Tegete: Aweka wazi kitakachoiua Simba Jumapili

Friday July 10 2020

 

By Masoud Masasi, Mwanza

KOCHA wa zamani Toto Africans, John Tegete amesema kama Simba watawadharau na kuingia kwa hasira katika pambano lao la keshokutwa Jumapili basi mchezo huo utakuwa rahisi kwa Yanga.
Timu hizo zinakutana katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam utakaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mshindi wa mchezo huo atafuzu fainali ambapo atacheza na mbabe wa mpambano lingine la nusu linalotarajiwa kuchezwa kesho Jumamosi kati ya Sahare All Stars na Namungo FC mechi itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Akizungumza na Mwanaspoti Online, Tegete amesema Yanga wanahitaji utulivu katika pambano hilo kwani Simba wataingia na presha kubwa kitu ambacho kwao kitakuwa rahisi kuwafunga.
“Unajua huu mchezo Yanga wanahitaji umakini sana, Simba watakuja na presha ya kile kichapo walichowapa kwenye mechi ya Ligi Kuu kitu ambacho kitakuwa rahisi kwao kuwafunga.
“Kikubwa Yanga wanatakiwa kuwa na nidhamu ya mchezo wacheze kwa uangalifu na pia kupunguza makosa ambayo yanaweza kuwagharimu kwangu naona hili pambano litakuwa na burudani kubwa,” amesema Tegete.
Amesema wachezaji wa Yanga wanatakiwa kutambua wazi kuwa taji lililobaki msimu huu ni hilo hivyo wanatakiwa kupambana na kulinyakuwa ili kuweza kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa ambapo bingwa atashiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika.
“Hii ndio nafasi waliyokuwa nayo Yanga wamelikosa taji la Ligi Kuu sasa huku wanatakiwa kupambana ili kutwaa ubingwa wa kombe hili msimu huu,” amesema Kocha huyo ambaye ni baba mzazi wa Straika wa zamani wa Yanga Jeryson Tegete.

Advertisement