STRAIKA WA MWANASPOTI : Tukizisapoti vyema, Afrika Mashariki itatamba Afcon

Muktasari:

Tanzania imeingia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980 iliposhiriki michuano iliyofanyika nchini Nigeria huku Burundi wakiwa wanapiga hatua yao ya kwanza.

ZIMEBAKI siku 11 kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) huku baadhi ya timu shiriki zikiwa zinafanya mandalizi kwa ajili ya michuano hiyo mikubwa Afrika.

Ukanda wa Afrika Mashariki tunawakilishwa na mataifa manne, Kenya, Tanzania, Uganda na Burundi.

Ni furaha isiyo kifani kwa ukanda huu kutoa angalau timu nne.

Ni kazi kwetu mashabiki wa soka wa ukanda huu kuzishangilia timu zetu hizo ili angalau ziweze kupiga hatua katika mashindano hayo.

Kenya inarudi katika mashindano hayo baada ya miaka 15, huku majirani zao Uganda wenyewe wakizidi kuwa wazoefu katika michuano hiyo.

Tanzania imeingia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980 iliposhiriki michuano iliyofanyika nchini Nigeria huku Burundi wakiwa wanapiga hatua yao ya kwanza.

Hii inaonyesha wazi ukanda huu soka limeanza kukua na katika kuthibitisha hilo, ni juzi tu tulishuhudia kwa upande wa michuano ya klabu, Simba na Gor Mahia ziliweza kuiwakilisha vyema ukanda huu kwenye michuano ya kimataifa Afrika.

Simba ilifanikiwa kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Gor Mahia wakifika hatua kama hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mafanikio ya Simba na hata yale ya Yanga ya miaka ya nyuma kabla ya kuwapisha watani zao hao kwenye michuano hiyo mikubwa yameisaidia Tanzania sasa kupata nafasio ya kuwakilishwa na timu nne kimataifa, huku mbili zikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na mbili zikishiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho.

Simba na Yanga ndizo zitashiriki Ligi ya Mabingwa, huku Azam FC na KMC zikishiriki kombe la Shirikisho.

Iwapo Gor Mahia ingesonga mbele na kufika nusu Fainali, Kenya ingeingiza timu nyingine mbili kwenye michuano ya kimataifa.

Sasa fikiria, endapo timu zetu za Uganda, Kenya na Tanzania ziwe katika nchi kumi bora barani Afrika. Inamaanisha kila nchi itatoa timu nne kushiriki katika mashindano tofauti ya kimataifa. Hiyo inamaanisha timu 12 zitakuwa zinashiriki.

Hii itawezekana kama tu tutatilia mkazo na kuzipa sapoti timu zetu kwenye michuano hiyo ya kimataifa.

Kwenye michuano ya Afcon, Kenya na Tanzania zipo katika kundi moja pamoja na Algeria, Senegal.

Ni kundi gumu kwa nchi zetu hizi kutokana na pia kutakuwa na debi la Afrika Mashariki kwa Kenya kuumana na Tanzania.

Mbali na debi hilo, timu zetu hizi zitakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha zinazisimamisha Algeria na Senegal zenye mastaa wakubwa huku ukanda wetu ukiwa na nyota kama Mbwana Samatta, Olunga Michael na Victor Wanyama. Itakuwa shughuli pevu.

Mpaka sasa Tanzania imeshaingia nchini Misri na imeweka kambi nchini humo kujiandaa kwa siku zilizosalia ikiwa pia na nia ya kuzoema mazingira ya huko kunakopigwa fainali hizo.

Kenya wao wako Ufaransa huko Uganda wakiwa Qatar.

Ni matumaini yangu zimejiandaa vyema na safari hii lazima tupate timu itakayoingia nusu fainali.

Inawezekana. Ni sisi kuwapa sapoti wachezaji wa timu hizi na kuwaombea kila la kheri wafanye vyema. Mziki ni wao sasa. Wakaucheze.