Tshishimbi: Huyu Banka ni hatari

Friday August 9 2019

 

By Charity James

NAHODHA wa klabu ya Yanga, Papy Tshishimbi ameeleza kuwa usajili wa vikungo wa maana uliofanywa na mabosi wake msimu huu, umempunguzia majukumu uwanjani tofauti na msimu uliopita alipokuwa akihaha kutafuta matokeo mazuri.

Pamoja na usajili mkubwa uliofanywa na uongozi wa klabu hiyo kwa kuzingatia mahitaji, Tshishimbi ameichambua safu ya kiungo akisema imetendewa haki na kwamba, msimu ujao hatakuwa na majukumu mazito.

Alisema ujio wa Mapinduzi Balama na Abdulaziz Makame umempunguzia kazi na anaamini kuwa safu hiyo ndio itakayoongoza kwa kutengeneza nafasi za mabao kwani, nyota wote wako vizuri.

“Unajua wanazungumziwa sana Makame na Balama, kuna mtu anaitwa Banka amerudi msimu uliopita hakuwa na nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha (kocha Mwinyi) Zahera, lakini sasa anafanya vizuri,” alisema.

“Ni mapema kuzungumzia uwezo wa mmoja mmoja, lakini mwalimu ana kazi ya kufanya, la sivyo abadili mfumo ili kutoa nafasi ya kila mchezaji kupata nafasi ya kucheza hasa safu ya kiungo ambayo ndio msingi wa kutengeneza mabao.

“Tumecheza mechi na Kariobangi timu ilimiliki mpira kwa asilimia kubwa hasa safu ya kiungo wachezaji walionekana kufanya majukumu yao kwa wakati japo kulikuwa na kasoro ndogo ambayo mwalimu ameshaifanyia kazi na anaendelea kabla ya kushuka dimbani Jumamosi.”

Advertisement

Tshishimbi aliongeza kuwa baada ya kupunguziwa majukumu, ana mpango wa kurudisha fadhila kwa Wanayanga kwa kucheza soka ambalo anaamini litakuwa chachu kwake na kwa klabu, huku akiongeza kuwa yupo fiti kwa mapambano.

Alisema timu yao iko vizuri na imejiandaa kwa ushindani.

Akizungumzia mchezo wao na Township Rollers, alisema wanawaheshimu wapinzani wao na wataingia uwanjani kwa tahadhari, lakini lengo ni kumaliza mchezo nyumbani.

“Tumepata nafasi nzuri ya kuanzia nyumbani, ni muda wa sisi kupambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri bila ya kuruhusu nyavu zetu kutikiswa, hilo linawezekana kutokana na ubora wa safu ya ulinzi ikiwa ni sambamba na kipa,” alisema.

“Uwanja wa nyumbani ndio utakaoamua matokeo, tunaomba sapoti kama ilivyokuwa katika mchezo wa kirafiki uliopita ili tuweze kucheza kwa kujituma zaidi na kurudisha furaha ya Watanzania, wengi wanapenda mpira.”

Advertisement