Tenga ataja changamoto tatu za michezo

Dar es Salaam. Wakati mafanikio ya michezo kwa miaka mitano yakianikwa, Baraza la Taifa la Michezo la Taifa (BMT), limetaja changamoto tatu zinazoikabili sekta hiyo nchini.

Akizungumza katika mkutano wa kueleza mafanikio ya michezo kwa miaka mitano iliyopita, Mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga alizitaja changamoto hizo kuwa ni kukosekana kwa miundombinu, ukata na utawala usioridhisha

“Pamoja na mafanikio tuliyopata kuna changamoto tatu ambazo zikifanyiwa kazi tutapiga hatua. Kwanza ni miundombinu. Tunahitajika kuiboresha. Kwa sasa bado tuko nyuma na kama tunataka kupiga hatua tunatakiwa kuiboresha,” alisema Tenga.

“Nchi yetu haina uwanja wa kisasa wa ndani wa michezo (indoor), lakini pia hatuna bwawa la kuogelea lenye hadhi ya kimataifa. La pili ni uwepo wa vyanzo endelevu vya fedha. Kuna vyanzo viwili vya fedha.”

Tenga alifafanua kuwa: “Ukiachana na serikali kuna kampuni na watu binafsi. Tunaomba serikali itoe motisha au ruzuku kwa hawa watu binafsi, hii itasaidia kuwashawishi hao watu kuweka fedha huku kwenye michezo. Lakini pia katika hili tunaomba sehemu ya fedha inayopatikana katika ‘betting’ (ubashiri) wa matokeo ya michezo iwekwe huku katika michezo.”

Tenga pia alisema jambo lingine ni suala la utawala bora ambalo bado limekosekana katika vyama vingi vya michezo.

“Sisi huku katika michezo lazima tuwe safi hasa katika suala zima la matumizi ya fedha. Lazima wale wanaotupa fedha waone na kufahamu zimetumikaje,” alisema Tenga.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema changamoto hizo watazifanyia kazi.

“Suala la miundombinu kwa mfano, tayari Katibu Mkuu wa Wizara ameshafanya mazungumzo na Kampuni moja kubwa tu kwa ajili ya kujenga Uwanja wa kisasa wa ndani pale katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Na kuhusu hilo suala la mapato ya ‘betting’, lipo pazuri. Tumeshazungumza na Waziri wa Fedha. Sheria na Kanuni tumeshaziandaa na kilichobakia kama ni kwenye mpira wa miguu ni kusukuma mpira wavuni,” alisema Mwakyembe.

Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msita alitaja mafanikio yaliyofikiwa michezoni ndani ya miaka mitano.

“Kuna mengi yamefikiwa miongoni mwa hayo ni timu mbalimbali za Taifa kufuzu katika mashindano makubwa, timu ya soka la ufukweni kushiriki fainali za Afrika na kubwa zaidi ni timu yetu ya taifa ya walemavu kufuzu Fainali za Dunia zitakazofanyika London, England mwaka 2022.

Kiukweli yapo mengi sana ambayo yote yametokana na taarifa tulizopewa na vyama na mashirikisho ya michezo,” alisema Msita.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi alisema kilichofanyika michezoni kwa muda wa miaka mitano ni kitu kikubwa.

“Niwape hali ya kujiamini kwa mafanikio haya makubwa yaliyofikiwa michezoni, tuko tayari kuendelea kusaidiana na nyinyi,” alisema Dk Abbasi.