Tarimba ajitosa ubunge Kinondoni

Muktasari:

Tarimba amekuwa mwanachama wa kwanza wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kupeperusha bendera katika kinyang'anyiro cha ubunge wa jimbo hilo.

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Abbas Tarimba leo Jumanne amechukuwa fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania ubunge wa Jimbo la Kinondoni katika uchaguzi mkuu wa nchi utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Tarimba amekuwa mwanachama wa kwanza wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kupeperusha bendera katika kinyang'anyiro cha ubunge wa jimbo hilo.

Abbas alifika kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Kinondoni saa 1:55 asubuhi na alikuwa mtia nia wa kwanza kufika katika ofisini hizo zilizopo Kinondoni ambazo zinazohudumia watia nia wa chama hicho katika majimbo ya Kinondoni na Kawe.

Ilipofika saa 2 kamili milango ya ofisi hizo ilifunguliwa na Tarimba alifuata taratibu zote na kupatiwa fomu kisha kuondoka nayo.

Saa 3:16, Tarimba alirejesha fomu hiyo baada ya kuijaza na hivyo kuwa mgombea wa kwanza wa ubunge wa jimbo hilo kurejesha fomu.

"Kugombea ni haki ya kila mwana CCM, nimekuwa nikijipima siku zote nimeona ninatosha kuwa kiongozi wa jimbo hili, mimi ni mkazi wa Kinondoni nimekuwa diwani kwa miaka 10 na nimekuwa kiongozi katika chama kwa ngazi mbalimbali tangu 2020, " amesema Tarimba akiwa katika ofisi za chama hicho.

Mara baada kurejesha fomu Tarimba amesema amerejesha upesi fomu hiyo kwakuwa haikuwa na dodoso refu naye anakaa jirani na ofisi hizo.

Tarimba amewahi kuwa Katibu Mipango wa Yanga mwaka 1992, kisha Mwenyekiti muda na kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo mpaka mwaka 2003.

Mbali na kuongoza Yanga katika nafasi tofauti, Tarimba aliwahi kuongoza Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa miaka minne, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Michezo kwa miaka mitano na Mjumbe wa baraza hilo.