UCHAMBUZI: Kwa huyu Donny van de Beek shida ni nini?

ILIANZIA kwa Paul Pogba. Walau yeye alikuwa anajua kipindi benchi lilipomhusu huko Old Trafford.

Hata wikiendi iliyopita alipoanzia benchi dhidi ya Chelsea wapo walioshangaa na wapo ambao hawakushangazwa.

Kinachoshangaza ni Donny van de Beek. Kuna shida gani? Bila shaka, hata yeye mwenyewe atakuwa anakuna kichwa kutafuta namna gani ya kufanya ili kuanza kupata nafasi ya kucheza kwenye timu.

Ole Gunnar Solskjaer alimfanyia ngumu Pogba kumfanya acheze kwenye kiwango bora. Alimwaanzishia benchi kwenye mechi nne mfululizo akiwa na maana ya kumtia hasira ili atakapopata nafasi aonyeshe uwepo wake uwanjani.

Jumamosi iliyopita Pogba na Van de Beek, wote walianzia benchi. Kitu kilichowashangaza zaidi ni kuona Solskjaer amemwaanzisha Daniel James. Kwenye mchezo ambao ulitarajia Man United kuwa na huduma bora ya wachezaji wake bora ndani ya uwanja ili kuwadhibiti Chelsea walionekana kwenda Old Trafford kutafuta sare, bado Solskjaer alichaguo kuwaweka nje wachezaji hao wawili.

Heri kwake Pogba yanaweza kuwa ni maisha ya kawaida. Kwa Van de Beek mambo yanaweza kuwa magumu. Kucheza dakika 61 kwenye Ligi Kuu England hadi sasa kwa timu hiyo alijiunga nayo kwa mapenzi makubwa, akiondoka Ajax alikokuwa nyota mwenye hadhi yake, inaibua mashaka na maswali mengi.

Katika mechi ambayo wengi walitamani kuona kitu gani Van De Beek atafanya kwa kukabiliana na timu ngumu kwenye ligi, Solskjaer aliamua kuanza na Juan Mata na Scott McTominay.

Na hata Mata alipoonekana kuchoka, Pogba ndiye aliyeingia na kumwaacha Van de Beek kwenye benchi akiwa mpweke. Solskjaer alimwambia Van De Beek kwamba nyakati zake zitakuja, lakini si kwa ushawishi wa kumtumia kwenye mechi za Kombe la Ligi tu.

Mbaya zaidi, wakati akiwa kama yatima jukwaani, timu yake ya zamani inacheza mechi na kushinda 13-0.

Bila ya shaka, si muda mrefu atayaona maisha ya Old Trafford machungu na kujilaumu kutua kwenye timu hiyo.

Patrice Evra hivi karibuni amehoji. Van De Beek alisajiliwa wa kazi gani? Kwa maana timu inacheza, inashindwa kufanya vizuri huku mchezaji huyo akiwekwa tu benchi na wakati mwingine anapewa dakika nne za kucheza.

Solskjaer kama hakuwa na ufahamu atamtumiaje Van De Beek asingefanya usajili wake.

Staa huyo ni muhimu kwa taifa lake na bado mchanga, hivyo anahitaji kujenga kisaikolojia kwa kuaminiwa na kupewa mechi kuliko kumvuruga akiwa kwenye umri mdogo huo. Ukizingatia hata pesa iliyotumika kunasa saini yake si ndogo.

Solskjaer hawaoni makocha wenzake Frank Lampard na Mikel Arteta. Hata Pep Guardiola na Jose Mourinho.

Wamekuwa wakitoa nafasi kwa wachezaji wao wapya kucheza. Sasa hii leo utawezaje kukosoa kiwango cha Van De Beek kwenye ligi kama kuchezeshwi? Solskjaer awaambia mashabiki wa Man United, nini shida ya Van de Beek.

Man United imekusanya pointi saba tu kwenye mechi tano ilizocheza kwenye ligi hadi sasa, imeshinda mbili, sare moja na vichapo viwili. Mashabiki wanahitaji kuona wachezaji wao wote mahiri wakipewa nafasi ya kucheza ili hata kama watashindwa kupata matokeo mazuri isiwe lawama za nani kacheza na nani hakucheza. Solskjaer hapaswi kukiharibu hiki kipaji cha Van De Beek ambacho dunia itapenda kukiona kwa miaka mingi ijayo.