UCHAMBUZI: Morrison, mtata anayekumbusha mabadiliko Yanga

Thursday July 16 2020

 

By KHATIMU NAHEKA

Adui mkubwa sasa ndani ya klabu ya Yanga ni shujaa wao, Bernard Morrison, ambaye mashabiki na wanachama wanaonyesha kuchoka vurugu za mchezaji huyo kwani kila siku mpya amekuwa na jipya katika maisha yake ndani ya klabu hiyo.

Morrison amezidi kuonyesha sura halisi ya akili yake na kwanini huko alikopita amekuwa hadumu kwa muda mrefu, na akiwa Yanga amekuwa na vurugu tofautitofauti kuliko utulivu kwa sasa, kila siku mpya amekuwa na filamu mpya ndani ya klabu hiyo.

Sishangai anayoyafanya Morrison ndani ya Yanga kwani hakuna jipya ni yaleyale ambayo aliyafanya akiwa nchini DR Congo.

Lakini pia, ni yaleyale aliyoyafanya akiwa Afrika Kusini bahati mbaya sana Yanga waliamua kuishi na Morrison kama mfalme mpya na hapo ndipo makosa yalipoibukia ndani ya klabu hiyo.

Wala Morrison hatakiwi kulaumiwa sana na mashabiki wa Yanga, kwani anaishi maisha yake halisi ndani ya klabu hiyo.

Pengine kama watatafuta wa kumlaumu, basi utakuwa ni uongozi wa klabu hiyo ambao kuna mengi umekosea na sidhani kama wanajua wapi wamekosea.

Advertisement

Yanga imeanguka kwa kukosa utendaji wa kiuongozi, na hili narudia kuliandika hapa kuwa Yanga haina utendaji mzuti katika masuala ya klabu ambao ulipaswa kutulia katika kumsajili Morrison na waingie naye mkataba wa aina gani, na kisha waishi naye vipi ndani ya klabu yao.

Walipaswa kwanza kujua wanamsajili mchezaji wa aina gani kwa kutangulia tu kujiuliza mchezaji mwenye ubora kama wake kwanini wamkute hana timu wamsajili akitokea katika makochi ya nyumbani kwake?

Wangejiuliza hili haraka wangepata majibu ya haraka ya kwamba ni aina gani ya mkataba wanatakiwa kumpa mchezaji huyo ili waishi naye kwa mazingira salama, bahati mbaya sana wakaamua kumsikiliza yeye akiwaeleza anaonewa tu kila anakokwenda.

Morrison ananufaika na udhaifu wa kiutendaji wa klabu hiyo haujui unatakiwa kumfanya nini mchezaji huyo na unyonge wao huo unawafanya sasa kuendelea kumuani zaidi katika kikosi chao na moto wake ndio wanaouona.

Ukifuatulia matukio ya Morrison unapata picha halisi kwamba Yanga inatakiwa kwanza kutafuta uongozi hawa wa sasa wamechoka mapema - tena wakiwa safarini na sioni kama wataweza kuifikisha klabu hiyo sehemu wanayotakiwa kwenda,utulivu mkubwa ambao uongozi wa Yanga unaupata ni kuamua kuishi katika kivuli cha wadhamini wao GSM.

Haya yanayotokea sasa ni pale ambapo sasa ikitokea GSM nao wakateleza kidogo basi klabu kubwa inaanguka,mambo mengi yanaendeshwa kienyeji sana ndani ya klabu hiyo na sasa dosari kubwa zimeanza kujitokeza hadharani.

Kama Yanga hawatashtuka na udhaifu wa uongozi wao kuna kubwa linaweza kuja kujitokeza hata kuipasua timu yao kwa matabaka hasa katika kikosi chao kutokana na kila mchezaji ndani ya klabu hiyo kuweza kufanya kama anachofanya Morrison kwa kuwa hawatakuwa wanaridhika na hatua ambazo zinachukuliwa katika kutatua mgogoro uliopo.

Hatua mbaya zaidi ni kwamba mpaka sasa katika vurugu zote ambazo Morrison amekuwa akizisababisha katika kikosi hicho, hakuna tamko lolote limetolewa katika kuwaeleza kipi kinaendelea kati ya uongozi wa klabu hiyo na mchezaji huyo, huku wakijua fika kwamba mashabiki na wanachama wao wanaumizwa na hali inayoendelea.

Katika maisha ya namna hiyo ni lazima mafanikio yajiweke kando na kuacha matatizo yatangulie, na sioni kama Yanga itakuja kuinuka sasa kama itaendelea kuishi katika maisha ya kiutendaji uliopo sasa ambao wengi wao wanaonekana wazi kwamba hawakuwa watu sahihi kuiongoza klabu hiyo kama ambavyo waliaminiwa wakati wanaomba ridhaa.

Advertisement