Tofauti ya penalti ya Samatta na salamba

Muktasari:

  • Samatta amekuwa na rekodi mbaya ya kukosa penalti katika timu ya taifa, lakini bado ni kipenzi cha mashabiki

BAADA ya kukosa penalti kwenye mchezo wa Tamasha la Simba Day dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana, Adam Salamba alidai kuwa alitamani kuomba atolewe asiendelee kucheza mchezo huo.

Salamba alifichua kuwa kitendo cha kukosa penati hiyo kilimfanya atoke mchezoni na alijikuta akiwa mwenye presha kubwa kutokana na zomeazomea ya umati wa mashabiki wa Simba waliojawa na hasira baada ya nyota huyo kijana aliyenunuliwa kutoka Lipuli kukosa penati.

Ilikuwa ni jambo gumu kwa Salamba kuhimili presha ya mashabiki wa Simba na hadi anafikia hatua ya kusema alikuwa anatamani atolewe ili asiwe kuendelea kucheza, maana yake asingeweza kufanya chochote cha kuisaidia timu yake kwa muda ambao ulibakia.

Huenda jinamizi la tukio la kukosa penati likaendelea kumsumbua zaidi Salamba na anahitaji kupata msaada wa kisaikolojia ili aone kwamba suala la kukosa penati ni jambo la kawaida kwa wanasoka na halipunguzi ubora wake ndani ya uwanja.

Kwa bahati mbaya timu zetu hazina wataalamu wa kisaikolojia wa kuweza kuwarudisha wachezaji hasa wenye umri mdogo kama Salamba katika hali ya kawaida pindi wanapokutwa na matukio kama lile la kukosa penati. Inahitaji moyo mgumu kuvumilia presha ya mashabiki hasa wa soka la bongo.

Miezi miwili baadaye, ndani ya uwanja uleule ambao presha ya mashabiki ilimshinda Salamba, nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta alionyesha utofauti baina yake na akina Salamba.

Huku ikihitaji ushindi muhimu dhidi ya Cape Verde nyumbani, Samatta alikosa mkwaju wa penalti ya mapema ambayo ingeweza kuipatia Taifa Stars bao la kuongoza baada ya mpira aliopiga, kugonga mwamba wa juu na kurudi uwanjani kabla ya kuokolewa.

Tofauti na Salamba, Samatta hakuonyesha hata chembe ya presha baada ya kukosa penalti hiyo muhimu na zaidi ni kama ilimchochea kufanya vizuri zaidi kwenye mchezo huo na kutoa mchango mkubwa kwa Stars iliyopata ushindi wa mabao 2-0.

Alihusika katika mabao yote mawili, akitoa pasi ya mwisho kwa Saimon Msuva aliyefunga bao la kwanza lakini pia alifunga bao la pili huku akiwaweka kwenye wakati mgumu mabeki wa Cape Verde kutokana na kasi na uwezo wake wa kumiliki mpira kila Stars ilipokuwa inaelekea langoni mwa timu pinzani.

Wakati Salamba alidai kuwa aliathirika kisaikolojia na angekuwa radhi kutolewa baada ya kukosa penalti dhidi ya Asante Kotoko kwenye mechi ya kirafiki, Samatta ambaye alikosa penati kwenye mechi muhimu iliyobeba matumaini ya mamilioni ya Watanzania, aliwajibu waandishi wa habari kuwa tukio la kukosa penati kwake lilikuwa la kawaida na halikumtoa mchezoni kwani yeye sio mchezaji wa kwanza kufanya hivyo.

Majibu ya Samatta yanathibitisha wazi kwamba daraja na maisha wanayoishi wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi na wale wazawa waliopo kwenye ligi yetu ya ni mbingu na ardhi na kuna tofauti kubwa baina yao.

Kitendo cha Samatta kuibeba timu mgongoni kwa kufunga bao na kutoa pasi ya mwisho huku akiwa ametoka kukosa penati, kinatuthibitishia kuwa mahali alikopita pamemjenga kisaikolojia kiasi ambacho anaweza kufanya kazi katika mazingira yoyote yale na kukabiliana na nyakati ngumu hasa presha za mashabiki.

Ndani ya TP Mazembe alikocheza zamani na Genk ambayo anachezea kwa sasa, Samatta amekutana na wataalamu ambao wamemtengeneza na kumuandaa namna ya kudhibiti hofu na presha pindi awapo uwanjani na ndio maana alichukulia ni jambo la kawaida kwake kukosa penati.

Tunataka kuona tunakuwa na nyota wenye uwezo wa kukabiliana na mazingira ya aina yoyote ile ikiwemo presha za mashabiki ili wawe na msaada kwenye timu yetu ya Taifa kama alivyofanya Samatta juzi.

Kama Salamba alishindwa kuhimili presha za mashabiki wa Simba ndani ya dakika chache alizocheza kwenye Tamasha la Simba Day, ataweza vipi kuhimili presha ya mashabiki wa Uganda, Misri, Nigeria, Morocco au Tunisia pindi akiwa na jezi ya Taifa Stars na wakati huo inatafuta matokeo ifuzu?