Tshabalala akamua Sh168 milioni

Wednesday June 26 2019

 

By Thobias Sebastian

UONGOZI wa Simba unaendelea kufanya usajili wa kimyakimya kwa kuwasainisha mikataba mipya nyota wao waliomaliza muda pamoja na kuingiza wachezaji wapya.

Mpaka sasa Simba imesajili nyota wapya watano ambapo wawili ni wa kigeni, Shiboub Eldin Sharaf kutoka Sudan na Wilker Henrique de Silva raia wa Brazil huku wazawa wakiwa watatu Kennedy Juma, Beno Kakolanya na Miraji Athuman.

Wachezaji hao walisajiliwa wakati tayari imewaongezea mikataba mipya Aishi Manula, John Bocco, Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Meddie Kagere.

Jana Jumatatu, uongozi umetangaza kumwongeza mkataba mpya wa miaka miwili beki wao Mohamed Hussen ‘Tshabalala’, ambaye pia ni nahodha msaidizi wa kikosi hicho.

Simba wanafanya usajili wao kimyakimya huku ikielezwa kwamba ni kwa mujibu wa ripoti ya kocha wao, Patrick Aussems aliyeiwezesha timu hiyo kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara pamoja na kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Habari za ndani kutoka Simba zinasema Tshabalala ambaye mkataba wa awali uliokuwa wa miaka miwili ulikuwa na thamani ya Sh40 milioni, sasa wamepanda dau hadi Sh55 milioni huku mshahara kwa mwezi ukiwa ni Sh4.5 milioni.

Advertisement

Kuongezwa kwa mkataba huo kunaaminisha kwamba, Tshabalala kwa muda wa miaka miwili ndani ya klabu hiyo mbali ya posho zingine, ataikamua Simba jumla ya Sh163 milioni.

Iko hivi, mkataba wa Tshabalala una thamani ya Sh55 milioni, mshahara kwa mwezi ni Sh 4.5 milioni. Kwa maana hiyo pesa ya mshahara ukizidisha mara miezi 24 (miaka miwili) atakuwa amekusanya Sh108 milioni ambazo zikijumlishwa pamoja.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema usajili unaendelea na msimu huu watafanya usajili makini ambao utakuwa tofauti na misimu mingine yote kutokana na umakini wanaotumia kupata wachezaji wapya na wanaomaliza mikataba.

“Masuala ya usajili bado yanaendelea, tulipumzika kidogo lakini wiki hii tunaendelea kuwatangaza wachezaji wapya na wale tunaowaongeza mikataba,” alisema Magori.

Kwa upande wa meneja wa mchezaji huyo, Herry Mzozo alisema, “tunashukuru Simba wanaendelea kumwamini Tshabalala juu ya kiwango chake, ameongeza mkataba huo ambao naamini ni deni kwake kujituma zaidi na kufikia malengo yake na timu.

“Kuna maboresho ambayo tuliomba na walisikia na kuyafanyia kazi na sasa kila kitu kiko vizuri.”

Advertisement