Tofauti kati ya Leeds United na Tukuyu Stars hii hapa

Tuesday July 21 2020

 

By EDO KUMWEMBE

LEEDS United wamerudi Ligi Kuu. Kuna wakati tuliwapenda sana lakini wakaja kushuka miaka 15 iliyopita. Walikuwa na mastaa wazuri ambao walitusisimua.

Walikuwepo akina Harry Kewell, Mark Viduka, Alan Smith, Ian Harte, Dan Mills, Rio Ferdinand na Wengineo. Lakini kwa Waafrika huwa hatumsahau, Lucas Radebe ambaye alikuwa Mwafrika wa kwanza kuwa nahodha katika timu ya Ligi kuu ya England.

Waliposhuka tulisikitika. Tulisikitika zaidi waliposhuka tena kwenda Ligue 1 ambayo kwa huku kwetu kwa sasa ni kama daraja la pili. Tulikuwa tuna matumaini kwamba siku moja tungewaona tena. Wenzetu huwa wanajipanga.

Huku kwetu kuna timu zilishuka zamani hatujaziona tena. Tukuyu Stars, Pamba, CDA na wengineo. Tunasikia zipo madaraja ya chini zinapambana lakini mambo yamekuwa magumu kwao. Nilitazamia mambo yawe magumu. Kwanini nilitazamia? Mashabiki wa Leeds timu yao iliposhuka wakaendelea kubaki nayo. Kule kwa wenzetu mashabiki huwa ni walewale tu. Hawana timu mbili. Ukiwa Leeds wewe ni Leeds. Kila timu ina mashabiki lukuki wa jimbo lake.

Huku kwetu unaweza kuwa Tukuyu Stars lakini ni shabiki mkubwa wa Simba au Yanga. Hii ni kuanzia kwa mashabiki hadi viongozi. Timu inaposhuka kiongozi anawapeleka wachezaji wake Simba au Yanga. Anaendelea kushabikia timu yake ya Dar es salaam ambayo ipo kilomita 800 kutoka yeye anapoishi.

Mashabiki pia wana chaguo jingine ambalo linaweza kuwa kubwa kuliko Tukuyu Stars. Huyu wa Simba ataenda kuishabikia Simba kwa nguvu zaidi, na yule wa Yanga ataenda kuishabikia Yanga kwa nguvu zaidi. Hakuna kikubwa kinachopungua kwao. Zaidi ni kwamba wanazitia nguvu ya kiuchumi zaidi timu za Dar es salaam. Kwa timu za kiasili kama CDA, Pamba, Tukuyu Stars inakuwa ngumu kurudi. Zikienda chini zinakutana na tatizo kubwa la kiuchumi kwa sababu mashabiki wanazitelekeza. Kwa Leeds United hali ni tofauti. Wanashuka na mashabiki wao ambao wanaendelea kulipa viingilio.

Advertisement

Wanashuka na mashabiki wao hali ambayo inasababisha wadhamini waendelee kuwepo na kuona thamani ya klabu. Tanzania ukishuka umeshuka. Jina linashuka bila ya mashabiki. Kuna mashabiki wale wale wa Tukuyu wanasafiri kutoka Tukuyu hadi Mbeya mjini au Dar es salaam kwa ajili ya kwenda kuitazama Simba au Yanga ikicheza.

Tofauti kwa kule ni kwamba hakuna shabiki wa Leeds anayejishughulisha kwenda kuitazama Manchester United au Liverpool ikicheza. Timu ikishuka atarudi uwanjani wiki ijayo kuitazama ikicheza dhidi ya Blackpool.

Kufikia hapo inakuwa rahisi kwa Leeds United kurudi Ligi Kuu kuliko Tukuyu. Wanaweza kuchelewa lakini wana uwezo mkubwa wa kurudi. Timu nyingi za Tanzania zinakosa nguvu za kiuchumi kwa sababu sio timu za mashabiki. Timu zenye mashabiki wa kweli ni Simba na Yanga tu.

Kitu kinachonishangaza ambacho ni ukweli mwingine upo Tanzania tu ni kwamba ndani ya jiji la Tukuyu inaweza kutengenezwa timu nyingine ya ajabu ajabu tu na ikafika Ligi Kuu ndani ya miaka mitatu. Timu ambayo itapandishwa kwa nguvu za siasa. Inaweza kuwa siasa hii hii tunayoifahamu au siasa za soka.

Jaribu kuzitazama timu kadhaa ambazo zimepanda kisiasa katika miaka ya karibuni. Hazikuwepo katika ulimwengu wa soka hadi kufikia mwaka 2010 lakini zimefika Ligi Kuu. Gwambina, Mbeya City, Dodoma City, Namungo ni baadhi ya timu hizi.

Wengine ni wale ambao walikuwepo tangu zamani, japo sio sana, lakini wakatiwa nguvu kutokana na sababu za kisiasa, na Wanasiasa walipopoteza nguvu basi na timu ikapotea. Mfano ni Singida United. Haikuwa timu ya kudumu Ligi Kuu. Usishangae kuona kuna timu kutoka Tukuyu ikapigiwa debe na Wanasiasa na matajiri wa muda kisha ikapanda Ligi Kuu huku Tukuyu Stars ikiwekwa kando. Malengo ya kisiasa yakitimia na kupita basi timu hiyo inashuka na tunaisahau.

Kitu kama hiki hakiwezi kutokea katika jiji la Leeds. Leeds United inabakia kuwa Leeds United. Inawezekana kuna timu nyingi katika jiji la Leeds lakini nazo zilianzishwa miaka mingi iliyopita na zimeendelea kuwa katika hadhi zilezile tu.

Hata pale jiji la Manchester ingekuwa kitu kigumu kwa timu nyingine kuanzishwa na kuwa juu ya Manchester United na Manchester City. Zilishakuwepo miaka mingi iliyopita. Walichofanya matajiri wa Kiarabu ni kuinunua Manchester City na kuitia nguvu lakini ilishakuwepo awali na ilishawahi kutwaa hata ubingwa wa Ligi Kuu ya England.

Mtu akifanya hivyo kwa Tukuyu Stars tunaweza kumuelewa lakini akianzisha timu yake ghafla ghafla na ikafika Ligi Kuu ndani ya miaka mitatu ujue kuna ajenda ya Kisiasa nyuma yake. Moyo wa timu unakosekana na ni rahisi kwa timu hiyo kurudi ilikotoka.

Wakati huu tukishabikia Leeds United kurudi Ligi Kuu tujikumbushe tu namna ambavyo tumezipoteza klabu nyingi za Ligi Kuu ya Tanzania ambazo zilitamba kwa miaka mingi na zimeshindwa kurudi Ligi Kuu. Na hata zinaporudi hazipati uimara tena kama ule wa mwanzo. Sababu ya kwanza kubwa ni mapenzi yetu yaliyopitiliza kwa Simba na Yanga. Safari ya pili iliyoanza kujitokeza ni hii ya kuunda timu za ghafla ghafla kwa lengo la kuzihepuka timu za zamani. Kwa mfano, nguvu iliyopelekwa Gwambina kama ingepelekwa Pamba ya Mwanza nadhani ingekuwa imerudi Ligi Kuu. Hata hivyo hauwezi kujua aliyeanzisha Gwambina alianzisha kwa sababu zipi na hatuwezi kujua kwanini aliikwepa Pamba. Labda timu kama hizi Pamba na Tukuyu zina watu wanajifanya ni wenyewe zaidi na hawataki mfumo mpya na mawazo mapya. Labda!

Advertisement