Tshishimbi afichua mbinu mpya Yanga

Muktasari:

Akizungumzia mchezo huo ambao ulipigwa juzi Jumanne, Tshishimbi alisema kwa upande wao changamoto kubwa ilikuwa uwanja hasa eneo la kuchezea (pitch) alilodai lilikuwa gumu, lakini mengine inabidi awapongeze tu wenyeji wao walivyowapa wakati mgumu dakika zote za mchezo huo.

KABLA ya mchezo wa Polisi Tanzania dhidi ya Yanga kupigwa kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Kocha Mbelgiji Luc Eymael alilalamikia chumba cha kubadilishia nguo walichopewa akidai hakikuwa na hewa ya kutosha, na pia akilizwa na eneo la kuchezea uwanjani hapo.

Madai ya Eymael yaliungwa mkono na nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi lakini yeye akawasifu maafande wa Polisi akidai waliwapatia vilivyo katika kipindi cha pili na hata kupata kwao sare ilikuwa kama bahati kwani, walizidiwa, ila walipambana na kuambulia sare. Tshishimbi pia alionyesha njia ya kupita ili kula sahani na watani wao, Simba. Alisema kwa namna Polisi walivyocheza kipindi cha pili ilikuwa ni bahati kwao kutoka salama kwenye Uwanja wa Ushirika na kushukuru hata kuambulia sare hiyo iliyozidi kuongeza pengo dhidi yao na Simba waliopo kileleni. Timu hizo zilitoka 1-1.

Akizungumzia mchezo huo ambao ulipigwa juzi Jumanne, Tshishimbi alisema kwa upande wao changamoto kubwa ilikuwa uwanja hasa eneo la kuchezea (pitch) alilodai lilikuwa gumu, lakini mengine inabidi awapongeze tu wenyeji wao walivyowapa wakati mgumu dakika zote za mchezo huo.

“Uwanja haukuridhisha kwani ulikuwa mgumu na ulitupa changamoto mchezoni, lakini pia lazima tukiri Polisi walirudi kipindi cha pili kivingine na kucheza kwa kiwango cha juu na juhudi zao wakapata bao la kusawazisha,” alisema Tshishimbi aliyedai kwa sasa akili yao ipo Mkwakwani, Tanga watakapovaana na wenyeji wao Coastal Union Jumamosi hii.

Alisema kwa mechi zilizosalia ikiwamo watakapokutana na Simba, kama wataamua kukomaa nazo lazima kitaeleweka kwa vile soka huwa halitabiriki. “Bado hatujakata tamaa, nafasi ya kupambana ipo na tunaziangalia mengi zilizopo mbele yetu,” alisema Tshishimbi ambaye yeye na chama lake wamekuwa wakikata pumzi kipindi cha pili. Yanga yenye alama 40 kwa sasa baada ya kucheza mechi 21, kama itashinda mechi zao zote itafikisha pointi 91.

Naye straika wa zamani wa Yanga anayekipiga Polisi, Matteo Anthony alidai waliingia kucheza mchezo huo kuhakikisha wanashinda lakini mwisho wa siku walipata pointi moja.

“Yanga ni nzuri na kubwa, lakini tulipambana tukapata matokeo hayo. Kipindi cha pili mwalimu (Hamsini Malale) alitujengea hali ya kujiamini, akatuambia tupambane, alituelekeza pia mambo mengine ya kiufundi sitayazungumza na kweli tukafanikiwa,” alisema Matteo. Mabadiliko waliyofanya kipindi cha pili kwa kumtoa Baraka Majogoro na kumwingiza, Mohammed Mkopi ni kama walizaliwa upya.

Mkopi aliyecheza nafasi ya kiungo, aliongeza nguvu kwenye ushambuliaji, washambuliaji wake kama Matheo, Sixtus Sabilo na Marcelo Kaheza wakang’ara lakini hata kukaba na kuifanya Yanga kushindwa kuongeza bao lingine.