mzalishaji kujipangia kiasi cha faida kwa kuongeza asilimia fulani kwa kila bidhaa tofauti na bidhaa za wachezaji ambazo bei zake sokoni zinatokana na kiwango cha upungufu wa kiuchezaji katika timu, na njaa ya mafanikio ambayo hutofautiana kati ya timu moja na timu nyingine.

Hivyo hufanya bei za wachezaji sokoni kuwa huru na kutoratibiwa na taasisi yoyote zaidi ya timu inayouza na ile inayonunua.

Kwa mfano timu ya Chelsea ndio imenunua mchezaji kwa gharama kubwa zaidi kuliko timu zote baada ya kumsajili Kai Haverts kutoka Bayer Leverkusen kwa kiasi cha Uro Milioni 71 ambazo ni sawa na Sh193 bilioni za Tanzania.

Hivyo Haverts ndiye mchezaji aliyeongoza kuwa na thamani kubwa kuliko wachezaji wote waliosajiliwa na klabu zote vya soka nchini Uingereza katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha kubwa.

Mchezaji aliyeshika nafasi ya pili kwa kusajiliwa na fedha nyingi ni Ruben Dias aliyesajiliwa na Manchester City akitokea timu ya Benfica ya Ureno ambapo amesajiliwa kwa kiasi cha Euro milioni 62 ambazo ni sawa na Sh169 bilioni huku mchezaji aliyeshika nafasi ya tatu kwa kusajiliwa na fedha nyingi akiwa ni Timo Werner aliyesajiliwa na Chelsea akitokea katika timu ya RB Lepzig ya nchini Ujerumani ambapo amesajliwa kiasi cha Euro 48 milioni ambazo ni sawa na Sh130 bilioni.

Nafasi ya nne imeshikwa na wachezaji watatu ambao ni Tomas Partey aliyesajiliwa na Arsenal kwa kiasi cha Euro 45 milioni ambazo ni sawa na Sh122 bilioni akitokea katika timu ya Atletico Madrid ya Hispania, Diogo Jota aliyesajiliwa na Chelsea akitokea timu ya Wolves kwa gharama za Euro45 milioni pamoja na Ben Chilwell aliyesajiliwa na timu ya Chelsea akitokea timu ya Leicester City kwa Euro45 milioni.

Huku nafasi ya tano ikishikwa na Nathan Ake aliyesajiliwa na timu ya Manchster City kwa kiasi cha Euro 41 milioni ambazo ni sawa ni Sh111 bilioni akitokea timu ya Bournemouth ya Uingereza.

Hivyo ukiangalia fedha halisi iliyotumika kusajili wachezaj hao saba katika klabu za Chelsea, Arsenal na Mancester City ambazo kwa fedha za Kitanzania ni zaidi ya Sh770 bilioni utaona kuwa bei ya wachezaji sokoni haijaathiriwa kama zilivyoathiriwa bidhaa nyingine kutokana na janga la corona.

Hivyo, katika biashara ya wachezaji tunasema kuwa bei hupangwa na hutokana na uhitaji wa mchezaji na njaa ya timu ya kutwa mataji.

Katika hili kuna jambo la kujifunza katika ligi zetu za Afrika ikiwamo Tanzania juu ya namna soko la usajili linavyojipanga na kujiamulia lenyewe.