Tshishimbi: Tunawapiga Simba mapema

Muktasari:

Tshishimbi ambaye ni raia wa DR Congo alisema: “Hao wanaosema nimegoma wana msongo wa mawazo, nigome sasa wakati mambo mazuri, kama kugoma ningegoma huko nyuma mambo yalipokuwa hovyo, nilikuwa naumwa na sasa naanza kurejea kwa maelekezo ya madaktari.”

NAHODHA wa Yanga, Pappy Kabamba Tshishimbi amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo huku akisisitiza kwamba wana sababu tatu nzito za kuifunga Simba kwenye nusu fainali ya Kombe la FA Julai 12.

Amekwenda mbali zaidi kwa kuwaambia kwamba hawezi kugomea mechi hiyo kwa sababu yoyote kwa kuwa anaelewa thamani na hadhi yake kama mchezaji wa Yanga hata kama mkataba utakuwa unamalizika.

Tshishimbi ambaye ni raia wa DR Congo alisema: “Hao wanaosema nimegoma wana msongo wa mawazo, nigome sasa wakati mambo mazuri, kama kugoma ningegoma huko nyuma mambo yalipokuwa hovyo, nilikuwa naumwa na sasa naanza kurejea kwa maelekezo ya madaktari.”

Alisema sababu ya kwanza kubwa ya kuifunga Simba ni kwamba, mchezo huo utatoa hatima ya kikosi chao kurejea anga za kimataifa msimu ujao.

“Unajua Simba tayari wao wana uhakika wa kucheza mashindano ya kimataifa, watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa hiyo mchezo huu lengo lao litakuwa moja tu kutokukubali kufungwa mara mbili na sisi (Yanga),” alisema Tshishimbi ambaye Kocha Luc Eymael amesisitiza kuwa atakuwa fiti kufikia siku ya mchezo huo.

“Tunaitaka tiketi hiyo hata kwa kuvunjika miguu, tunahitaji kushiriki kimataifa na nafasi kubwa na ngumu ni hapa, lazima tuvuke kwa ushindi wowote ndio maana nasema hii ni fainali kwetu.”

Kiungo huyo ameitaja sababu ya pili kuwa ni heshima na kwamba, hawatakubali kufungwa na watani wao hao ambao iwapo watawafunga watakuwa wamewaondoa bila taji lolote msimu huu.

“Tunatakiwa kulinda heshima ya mashabiki na viongozi wetu, nafasi pekee ya kupata kombe msimu huu ni hapa, Simba kombe wanalo - tena lenye heshima, wachezaji tunalijua hilo na nimewakumbusha wenzangu na tunaendelea kukumbushana,” alisema.

Sababu ya tatu ambayo imetajwa na Pappy anayehusishwa na kujiunga na Simba msimu ujao ni kwamba, mchezo huo utakuwa njia nzuri kwao kuvuna fedha nyingi kwani katika ushindi wa bao 1-0 walitumia dakika 90 na kuingiza mamilioni ya kutosha.

“Hii ndio mechi ya pesa wote tunajua, mechi iliyopita tulipata fedha nyingi lakini sasa itakuwa zaidi, kwa hiyo kila mchezaji ndani ya timu yetu anatamani kuona siku hiyo anapata nafasi ya kucheza, uongozi umekuwa ukitupa fedha nyingi katika mechi ya namna hii.”

Yanga ilipoifunga Simba kwa bao 1-0 wachezaji walikabidhiwa Sh200 milioni ambapo kila mchezaji aliyecheza mchezo huo alijikamatia kiasi cha Sh10 milioni huku waliokaa benchi wakipata Sh2 milioni achilia mbali zile ndogondogo za mashabiki walizotumiwa kwa nji ya simu.

Kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema mchezo huo utakuwa mgumu na ana matumaini ya kumtumia straika wake, Bernard Morrison licha ya kwamba amehitilafiana na uongozi.

Morrison ameishtaki Yanga katika Shirikisho la Soka nchini (TFF) akidai imeghushi mkataba mpya, ilhali hajaingia nayo mkataba mwingine.

“Nimezungumza naye ameniambia kwamba atapenda kucheza mechi hiyo, akimaliza mambo yake na uongozi akija mazoezini na kuonyesha uwezo nitampa nafasi kwa vile ndio wachezaji nilionao,” alisema Eymael.

Katika mchezo wa Machi 8 dhidi ya Simba, Morrison alifunga bao pekee katika mechi hiyo lililowalaza na viatu watani zao.