UCHAMBUZI: Ligi iko vizuri, hakuna konakona

Tuesday October 20 2020
uchambuzi pic

Ni msemo wa Twaha Kiduku ukiupamba mchezo wa masumbwi ambao kwa kweli amerejea kwa kishindo kizito sana hapa nchini.

Siyo mbaya misemo ya michezo mingine ikatamalaki kwenye soka, kwa sababu hiyo ndiyo asili ya mchezo huu.

Neno hat trick asili yake ni mchezo wa kriketi, lakini limetamalaki kwenye soka.

Ligi ya Tanzania inaingia raundi saba ambapo leo, Jumanne ya Oktoba 20 kutakuwa na michezo kadhaa ikiwemo Ihefu SC dhidi ya Ihefu SC saa nane mchana katika Uwanja wa Sokoine huko Mbeya.

Hadi kufikia raundi hii mwendo wa ligi bado uko vizuri ukiachilia mbali mvurugano wa ratiba uliosababishwa na ratiba mpya ya kimataifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka duniani (Fifa), kuhusiana na michezo ya timu za taifa ambayo imechelewa kutoka na kukuta tayari ratiba ya Tanzania imetoka.

Azam TV, luninga yenye ya matangazo ya moja kwa moja inajitahidi kuonyesha mechi zote za kila siku ya mchezo. Ni dhahiri kwamba hakuna konakona.

Advertisement

Waamuzi wanajitahidi sana kutenda haki, ukiacha makosa madogomadogo ya kibinadamu ambayo hata Ulaya ambako ndiko tunakokimbilia kila siku kutolea mifano, yanatokea - tena licha ya wao kupatiwa vifaa vya kisasa vya kuwasaidia kupunguza makosa. Wachezaji wanatupa kile tunachohitaji kuona, yaani maarifa na jitihada.

Timu zinapambana kwelikweli uwanjani na kudhihirisha kwamba zilijiandaa na ligi kisawasawa.

Kwa sasa kushinda ugenini na kushindwa nyumbani kumekuwa kawaida tu.

Raundi hizi saba zinatoa picha ya matumaini kwa msimu mzima utakavyokuwa endapo wasimamizi wa ligi, bodi ya ligi, hawatakengeuka hapo baadaye.

Ratiba imepangwa vizuri kutoka kwa timu kusafiri na kupata muda wa kupumzika, kulingana na mazingira yetu.

Hii imetoa fursa hata kwa klabu kuwa na mechi nyingi za kirafiki katikati ya mechi na mechi za ligi kwa sababu muda unaruhusu.

Mechi hizi za kirafiki zinasaidia sana kuzijenga timu lakini pia kutoa nafasi kwa wachezaji ambao wamekuwa wakikosa muda wa kucheza - nao kupata wasaa.

Ligi ni mbio za marathoni ambazo mkimbiaji anahitaji kuwa na nishati mwilini mwanzo hadi mwisho ili kumaliza vizuri tena akiwa na ushindi mkononi.

Kunapokuwa na mechi mfululizo, wikiendi na katikati ya wiki, ni sawa na kukimbia marathoni kwa kasi ya mbio fupi ambazo huwezi kumaliza.

Kwa hiyo tuwapongeze wadau wote wanaohusika na ligi hadi sasa kwa mafanikio hayo.

LAKINI...

Uzoefu inaonyesha ligi yetu huharibika sana pale mbio za ubingwa na vita vya kukwepa kushuka daraja zinaposhika kasi zaidi, ambapo timu hupambana kwa kila hali kuweka mambo sawa.

Utaanza kuona mabao halali yakikataliwa au yaliyo haramu yakikubaliwa.

Hii ni shime kwa mamlaka, za kisoka na kiserikali, kama kweli tumedhamiria kuimarisha ligi yetu na kuifanya izidi kuwa bora kwa kulinganisha na majirani zetu, hatuna budi kujipanga kuhakikisha upungufu ulio ndani ya uwezo wetu anafanyiwa kazi.

Mazoea ya kuwakopa waamuzi kwa takribani msimu mzima yanachangia sana kuwafanya waingie vishawishi.

Haingii akilini waamuzi wanatoka majumbani mwao mathalan Tanga wanakwenda Mwanza kuchezesha mechi ya Ligi Kuu bila ya kupewa nauli wala pesa za kujikimu.

Inabidi wajinyime kile kidogo kwa ajili ya familia, huku wanakitumia katika kuusaidia mpira wetu.

Akitoka Tanga mwamuzi anapangiwa mechi nyingine Mbeya. Hali ni ile ile - mazingira haya ni hatarishi.

Hata angekuwa mtakatifu vipi, katika mazingira haya ni rahisi sana kushawishika na kuharibu mchezo.

Msimu huu hatujayasikia haya. Bila shaka ndio maana hadi sasa ligi inakwenda vizuri, hakuna konakona...mako dinda mako stamina.

 

Advertisement