Tambwe ni kupiga mabao tu uarabuni

Aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga na Simba Amissi Tambwe akitambulishwa rasmi katika klabu yake mpya ya Fanja ya Oman

Muktasari:

Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Mrundi Amissi Tambwe amesema, atahakikisha anarejesha makali yake ya kutupia mabao kwa wingi ndani ya kikosi chake kipya cha Fanja FC.

MKALI wa mabao wa Simba na Yanga, Mrundi Amissi Tambwe amesema, anakwenda kurudisha heshima yake ya kupachika mabao uarabuni ambako amejiunga rasmi na kikosi cha Fanja FC kwa mkataba wa miaka miwili.
Tambwe ambaye amejiunga na kikosi hicho leo Ijumaa ni siku ya pili baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga.
"Ndio nimejiunga na Fanja kwa sasa ni siku ya pili. Kiujumla mazingira ya hapa bado sijayajua lakini ninachokiamini kwenye akili yangu ni kucheza kwa nguvu na kujituma katika kiwango bora,"alisema Tambwe.
Amesema, kutokana na namna alivyopokelewa anaamini kila kitu kitakwenda sawa kwenye timu hiyo.
Mshambuliaji huyo aliyecheza Ligi ya Tanzania kwa kipindi kirefu na akawa na wakati mzuri ndani ya kikosi cha Simba baada ya kumaliza akiwa mfungaji bora wa msimu wa 2013-2014.
Hata hivyo, akiwa mfungaji bora Simba walimwacha kwenye dakika za mwishoni na Yanga ikamsajili akaichezea kwa kipindi hicho hadi msimu wa 2018-2019 ulimalizika, akarudi nyumbani kwao kwa mapumziko na juzi akatambulishwa Fanja FC.
Akiwa na Yanga msimu wa 2015-2016, aliibuka mfungaji bora na kufanya kuweka rekodi ya kuwa mfungaj bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili akiwa na timu mbili tofauti za Simba na watoto hao wa Jangwani.