UCHAMBUZI: Mfalme Okwi alipiga mpira, Morrison anafanya dharau

Thursday July 16 2020

 

By Mwanahiba Richard

Achana na matokeo ambayo Simba waliyapata dhidi ya Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC). Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 na hivyo kutinga fainali ambapo watacheza na Namungo FC - fainali ikiwa imepangwa kufanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Nelson Mandela mjini Sumbawanga.

Lakini matokeo hayo ni kama vile hayajawashtua wengi kwani inaonekana kama yalitarajiwa na pengine hata ushindi wa zaidi ya hayo kulingana na vikosi vya timu hizo pinzani. Kikubwa ambacho kinazungumzwa kwasasa kuliko hata matokeo yenyewe ni kitendo cha mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison alichokionyesha siku hiyo na kimetafsiriwa kama ni kitendo cha utovu wa nidhamu.

Katika mechi hiyo, kiukweli Morrison alicheza chini ya kiwango tofauti na michezo mingine aliyocheza ndani ya Yanga hata ile mechi ya ligi ikiwemo ya watani hao ambapo alifunga bao 1-0.

Hakuna shabiki ambaye hakuona ubovu wa kiwango cha mchezaji huyo kwa siku hiyo huku wengine wakifika mbali zaidi kwamba hakukuwa na sababu za kumpanga kikosini kutokana na mwenendo wake wa sasa ndani ya Yanga lakini yote huachiwa kocha kuamua nani ampange siku hiyo.

Nadhan hata kocha wa Yanga Luc Eymael atakuwa anajuta kwanini alimpanga mshambuliaji huyo ambaye kwa namna moja ama nyingine amemdharua hata yeye aliyempa nafasi ya kucheza.

Timu inapozidiwa kocha ndiye huamua ni namna gani afanye ili apate matokeo, pengine ndiyo maana Luc aliamua kumtoa nje Morrison baada ya kuona kiwnago chake hakimridhishi na kumwingiza Patrick Sibomana.

Advertisement

Kitendo hicho ndicho kilimfanya Morrison akasarike na kutoka uwanjani moja kwa moja wakati sheria alitakiwa arudi kwenye benchi kama ilivyokuwa kwa Haruna Niyonzima ambaye alipofanyiwa mabadiliko ingawa hakuonyesha kuyafurahia lakini alikwenda kukaa kwenye benchi na wenzake.

Kikubwa ninachokiona kwa Morrison pengine viongozi wa Yanga hawakukiona walipokuwa wanamsajili ni usumbufu, dharau, kiburi na jeuri alivyonavyo.

Haikatazwi kwa mtu yeyote kuwa na misimamo yake katika maisha lakini wakati mwingine misimamo ikizidi unaikosea jamii kama alivyoikosea Morrison ambaye amejiona ni mfalme ndani ya Yanga na jamii ya wapenda soka.

Kuna habari za chinichini ambazo zinadai Simba wanamuwinda mchezaji huyo ambaye mkataba wake wa awali na Yanga umemalizika, lakini Morrison akae akijua kwamba kama kweli atatua Simba kiburi alichonacho akiache huko Yanga.

Maisha ya hizi timu mbili ni kama yanafanana kwa kiasi kikubwa, hawapendi dharau, hawapendi mchezaji kujiona yeye ni mkubwa kuliko klabu, huko atakwenda kupotea kabisa katika ubora wake.

Kama hii ni tabia yake ambayo pengine hairekebishiki basi hata huko atakakokwenda atawasumbua vile vile na ndipo hapo atakapoona mpira wa Tanzania sio rafiki kwake.

Kama Morrison ameonyesha dharau kwa benchi la ufundi la Yanga, wachezaji wenzake na viongozi ambao walionekana mwanzo kumkumbatia basi itakula kwake mazima huko atakakokwenda ambako sasa wanataka kazi kazi tu.

Hizi dharau za wachezaji pia ziwafunze viongozi wenye kukumbatia ‘majipu’ ndani ya timu kisa tu wao ndiyo walisajili, wao ndiyo walibembeleza usajili wa nyota fulani, madhara yake ni kama hayo ya kuwavua nguo.

Kiongozi hapaswi kujishusha ama kunyenyekea kwa kiasi hicho kwa mchezaji ambaye unamlipa na huduma zingine unamfanyia, viongozi wa Yanga walijishusha na kumuogopa Morrison.

Viongozi watimiza wajibu wao kwa mchezaji naye atimize majukumu yake, vingine mtadharaurika sana na wachezaji wenye tabia kama za Morrison.

Morrison nikukumbushe tu, miaka iliyopita kabla Simba haijabadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu kutoka wanachama kwenda kampuni, kuna kijana aliitwa Emmnauel Okwi, alijua kuzitumia vizuri akili za viongozi wa Simba.

Okwi aliishi ndani ya Simba kama mfalme hadi akaitwa Mfalme Okwi, lakini ufalme wa Okwi ulionekana hadi uwanjani alijuwa kusawazisha makosa yake, Okwi alikuwa anajitambua kuwa akifanya kosa ili kosa lake lifutike ni kuonyesha kiwango bora uwanjani.

Lakini haipo hivyo kwa Morrison, alianza kuvurugana na viongozi wake hadi uwanjani anaamua kuwakomesha, hivyo ukiondoka Yanga basi tarajia kwamba unaweza kukutana na timu yenye viongozi kiburi kuliko wewe.

Advertisement