Top Four tamu kuliko ubingwa wa EPL msimu huu

Muktasari:

Man City wanaongoza kisha wanafuatia Chelsea, Liverpool, Spurs, Arsenal kisha wanakuja Bournemouth halafu ndio Man United. Bournemoth na Man United wanalingana pointi, wote 20 na wanatofautiana kwenye mabao ya kufunga na kufungwa tu. Hivyo kwenye wiki ya 12,

WIKI ya 11 tayari kwenye Ligi Kuu England. Pointi 26 zinawatenganisha anayeongoza Man City na anayeshika mkia, Huddersfield. Man City wamekusanya pointi 29 kwenye mechi hizo na Huddersfield wana pointi tatu tu. Hawa, Huddersfield kushuka daraja kunawahusu. Jana Jumamosi walikuwa na mechi yao na sijui kilichowakuta huko kwa Fulham. Hebu achana nao hao.
Wasiwasi wangu upo pale kwenye Top Four. Msimamo wa ligi sasa unaanza kujitengeneza. Kila mtu taratibu anaanza kurejea kwenye nafasi yake. Kwenye ile Big Six kwa maana ya Man City, Chelsea, Liverpool, Tottenham na Man United ni Bournemouth tu ndiye aliyeingia kati. Man City wanaongoza kisha wanafuatia Chelsea, Liverpool, Spurs, Arsenal kisha wanakuja Bournemouth halafu ndio Man United. Bournemoth na Man United wanalingana pointi, wote 20 na wanatofautiana kwenye mabao ya kufunga na kufungwa tu. Hivyo kwenye wiki ya 12, mambo yanaweza kuwa tofauti na ile Big Six ikawa yenyewe imejipanga kwenye timu sita za juu kwenye msimamo. Mechi ijayo Man United watacheza na Man City, kisha watacheza na Crystal Palace. Bournemouth wao watacheza na Newcastle ugenini, kisha watacheza na Arsenal. Hapo unaweza kuona hadi kufikia wiki ya 13 kwenye Ligi Kuu England, Big Six watakuwa kwenye nafasi sita za juu. Hapo ndipo utakapokuja utamu halisi. Vita itakuwa kwenye timu hizo sita kuwania nafasi nne. Hakuna anayependa kucheza kwenye Europa League. Wote wanataka kucheza kwenye michuano yenye hadhi kubwa, Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hapo ndipo inapokuja ile methali ya kwamba mwenye kisu kikali ndiye anayekula nyama. Man United wanaonekana kuikaribia kasi yao, huku kocha Jose Mourinho akionekana kuanza kupata huduma nzuri kutoka kwa Luke Shaw na Anthony Martial. Lakini, huko kwenye kikosi cha Arsenal, kocha Unai Emery, naye anaonekana kuanza kuipata huduma nzuri ya Granit Xhaka na Alexandre Lacazette. Huko kwa Maurizio Sarri, Alvaro Morata amerudi kwenye makali yake ya kufunga mabao huku Mauricio Pochettino na Jurgen Klopp wakifanya vyema na vikosi vyao vya Spurs na Liverpool. Pep Guardiola na Man City yake ndiye anaonekana kuwa na uhakika wa kwamba hawezi kukosekana kwenye ile Top Four. Shughuli kwa hawa wababe wengine, nani atapenya na nani atashindwa? Tofauti ya pointi baina ya vigogo hao sita ni ni tisa, lakini kuna tofauti ya pointi nne baina ya timu inayoshika nafasi ya nne na ile ya saba, ambao ni Man United. Lakini, Man City yenyewe imezizidi timu zinazoshika namba mbili na tatu, Chelsea na Liverpool pointi mbili tu. Hiyo ina maana kama Man City watashindwa kuifunga Man United kwenye mechi ijayo, kisha Liverpool au Chelsea zikashinda mechi zao, msimamo utakuwa tofauti kabisa. Huu ndio ukweli unaoifanya Ligi Kuu England hasa kwa wale vigogo wa Top Six kila mmoja acheze kama fainali ili asipoteze. Kupoteza kwa sasa hakuruhusiwi na ndio maana Man United walipambana kugeuza matokeo ya kufungwa na Bournemouth na kushinda ili kuendelea kuwamo kwenye vita hiyo. Ndio maana Arsenal waligoma kupoteza mbele ya Liverpool. Hupaswi kupoteza, ukipoteza unapotezwa. Ni kipindi kizuri cha kuona ufundi wa makocha na hicho ndicho kitakacholeta tofauti. Ni wakati wa Mourinho kuonyesha kwanini yeye ni Special One, lakini makocha wengne pia wakiwa na kazi ya kuthibitisha kwamba hawajakosea kuwamo kwenye vikosi hivyo vinavyohesabika kuwa ni timu kubwa zaidi kwenye ligi hiyo. Nani atabaki? Hivi ndivyo Top Four inavyoleta raha kuliko mbio za ubingwa wenyewe kwenye ligi hiyo.