Timu zinazomiliki vikosi vya pesa nyingi Ulaya kwa sasa

Muktasari:

Lakini unafahamu ni klabu gani yenye kikosi ghali zaidi kwenye soka la Ulaya kwa sasa kwenye ligi za Ulaya. Hizi hapa timu ambazo vikosi vyao ni vya pesa ndefu kwenye ligi za Ulaya msimu huu wa 2019/20.

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHESTER City imetumia pesa nyingi kufikia ilipofikia kwa sasa na kuhesabika kuwa moja kati ya timu tishio kwenye soka la Ulaya.

Ndani ya miaka 10, kuanzia mwaka 2009 hadi 2019, wababe hao wa Etihad ndio waliotumia pesa nyingi kwenye kufanya usajili wa kuboresha kikosi chake, ikitumia Pauni 1.5 milioni kujijenga.

Lakini unafahamu ni klabu gani yenye kikosi ghali zaidi kwenye soka la Ulaya kwa sasa kwenye ligi za Ulaya. Hizi hapa timu ambazo vikosi vyao ni vya pesa ndefu kwenye ligi za Ulaya msimu huu wa 2019/20.

Tottenham – Pauni 317 milioni

Kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya, Kocha Mauricio Pochettino alifanya usajili wa pesa nyingi wakati alipomsajili kiungo Tanguy Ndombele kwa ada inayotajwa kuwa Pauni 62 milioni. Usajili huo umeifanya Tottenham Hotspur kuwa na timu yenye kikosi chenye thamani ya Pauni 317 milioni na kuwa moja ya timu zenye vikosi vya pesa nyingi kwenye soka la Ulaya kwa kipindi hiki.

Bayern Munich – Pauni 321 milioni

Hivi karibuni mabingwa wa Bundesliga, Bayern Munich walifanya usajili wa staa wa Kibrazili, Philippe Coutinho kwa mkopo kutoka Barcelona, lakini kukiwa na makubaliano ya kumbeba jumla mwakani kwa Pauni 109 milioni. Wababe hao wa Allianz Areno ni moja ya timu zinazomiliki vikosi vyenye thamani kubwa huko Ulaya, kikosi chao cha sasa kikiwa cha Pauni 321 milioni. Kocha Nico Kovac ana kila sababu ya kutamba.

Everton – Pauni 323 milioni

Utashangaa, lakini ndio hivyo, Everton ipo kwenye nafasi 10 za juu kwenye timu yenye kikosi chenye thamani kubwa kwenye soka la Ulaya kwa sasa. Wakali hao wa Ligi Kuu England, kikosi chao cha msimu huu kina thamani ya Pauni 323 milioni na kuzizidi timu vigogo huko Ulaya ikiwamo Bayern Munich na Atletico Madrid kutokana na kuwa na kikosi cha pesa ndefu.

Arsenal– Pauni 357 milioni

Kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, Arsenal imefanya usajili wa nyota kadhaa, akiwamo winga Nicolas Pepe, iliyemnasa kwa mkwanja wa Pauni 72 milioni kutoka Lille ya Ufaransa. Usajili huo na mwingine kama wa David Luiz, umeifanya timu hiyo yenye maskani yake kwenye Uwanja wa Emirates kumiliki kikosi chenye thamani ya Pauni 357 milioni kwenye Ligi Kuu England kwa sasa. Kikosi cha Arsenal ni noma.

Juventus – Pauni 396 milioni

Mabingwa wa soka wa Italia, Juventus wao siku zote kitu ambacho wamekuwa wakikifanya ni kuhakikisha wanaboresha kikosi chao kila kinapofika kipindi cha usajili. Mwaka jana walimnasa staa Cristiano Ronaldo, wakati mwaka huu wamembeba beki wa kati Matthijs de Light wote kwa pesa ndefu na kufanya kuwa na kikosi chenye thamani ya Pauni 396 milioni na kuwa ghali zaidi huko kwenye Serie A.

Liverpool – Pauni 408 milioni

Wababe wa Anfield walihitimisha msimu wao uliopita kwa kubeba taji la ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushindwa kidogo kwenye Ligi Kuu England. Mwaka huu, Liverpool haijafanya usajili mkubwa sana, lakini bado inamiliki kikosi ghali kabisa katika Ligi Kuu England, kutokana na chama hilo linalonolewa na Mjerumani Jurgen Klopp kuwa na kikosi chenye thamani ya Pauni 408 milioni.

