Top 5 wamecheza mechi nyingi Ulaya

MADRID, HISPANIA. LIGI ya Mabingwa Ulaya imeanza wiki hii na juzi Jumanne na jana Jumatano kipute hicho kilipigwa huko Ulaya huku kile cha Europa League kikianza leo Alhamisi.

Ligi ya Mabingwa ndio maarufu zaidi duniani na ina historia ndefu tangu kuasisiwa kwake mwaka 1955 hadi sasa ikiwa ni miaka 65 kabla ya kubadilishwa jina kutoka Klabu Bingwa Ulaya na mwaka 1992 kuitwa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Europa Leagu yenyewe iliasisiwa mwaka 1971.

Timu nyingi Ulaya zimeshashiriki michuano hiyo tangu kuasisiwa kwake huku zikipishana kwa maana nyingine hukaa miaka mingi bila kufuzu na kuachia miamba mingine.

Hata hivyo, zipo timu ambazo kwenye michuano hiyo, zimeshiriki mara nyingi zaidi ikiwa ni zaidi ya asilimia 70 zikicheza michuano hiyo.

5. Benfica (Mechi 433)

Hii ni kwa michuano yote ya Ulaya kwa maana ya Ligi ya Mabingwa na Europa League. Imefanikiwa kushinda michezo 200, sare 100 na ikapoteza mechi 133, huku mabao ya kufunga yakiwa ni 691 na kufungwa 489.

Benfika imebeba taji la Ulaya mara mbili, huku Europa League haijaambulia chochote licha ya kucheza fainali tatu.

4. Juventus (mechi 437)

Yenyewe kwenye michuano hiyo kwa jumla shinda mechi 239, sare 98 na kufungwa mechi 100, pia imefunga mabao 749 na kufungwa mabao 398.

Ina mataji mawili ya Ulaya na matatu ya Europa League. Imeingia fainali mara mbili miaka ya karibuni, mwaka 2015 na 2017, hata hivyo iliondoka kapa kwenye Ligi ya Mabingwa.

3.Bayern Munich MECHI 464

Kati ya mechi hizo imeshinda 263, sare 101 na imepoteza 100, huku ikiwa imefunga mabao 936 na kuruhusu 478 kwenye michuano yote kwa jumla.

Inamiliki mataji sita ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja la Europa League na ndiye bingwa mtetezi wa michuano hiyo mikubwa baada ya kuifunga PSG msimu uliopita.

2. Barcelona (mechi 495)

Miamba hii imeshinda mechi 283 kati ya hizo, sare 283 na kupoteza 100. Pia imefunga mabao 975 na kufungwa 484.

Ina mataji matano ya Uefa na haijawahi kutwaa taji la Europa League. Imecheza fainali tatu za Uefa na haikufanikiwa kushinda taji, mwaka 1961, 1986 na 1994.

1. Real Madrid (mechi 547)

Ndio kinara wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa na mataji 13, huku Europa League ikibeba mawili tu. Imeshinda 318, sare 96 na kufungwa 133. Imefunga mabao 1163 na kufungwa 596 kwenye michuano yote miwili.