Tanzania kutumia Sh3 bilioni Afcon

Muktasari:

Fainali hizo zimepangwa kuanza Aprili 14 hadi 28 na zitahusisha nchi nane za Afrika ambazo ni Tanzania, Nigeria, Morocco, Angola, Uganda, Guinea, Cameroon na Senegal.

Dar es Salaam.Zikiwa zimebaki siku 30 kabla ya kuanza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, mashindano hayo yanatarajiwa kutumia Sh3.8 bilioni.

Fainali hizo zimepangwa kuanza Aprili 14 hadi 28 na zitahusisha nchi nane za Afrika ambazo ni Tanzania, Nigeria, Morocco, Angola, Uganda, Guinea, Cameroon na Senegal.

Mtendaji mkuu wa mashindano kwa upande wa Tanzania, Leslie Liunda alisema fedha hizo zimepungua kutoka bajeti ya awali ambayo ilikadiriwa kuwa Sh5.6 bilioni.

Liunda alisema bajeti hiyo haihusiani na maandalizi ya timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’.

"Serengeti katika maandalizi yao bajeti yake Sh1.6 bilioni bahati nzuri TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) wamesema bajeti hiyo ibaki kwao na Serikali ibaki na ile ya mashindano Sh3.8 bilioni," alisema Liunda.

Liunda alisema ana matumaini fainali hizo zinazoandaliwa na Serikali zitafanyika kwa kiwango bora kwa kuwa maandalizi ya miundombinu na mambo mengine yanakwenda vizuri.

Mtendaji huyo alisema aliyekuwa rais wa TFF Jamal Malinzi alipotuma CAF maombi ya kuandaa fainali hizo, aliomba ruhusa kutoka Serikali ambayo ilimpa baraka za kuandaa.

"Kitu kilichomleta Tanzania Ahmad Ahmad (rais wa CAF) ilikuwa ni kuja kutia saini makubaliano na Serikali, TFF haiwezi kuwa na fedha ya maandalizi zaidi ya Serikali.

"Bahati nzuri Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) ametuhakikishia mashindano yatafanyika, Serikali kwa namna inavyojua kwa kushirikiana na wadau wengine naamini yatafanyika kwa kiwango cha juu,” alisema Liunda.

Pamoja na Serikali kutoa fedha za maandalizi, Liunda alitoa rai kwa wadhamini wengine kujitokeza kudhamini katika maeneo tofauti kupitia Kampuni ya Lagardere iliyopewa na CAF mamlaka ya kusimamia matangazo katika fainali hizo.

‘Ingawa CAF imeipa Lagardere mamlaka ya matangazo, lakini atakayehitaji anaweza kwenda kwao na wao wakawapeleka kwenye kampuni hiyo. Taarifa zote kuhusu makubaliano yao yatakuwa wazi CAF watajua na sisi tutajua pia lengo ni kuhakikisha yale yaliyomo ndani ya mkataba yanatekelezwa,” aliongeza Liunda.

Viwanja

Akizungumzia viwanja, Liunda alisema vitakavyotumika Uwanja wa Taifa na Azam Complex ambavyo alisema vinaendelea kuboreshwa katika maeneo mbalimbali.

Alisema vitakavyotumika kwa mazoezi ni JK Youth Park, Uhuru, Gymkhana, Azam Complex (uliopo pembeni ya uwanja wa mkubwa wa Chamazi) na Uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Hopac.

"Uwanja wa Uhuru tulitaka utumike katika mechi, lakini CAF walishauri majukwaa ya kawaida nayo yaboreshwe. Hatukuwa na fedha ya kutosha. Fedha ilitosha kubadili kapeti la uwanja, zoezi ambalo linaendelea," alisema Liunda.

Mtendaji huyo amepongeza wamiliki wa Azam Complex kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuboresha miundombinu ya uwanja kwa kutumia fedha zao.