Real Madrid – Pauni 440 milioni

Miamba ya soka ya La Liga, Real Madrid mwaka huu imefanya usajili wa mastaa kadhaa ikiwamo supastaa wa Kibelgiji, Eden Hazard iliyemsajili kutoka Chelsea. Kwenye kikosi chake kuna Gareth Bale, ambaye pia ilimsajili kwa pesa ndefu na hivyo kuwafanya Los Blancos kwa sasa kumiliki kikosi chenye thamani ya Pauni 440 milioni kutokana na wachezaji iliwasajili siku za karibuni na waliopo Bernabebu kwa sasa.

Chelsea – Pauni 524 milioni

Chelsea haikufanya usajili wa mchezaji yeyote kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya kutokana na kuwa na adhabu ya kufungiwa kusajili. Hata hivyo, Kocha Frank Lampard bado haishi kinyonge kwa sababu anamiliki timu yenye kikosi chenye thamani kubwa huko Ulaya, kutokana na wakali hao wa Stamford Bridge kwa sasa kuwa na kikosi chenye thamani ya Pauni 524 milioni.

Barcelona – Pauni 642 milioni

Mabingwa wa La Liga, Barcelona wamefanya usajili mkubwa kwenye dirisha hili, wakimnyakua staa Antoine Griezmann kutoka kwa wapinzani wao kwenye ligi hiyo, Atletico Madrid. Usajili wa Griezmann na wakali wengine kama Frankie De Jong, umewafanya Barcelona kumiliki kikosi chenye thamani ya Pauni 642 milioni huko Nou Camp. Barca ipo kwenye mipango ya kumrudisha Neymar kikosini kwao.

Man United– Pauni 661 milioni

Manchester United kwenye dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi huko Ulaya imevunja rekodi kwa kumsajili beki kwa pesa nyingi baada ya kumnasa Harry Maguire kwa Pauni 80 milioni. Jambo hilo na usajili wa mkali kama Aaron Wan-Bissaka na Paul Pogba umekifanya kikosi cha Man United kuwa na thamani ya Pauni 661 milioni huko Old Trafford na kumfanya Kocha Ole Gunnar Solskjaer kumiliki timu ya mkwanja mrefu.

Paris Saint-Germain– Pauni 712 milioni

Kwenye kikosi cha PSG, kuna supastaa Neymar, ambaye saini yake peke yake ilinaswa kwa Pauni 198 milioni. Ndiye mchezaji ghali kuliko wote duniani kwa sasa. Usajili wa mshambuliaji huyo na mkali mwingine kama Kylian Mbappe umewafanya mabingwa hao wa Ligue 1 kuwa na timu yenye kikosi chenye thamani kubwa kwa sasa, Pauni 712 milioni na hivyo kumfanya Kocha Thomas Tuchel kucheza kwa kujiamini.

Man City – Pauni 777 milioni

Pep Guardiola ana kila sababu ya kufurahia maisha yake huko Manchester City kwa sasa. Ana kila sababu ya kuendelea kuwatesa kwenye Ligi Kuu England, kwa sababu ndiye kocha anayemiliki timu yenye kikosi chenye thamani kubwa zaidi Ulaya nzima. Kikosi cha sasa cha Man City kinaripotiwa kuwa na thamani ya Pauni 777 milioni. Kwenye kikosi cha Man City kuna mastaa wengi wa pesa nyingi.

Timu nyingine

Kwenye soka la Ulaya, katika orodha ya timu 20 zenye vikosi vya thamani kubwa kwa sasa, ipo AC Milan inayomiliki kikosi cha Pauni 270 milioni, wakati Atletico Madrid huko kwenye La Liga ina kikosi cha Pauni 264 milioni.

AC Monaco kwenye huko Ufaransa, kikosi chake kina thamani ya Pauni 253 milioni, wakati wakali wa Bundesliga, Borussia Dortmund inamiliki kikosi chenye thamani ya Pauni 237 milioni.

AS Roma huko kwenye Serie A, kikosi chao kina thamani ya Pauni 232 milioni, huku kile cha Southampton kwenye Ligi Kuu England kina thamani ya Pauni 203 milioni, Crystal Palace kina thamani ya Pauni 199 milioni, wakati Inter Milan inakamilisha orodha hiyo ikiwa na kikosi chenye thamani ya Pauni 192 milioni baada ya usajili wa straika wa Kibelgiji, Romelu Lukaku kutoka Manchester United.