Tanzania yafanya kweli tenisi Afrika

Muktasari:

  • Kocha wa tenisi na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo, Riziki Salum alisema wanatarajia idadi ya wachezaji watakaofuzu hatua ya robo fainali kuongezeka kutokana na ubora wa wachezaji wa Tanzania.

Dar es Salaam. Dar es Salaam. Timu ya Tanzania imesonga mbele katika mashindano ya tenisi ya Afrika, baada ya wachezaji Rashid Ramadhani na Kanuti Alangwa, kufuzu hatua ya robo fainali kwenye viwanja vya Klabu ya Gymkhana, Dar es Salaam.

Ramadhani jana alitinga hatua hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa seti 2-0 katika mechi za mtoano dhidi ya Jafari Hemed wa Somalia akipata ushindi 6-1, 6-1.

Wakati Alangwa yeye aliibuka kinara mbele ya Salum Mtahasi wa Burundi kwa kumfunga seti 2-0 akipata matokeo ya 6-3, 6-2 kwenye mashindano hayo yanayoshirikisha wachezaji kutoka nchi 11 za Afrika.

Alangwa alisema licha ya kushinda mchezo huo, Mtahasi mwenye miaka 16 alicheza kwa kiwango bora na haikuwa kazi rahisi kupata matokeo mazuri.

“Unajua akili iliyonijia ya kumpigia mipira ya kustukiza mpinzani wangu upande wa kushoto na kulia ndiyo iliyofanya niweze kupata ushindi katika seti ya pili ya 6-2,”alisema Alangwa.

Kocha wa tenisi na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo, Riziki Salum alisema wanatarajia idadi ya wachezaji watakaofuzu hatua ya robo fainali kuongezeka kutokana na ubora wa wachezaji wa Tanzania.

“Tuna nafasi ya kufanya vizuri na kubakiza kombe hili nyumbani, kwa morali ya vijana wetu na maandalizi mazuri waliyopewa, hakuna shaka kombe litabaki,” alisema Riziki.

Katika mchezo mwingine Derick Ominde wa Kenya alitinga nusu fainali baada ya kumshinda Joseph Junior akitokea Rwanda 6-2,6-2.

Ominde alisema uzoefu wa mashindano hayo ulimpa fursa ya kupata ushindi ingawa alikiri Junior alionyesha mchezo mzuri.

Mchezaji mwingine kutoka Kenya aliyetinga nusu fainali ni Kaeli Shah aliyemshinda Ahmed Mandour kutoka Sudani kwa 6-2,6-1.

Upande wa wasichana Victoria Ndosi alifuzu robo fainali baada ya kumshinda Yasmini Grandi akitokea Somali kwa 6-0,6-0.