Tuzo ya mchezaji bora Uingereza Rashford, Mane ndani

Muktasari:

MASTAA watatu wa Liverpool, Jordan Henderson, Sadio Mane na Trent Alexander-Arnold wametajwa kwenye orodha ya wakali saba watakaofukuzia tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu kwenye Ligi Kuu England.

 LIVERPOOL, ENGLAND

MASTAA watatu wa Liverpool, Jordan Henderson, Sadio Mane na Trent Alexander-Arnold wametajwa kwenye orodha ya wakali saba watakaofukuzia tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu kwenye Ligi Kuu England.

Henderson, ambaye alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari huko England, aliiongoza Liverpool kubeba ubingwa wao wa kwanza baada ya miaka 30.

Beki wa kulia wa kikosi hicho cha Anfield, Alexander-Arnold, alipiga asisti 13, wakati mshambuliaji wa chama hilo la kocha Jurgen Klopp, Mane alifunga mabao 18 na kuasisti mara saba.

Kwenye orodha hiyo, yumo pia mshindi wa Kiatu cha Dhahabu, Jamie Vardy, ambaye alifunga mabao 23 msimu huu, kiungo mchezeshaji wa Manchester City. Kevin de Bruyne, aliyenyakua tuzo ya Mchezeshaji Bora wa Msimu baada ya kupiga asisti 20. Straika wa Southampton, Danny Ings ametajwa pia kwenye orodha hiyo baada ya kufunga mabao 22, huku kipa wa Burnley, Nick Pope naye amejumuishwa.

Kwenye tuzo hizo, makinda wanne wa Manchester United, wametajwa kwenye kuwania tuzo ya Kinda Bora wa Mwaka, ambapo orodha hiyo ikiwahusu Marcus Rashford, Anthony Martial, Mason Greenwood na kipa Dean Henderson - ambaye msimu huu alikuwa kwa mkopo Sheffield United.

Makinda Rashford, Martial na Greenwood wamehusika kwenye mabao 60 kwenye michuano yote msimu huu.