Tatizo la Aishi Manula liwekwe hadharani

Saturday November 9 2019

 

By Ezekiel Kamwaga

KATIKA mchezo wa soka, tukio la mchezaji nyota wa kikosi cha timu kuachwa kuitwa kikosini ni cha kawaida. Limeshawahi kutokea kwa wachezaji mbalimbali huko nyuma na litaendelea kutokea. Ndivyo mchezo ulivyo.

Sababu zinaweza kuwa za kueleweka na kuelezwa au ngumu kueleweka. Ndiyo sababu, mara zote kumekuwa na habari kubwa wakati matukio ya namna hii yanapotokea.

Luiz Felipe Scolari aliwahi kufanya kwa Romario alipokuwa Kocha Mkuu wa Brazil. Alimwondoa kwenye kikosi mchezaji aliyekuwa kipenzi cha wengi ndani na nje ya timu.

Nahodha wa muda mrefu wa England, Tony Adams, aliyeweka rekodi ya kuichezea taasisi hiyo kwa muda wa miongo mitatu tofauti (miaka ya 80, 90 na 2000) Aliachwa katikati ya miaka ya 1990 na England ikashtuka.

Chama cha Mpira wa Miguu England kilijikaza kisabuni kutoa taarifa lakini mwishoni ikabidi taarifa itolewe na wakasema tatizo ni kwamba Adams alikuwa na shida ya ulevi na alikuwa kwenye tiba.

Kwamba ingawa bado alikuwa na kiwango kizuri, uwepo wake kambini na wenzake ungeweza kuathiri ustawi wa timu na ukuaji wa wachezaji vijana.

Advertisement

Kwa Romario na wengine utakuta walimu walikuwa wanahofia wachezaji wenye vinyongo na kununa kwenye timu.

wakati wa ukocha wa Marcio Maxime, kulikuwa hakuna nafasi kwa Haruna Moshi ‘Boban’ na Athumani Chuji. Tulisikia kwamba walidaiwa kwa matatizo ya utovu wa nidhamu wakati huo.

Nimeanza kuona kwamba jambo la kutoteuliwa kwenye timu ya Taifa kwa mlinda mlango namba moja wa Simba SC, limeanza kuleta shida mitaani na kwenye vyombo vya habari.

Inaonekana kwamba Kocha Mkuu, EtienenNdayiragije na benchi lake la ufundi wameshafanya uamuzi kwamba hawamhitaji Manula kwenye kikosi cha Taifa Stars. Nadhani hii ni mara ya tatu sasa wanamtosa.

Manula anajulikana kama pengine ndiye mlinza mlango bora zaidi hapa nchini kwa sasa. Suala la yeye kukaa benchi halieleweki vizuri na sasa kuna minong’ono mingi mtaani kuhusu kiini cha tatizo hili.

Ni muhimu sana kwa FA au Ndayiragije kutoa taarifa sahihi na mapema kuhusu suala la Manula. Kama ni jambo la kusaidiwa, kama ilivyokuwa kwa Tony Adams wa Arsenal na England, asaidiwe.

Kama ni jambo ambalo anatakiwa kuomba msamaha kwa wenzake, benchi la ufundi na Tanzania kwa ujumla - atakiwe kufanya hivyo na kisha maisha yaendelee.

Ukimya huu hausaidii pande zote. Sana sana unachochea tu kiwanda cha umbea na minong’ono kisicho na faida kwa mchezaji binafsi wala Taifa Stars.

Washabiki na wapenda mema kwa Taifa Stars wangetamani sana kama akili yetu yote ingejielekeza kwenye kujiandaa na mechi kubwa zinazoikabili timu katika siku za karibuni.

Na uwe utaratibu wa kawaida tu kwamba kama kuna mchezaji muhimu hapangwi au haitwi kwenye timu, basi sababu ziwekwe wazi ili asaidiwe au angalau kuwe na ufahamu wa aina moja wa nchi nzima kuhusu mchezaji mmoja.

Waswahili wana msemo kuwa “Miluzi mingi hupoteza mbwa” na hivyo ni muhimu kutengeneza sauti moja ya hakika kwenye masuala yanayogusa hisia za washabiki kama jambo hilo la kutoitwa kwenye timu kwa mtu ambaye wengi wanadhani anastahili kuitwa kikosini. Walau kuitwa tu.

Wakili wa shetani

Wiki hii nimebaini kwamba wengi wa washabiki wa mchezo wa soka hapa nchini hawana imani na makocha wazawa.

Nilijaribu kujenga hoja kwenye mitandao ya kijamii kwamba huu ni wakati ambapo vilabu vyetu vikubwa vinatakiwa kuanza kuwaamini na kuwapa kazi makocha wazawa.

Nilichobaini ni kwamba ni afadhali Watanzania uwape raia wa nchi ya kigeni mwenye vyeti sawa na mzawa awe kocha wa timu yao kuliko Mtanzania.

Nadhani, kwa hakika kabisa, kama Watanzania wangemudu kwenda nje kutibiwa afya zao, hakuna ambaye angekubali kutibiwa hapa nyumbani kwa sababu madaktari wetu hawaaniniki pia.

Hili lipo hata kwenye shule. Kama Watanzania wote wangekuwa na uwezo wa kusomesha watoto wao nje ya nchi, sidhani kuna ambaye angetaka mtoto wake asomee hapa na sababu ingetolewa kwamba walimu hakuna hapa kwetu.

Hili ni jambo ambalo sasa nimelibaini kwamba ni tatizo kubwa. Najua bado kuna safari ndefu kufika tunapotaka lakini ni muhimu kuwapa nafasi watu wetu washindwe kwanza ndiyo tujue hatuwezi.

Kizazi cha akina Fred Minziro, Charles Boniface Mkwassa, Jamhuri Kihwelo kinaanza sasa kubadilishwa na akina Selemani Matola, Bakari Shime, Maka Malwisi, Mecky Mexime, Shadrack Nsajigwa na naambiwa akina Nico Nyagawa sasa wameanza kujitosa kutaka kupata vyeti vya juu vya ukocha.

Mimi naamini kabisa kwamba wachezaji kama Juma Kaseja, Haruna Moshi, Kali Ongalla na wengineo wana maarifa, uelewa na vipaji vya kuwa makocha wa wachezaji wetu kwa miaka mingi ijayo.

Nafahamu kuwa tuna matatizo katika eneo hilo lakini tumeshatumia sana walimu wa kigeni na hatujapiga hatua kubwa sana.

Tunatakiwa sasa kutoa fursa kwa walimu wetu kufundisha timu hizi na kutengeneza vijana wengine wazuri zaidi kuwa makocha.

Kwa kufanya hivi nafahamu nakuwa Wakili wa Shetani yaani nashadahia jambo ambalo kwa wengi halikubaliki, lakini wenzetu wote waliofanikiwa michezoni walipitia njia hii.

Nani katuaminisha kwamba sisi hatuna tunaloweza?

Advertisement